Na Mwandishi Wetu, Manyoni
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema kumekuwapo na mafanikio katika vita dhidi ya majangili kwenye hifadhi za taifa na mapori ya akiba.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, majangili walivamia kwa kasi na kuwaua wanyamapori wakiwamo tembo na faru, hatua ambayo iliibua tishio la kutoweka kwa baadhi ya wanyamapori.
Juzi Waziri Nyalandu alitangaza kukamatwa kwa silaha za kivita zikiwamo bunduki za AK 47 na SMG katika Pori la Akiba la Rungwa lililopo katika wilaya za Manyoni na Chunya.
Silaha hizo zimekamatwa kutoka mikononi mwa majangili, ambapo katika msako huo, majangili 10 yalikamatwa kabla ya kukamilisha mipango ya kuua tembo.
Akizungumza baada ya kukagua silaha zilizokamatwa, Waziri Nyalandu alisema Serikali kamwe haitarudi nyuma hadi majangili wasalimu amri.
Alisema kukamatwa kwa shehena ya silaha hizo zikiwamo na kivita ni salamu kwa majangili.
Nyalandu alisema hakuna jangili ambaye atakuwa salama iwapo hataweka silaha chini na kuwa Serikali lazima ishinde.
Kaimu Meneja wa Pori la Rungwa, Kwaslema Male, alisema silaha hizo zimekamatwa katika kipindi cha kuanzia Januari 2012 hadi Aprili, mwaka huu, huku idadi kubwa zikiwa zimekamatwa mwanzoni mwa mwaka huu.
Alizitaja silaha hizo na idai kwenye mabano kuwa ni AK 47 (2), SMG (3), Bastola (38), gobore (263), risasi za AK 47 (28), risasi za SMG (823) na misumeno ya kukatia miti kwa ajili ya mbao (197).