30.3 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

VIWANJA 50 VYA NDEGE HAVINA HATI MILIKI

Na BENJAMIN MASESE-MWANZA           |          


MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), imesema viwanja vingi vya ndege vimeshindwa kupata hati miliki kutokana na wananchi kuvamia maeneo hayo na kusababisha migogoro ambayo ipo kwenye vyombo vya uamuzi.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mtendaji Mkuu wa TAA, Richard Mayongela, wakati akimwelezea hali ya sekta hiyo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwele, wakati wa majumuisho ya waziri huyo mkoani Mwanza.

Alisema kati ya viwanja vyote 58,  vilivyo na hati ni vinane tu na kutokana na hali hiyo, TAA imeanza kushughulikia migogoro hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambapo hadi sasa viwanja vingine vinne vipo katika hatua ya mwisho kupewa hati miliki na kufikisha idadi ya 12 kati ya 58.

Mayongela alisema mkakati wao ni kuhakikisha viwanja vyote nchini vinakuwa na hati miliki na ikiwezekana kuwekewa uzio ili kuepusha tena migogoro ya uvamizi.

“Nitumie fursa hii kuwasilisha kwako waziri changamoto zinazotukabili TAA, kwanza tumezoea kuitwa mamlaka lakini hatujapata nguvu hiyo bali kisheria tunatambulika kama wakala, sasa kutokana na hali hiyo tunashindwa kuwa na mamlaka kamili ya maamuzi, ikiwa tutapata mamlaka hayo tutaongeza utendaji zaidi.

“Tunakuomba ukiwa unapitia nakala  ofisini kwako ukifika kwetu umalizie vipengele kadhaa ili tuwe na mamlaka kamili, jambo lingine ni masilahi kwa wafanyakazi ni madogo mno kwani muda mrefu hayajaboreshwa jambo ambalo linasababisha hata morali ya watumishi kupungua, lakini tunamshukuru Rais Dk. John Magufuli, ameonyesha dhamira ya dhati katika kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege.

“Lipo jambo la kuboresha baadhi ya viwanja vyetu ili kuwa vya kimataifa kwani hata ndege kubwa ya Dreamliner iliyokuja hivi karibuni inatua katika viwanja vichache kama Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza, hivyo inatubidi kuendelea kuboresha na kuwa na hadhi ya kimataifa, pale Dodoma ambapo ndio makao makuu, tunatarajia kufanya maboresho ya uwanja wa Msalato ili kuwa wa kimataifa,” alisema.

Mayongela alimwomba Waziri Kamwele kusaidia kukamilisha mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Songwe ambao umechukuwa muda mrefu ili huduma ziweze kuendelea huku akitoa wito kwa Watanzania wote kuitunza miundombinu inayojengwa kwani fedha zinazotumika ni kodi ya Watanzania.

Pamoja na hayo pia aliainisha viwanja vingine vinavyofanyiwa ukarabati ni  uwanja wa Kigoma, Musoma, Bukoba, Shinyanga huku akisisitiza sekta ya ujenzi na uchukuzi inaendelea kuimarika.

Kuhusu changamoto, Mayongela, alizitaja baadh ikiwamo magari ya zimamoto ambayo alisema kukosekana katika baadhi ya viwanja kunasababisha kutokuwa na huduma ya ndege.

Alisema hadi sasa wana gari 10 mpya ambazo zilinunuliwa katika bajeti ya 2016/2017, 2017/2018.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles