Waandishi wetu, Dar es Salaam
UGAWAJI wa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo wakiwamo wamachinga, mama na baba lishe, linaendelea katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar as Salaam, huku ikielezwa kuwa wajasiriamali wapya wameibuka wakitaka vitambulisho hivyo.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti Jana, wafanyabishara hao wameunga mkono hatua hiyo ambayo wanaona inaweza kutatua kero za wafanyabiashara hao na mgambo wa Jiji.
“Tunamshukuru Rais Dk.John Magufuli kutupa vitambulisho hivi ambavyo vitasaidia kutatua mgogoro wetu na mgambo wa jiji ambao walikua wanatusumbua,” alisema Khamis Juma mfanyabiashara wa nguo solo la Kariakoo.
Alisema mpaka sasa wamachinga wengi wamehamasisha kujitokeza na kujiandikisha kila mmoja aweze kupata kitambulisho chake.
Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wamachinga Kariakoo (Kawasso), Namoto Yusuph, alisema hatuahiyo inaendelea vizuri na kuna ongezeko la wamachinga wapya waliokuja kujiandikisha.
“Tangu tuzindue hatua hii, kuna ongezeko kubwa la wamachinga wapya waliokuja kujiandikisha ofisini kwetu, kila mmoja anataka kitambulisho,” alisema Yusuph.
Katibu Tawala wa Manispaa ya Ilala, Sheila Lukuba, alisema mpaka sasa wamekwisha kutoa vitambulisho zaidi ya 3,000 na hatua inaendelea.
Alisema pia wameweza kuandikisha wafanyabiashara wapya kuhakikisha wanasajiliwa na kupatiwa vitambulisho.
“Bado tunaendelea na hatua ya uandikishajii wa wafanyabiashara waweze kupatiwa vitambulisho jambo ambalo linaweza kuwasaidia wafanyabiashara kutambulika katika sherià,” alisema Lukuba.
Alisema baada ya kupata vitambulisho hivyo wafanyabiashara hao wataweza kulipa kodi stahiki ya Serikali na kuongeza mapato.
Alisema ikiwa watakamilisha ugawaji wa vitambulisho, watalazimika kushirikiana na watendaji wa kata kuhakikisha wanawasajili wafanyabiashara wanaoendesha shughuli zao mitaani.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo, alisema hatua hiyo inaendelea vizuri kwa kuwaandikisha wafanyabiashara na aina ya biashara zao waweze kuwatambua na kuwapa vitambulisho.
“Kwa sasa tunamalizia kuwaandikisha wafanyabiashara wa Mwenge waweze kupata vitambulisho, tukimaliza tutaanza mtaa kwa mtaa kuhakikisha wote wanatambulika na aina za biashara hao,” alisema Chongolo.
Manispaa ya Ubungo imezindua hatua hiyo katika soko la Mawasiliano ili kuwapa vitambulisho wafanyabiashara wa manispaa hiyo.