Na Sheila Katikula, Mwanza
Serikali imekusanya zaidi ya Sh million 900 kutokana na madeni ya kodi ya ardhi kwa wadaiwa sugu huku viwanja 421 vikitarajiwa kuuzwa baada ya wamiliki wake kushindwa kutekeleza wajibu na kukaidi matakwa ya kisheria ya kulipia kodi viwanja hivyo.
Hayo yameelezwa na Kamishina wa ardhi Msaidizi Mkoa wa Mwanza, Elia Kamihanda wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mwendelezo wa kukusanya fedha hizo za kodi kutoka kwa wadaiwa hao mkoani hapa.
Alisema kesi za wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi 736 zilizosikilizwa na baraza la ardhi la nyumba na wilaya Machi 12 mwaka huu kwani amri ya mahakama iliwataka wananchi kulipa madeni yao.
“Tangu kipindi cha kesi hizo mpaka hivi sasa viwanja vilivyopelekwa mahakamani vya jijini na manispaa ya Ilemela tufalikiwa kukusanya sh Milioni 900 tofauti na matarajio ya idadi ya wananchi wanaodaiwa kwani amri ya mahakama imewataka wamiliki hao walipe kodi kwa kipindi cha siku kumi na nne na muda huo umepita na kuna baadhi yao hawajalipa.
“Kampuni ya madalali wa Rock City Tackers ya mkoani hapa imepewa jukumu la kufuatilia mali za wadaiwa sugu na itaanza rasmi kazi ya kukamata mali hizo ili kuhakikisha madeni ya serikali yanalipwa kwani Mei 7 mwaka huu tutauza kwa njia ya munada viwanja vya viwanda vinne vilivyopo kwenye halmashauri ya Magu kwani amri wazilizotolewa zimehusisha viwanja vyote vilivyopelekwa mahakamani,” alisema Kamihanda.
Hata hivyo amewataka wananchi waliofikishwa mahakamani ambao walipewa amri ya kulipa kodi hiyo na hawajatekeleza agizo hilo wanapaswa kutambua dalali ameanza kutekeleza rasmi wajibu huo ambapo jumla ya viwanja 421 vitauzwa kwa amri ya mahakama kwa sababu ya wamiliki kushindwa kulipa madeni yao.
“Wamiliki hao waliofikishwa mahakamani ni wadaiwa sugu kwani wamekaa muda mrefu na madeni hayo wapo wenye madeni ya miaka mitano, sita hadi kumi kwa mujibu wa sheria ya ardhi inampelekea kuwa mdaiwa sugu wa kodi hii kwa sababu anatakiwa kila mwaka wa fedha anatakiwa kutimiza wajibu huo,”alisema Kamihanda.
Kamihanda amewakumbusha wamiliki wa ardhi kulipa kodi kwa mujibu wa sheria ili kuepuka usumbufu unaojitokeza kiasi cha kupelekea hatua za kisheria kuchukuliwa.