Na Mwandishi Wetu – DAR ES SALAAM
Wakati Serikali ikitanfaza msako kwa watu walioghushi vyeti na kutumia majina ya watu wengine, Waziri wa mambo ya ndani ya Nchi, Mwigilu Nchemba, ameibuka na kutoa ufafanuzi wa utata wa majina yake.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuibuka kwa mjadala wa usahihi wa majina yake pamoja na kuhusishwa kughushi vyeti ya elimu.
Katika andiko lake aliloliweka jana katika mitandao ya kijamii ambalo baadaye lilithibitishwa na mmoja wa wasaidizi wake, Mwigulu alisema watu wanaoandika historia yake hawamjui kwani uhalisia alikuwa akiitwa Lameck Madelu Mkumbo, sasa Lameck si jina la Kinyiramba na Madelu si jina halisi la baba yake bali la utani.
“Ni vema kuweka rekodi sawa, kwanza anasema (aliyeandika) nilikuwa naitwa Lameck Madelu Mkumbo, sasa moja Lameck sio jina la kinyiramba, na Madelu sio jina halisi la baba bali ni utani kuwa ana ndevu nyingi, yaani ni mandevu. Ndiyo maana hata kwenye ubunge nililiongeza tu kama a.k.a ili watu, hasa wazee wanifahamu, hili haliko kwenye vyeti.
“Hili la Lameck siyo jina la Kinyiramba ni jina la daktari aliyenipokea zahanati iliyopo Kijiji cha Mukulu, daktari tunaita hivyo, lakini ni nesi ndiye aliyekuwa anaitwa Mwigulu na jina la kizungu Lameck.
“Mimi nilipelekwa hospitali nikiitwa Mugulo na jina la ukoo kwa watoto wote wa kiume ni Shumbi, ambalo hata hivyo wanatumia wazee tu, wanaojua Kinyiramba hilo ndio jina la Kinyiramba,” alisema Mwigulu na kuongeza:
“Mama yangu aliulizwa jina akanitaja kwa muuguzi (nesi) akamwambia mama unamwitaje jina hilo hakuna lingine, mama akamwambia hakuna labda mtaje wewe, basi jamaa akajitaja,” alisema.
Alisema suala hilo ni jambo la kawadai hasa kwa kijijini kwani familia inakuwa na watoto wengi hadi majina inakuwa si jambo la kujali.
“Hata pale kijijini kuna wengine waliotajwa majina ya waganga wa kienyeji wazee walikopewa dawa, majina ya manesi, matabibu kama mimi, majina ya walimu,” alisema.
Akizungumzia maisha yake ya elimu, alisema aliacha shule kwa mara ya kwanza mwaka 1984 baada ya kuanza na kaka yake aliyemtaja kwa jina la Jugulu.
Mbunge huyo wa Iramba alisema kutokana na hali hiyo, baba yao aliwataka wapeane zamu ya kwenda shule hali iliyomfanya aache shule.
“Mwaka 1985, nikaachia darasa la tano nikaenda kuchunga miaka kama miwili. Nikarudi tena baada ya mifugo kuanza kufa sana, mzee akashauriwa awekeze kwenye elimu. Walimu walikuwa wanashinda nyumbani kumsihi anirudishe shule, ndiyo nikarudi na nikachukua majina ya daktari.
“Mtu asichanganye kuona ni udanganyifu, mimi sijachukua vyeti vya mtu. Nimefanya mitihani tena kwa kupiga na picha za passport ili mtu asitumie haki ya mtu mwingine aliyefaulu na mpaka sasa naona ni struggle (kupambana) za mfano, kuwa nilisoma kwa mazingira ya kutoka kuchunga na kurudishwa shule na kufaulu mwenyewe,” alisema Mwigulu.
Waziri huyo alisema kwa anayetaka kuthibitisha maelezo aliyotoa, anaweza kuwauliza aliosoma nao shule ya msingi.
“Comrades kwa mawazo yangu kosa ni mtu kuchukua nafasi ya mtu aliyefaulu na kwenda yeye, hapo ni kuiba haki ya mtu. Najua hii ilikuwa ikitokea baadhi ya maeneo, mtu anafaulu ila anakuwa hataki kwenda shule au amefariki then anakwenda mwingine. Mimi sijawahi chukua nafasi ya mtu.
“Halafu watu wanasema jina la mtu, labda kama wanamaanisha tofauti na wizi wa jina kwani kila mmoja hapo alipo ana jina la mtu, yaani atakuwa John wa Biblia, Mohamed wa Quran, litakuwa la babu, bibi la mganga, daktari, rafiki, kiongozi au hata la tukio.
“Nijuavyo jina unakula kiapo tu kama sio la kwako kisheria na unatumia, na hata sasa nikitamani jina jipya nakula kiapo na kutangaza katika Gazeti la Serikali na lisipopingwa ndiyo linakuwa jina langu jipya.
“Hoja ni kama mtu kapora cheti cha mtu, kapora nafasi ya mtu mwingine aliyefaulu akaenda kuisomea yeye. But, things do change pia kutokana na nyakati na mazingira,” alisema Mwigulu.