26.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Visa vya unyanyasaji kingono kwa wanawake wenye ulemavu

visa-vya-unyanyasaji-kingono-kwa-wanawake-wenye-ulemavuNa Sussan Uhinga, Tanga

NI ukweli usiopingika kwamba wanawake ndio wanafahamu changamoto za utunzaji na ustawi wa familia.

Kwa wanawake walemavu wengi wameonekana kusahaulika hasa katika ushirikishwaji wa masuala ya msingi kama vile elimu na shughuli mbalimbali za kitaifa.

Kulingana na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu, unaeleza kuwa ubaguzi dhidi ya mtu yeyote kwa msingi wa ulemavu ni uvunjaji wa hadhi ya asili na thamani ya nafsi ya binadamu.

Hata hivyo licha ya kuwapo kwa mikataba mbalimbali, bado watu wenye ulemavu wameendelea kukabiliwa na vikwazo mbalimbali hasa kwa wanawake ambapo wengi wamekuwa wakifanyiwa unyanyasaji wa kijinsia.

Unyanyasaji wa kingono ni aina ya ubaguzi wa kijinsia. Ni unyanyasaji wa kingono na ubaguzi kama mtu anarudia rudia kusema au kufanya mambo ya kutukana au ya kukera. Inaweza kuwa maneno au vitendo ambayo yanahusiana na ngono au jinsia.

Katika makala haya tutaangazia unyanyasaji wa kingono wanaokutana nao wanawake wenye ulemavu wanapokuwa katika mahusiano ya kimapenzi au ndani ya ndoa.

Imekuwa ni jambo la kawaida katika jamii kuona mwanamke mlemavu ana idadi kubwa ya watoto huku wengi wakiwa ni wa baba tofauti.

Licha ya kuwa na idadi kubwa ya watoto, wanawake wengi wenye ulemavu pia wametelekezwa na kuachwa wakihangaika na mzigo mkubwa wa kutunza familia.

Mariam Siafu (56) mkazi wa Kisosora Jijini Tanga, ni mmoja wa wanawake wenye ulamavu anasema ukatili unaofanywa na wanaume dhidi yao ni suala la enzi na enzi kwani lipo kwenye jamii lakini wanawake ambao ndio wahanga hawalipigii kelele ili wanaume wa kizazi cha sasa waachane na tabia hiyo.

Mariam ambaye ana watoto watatu aliozaa na baba tofauti anasema; “Hakuna mwanamke anayependa kuzaa kila mtoto awe na baba yake lakini huku kwetu wanaume ni kama vile wanakuja kutuchunguza tuna maumbile ya kike kweli au vinginevyo lakini mapenzi hakuna.

Anaeleza kwa masikitiko kwamba wanaume huwafuata wanawake wenye ulemavu si kwa nia ya kuwa nao kimapenzi au kuwaoa bali kuwachunguza jinsia zao na hata wengine yawezekana wana imani za kishirikina.

“Nalazimika kusema hivi kwa sababu tangu nikiwa mdogo niliwahi kusikia kuwa wapo wanaume ambao huwatongoza wanawake wenye ulemavu kwa kuwalaghai na baada ya kukutana nao kimwili hutoweka bila kujali hisia za mwenzake.

“Wanawake wengi wenye ulemavu wamekuwa wakikumbana na changamoto ya kukimbiwa na wenza wao pamoja na kutelekezwa na watoto.

“Si siri mwanamume anakufuata kwa haja ya kutaka mahusiano ya kimapenzi lakini cha ajabu anataka mahusiano yenu yawe ya siri mno hata akikataa kabisa kuonekana yupo karibu na wewe kuwa jamii itamuelewaje,” anasema.

Anasema wapo wanaume wanaoamini wanawake wenye ulemavu hawana jinsi kama wanawake wengine huku wengine wakiamini kuwa wakishiriki tendo la ndoa na mwanamke mlemavu watafanikiwa.

“Mwanamume anakufuata tena anataka mkutanie nyumbani kwako kwa sababu hataki kuongozana na wewe kwenda hata nyumba ya kulala wageni,” anasema.

Kuwapo kwa imani hizo kwa wanaume katika jamii zetu kumesababisha wanawake wenye ulemavu kutelekezwa na watoto huku waliowapa mimba kukimbia wakiona aibu kuonekna kwamba amezaa na mlemavu.

“Ningefarijika sana kuona vipindi vya televisheni na redio vinapambana kuzungumzia suala hili kwa sababu kwa kuendelea kulifumbia macho litaathiri jamii yetu, mbali ya kuongezeka kwa watoto wa mitaani pia maambukizi ya Ukimwi yataongezeka,” anasema Mariam.

Anasema kumuacha aendelee kuishi katika mazingira hayo kutasababisha aishi maisha ya kimasikini kwani atakuwa anahangaika kulea watoto peke yake ili hali anakabiliwa na changamoto ya ulemavu.

Kwa upande wa Serikali, Mariam anaiomba itunge sheria kali kwa wanaume wanaowatelekeza watoto kwa kisingizio cha ulemavu au kazaa watoto walemavu.

“Serikali izisimamie sheria kwa wanaume wanaowatelekeza wanawake na watoto lakini pia wanaume wanaowapiga wanawake na kuwasababishia ulemavu wa viungo, sheria ikiwepo itasaidia kupunguza vitendo vya ukatili kwenye jamii dhidi ya wanawake,” anasema.

Haruna Jengo (42) anasema vitabu vya dini vimeelekeza kuwaoa wanawake wenye ulemavu na kwamba utakapomuoa unapata swawabu ya kwa Mungu.

“Dini imetuelekeza wanaume tuwaoe wanawake hawa lakini jamii nayo inaonyesha kumnyanyapaa mwanaume anaeonekana kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanamke mlemavu.

“Yaani ukionekana una mpenzi mlemavu labda wa miguu utasikia baadhi ya watu wanakukejeri kuwa wanawake wote waliojaa kwanini umuoe mlemavu kana kwamba umefanya kosa la uonevu vile,” anasema Jengo.

Naye Mashaka Mhando anasema suala la imani za kishirikina bado ni tatizo kwani wanaume wengine huamua kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanawake wenye ulemavu kwa kisingizio cha kupata mafanikio.
“Nimewahi kusikia toka enzi kuwa wanawake wenye ulemavu wana mafanikio ya kipekee hivyo inawezeakana baadhi yetu tunawafuata kwa tamaa tu za kujua kuwa kuna ukweli juu ya hilo,” anasema Mhando.

Anatoa rai kwa jamii kuondokana na dhana hiyo potofu na badala yake wanaume waone sasa ipo haja ya kuwapenda wanawake hao huku wakiwasaidia majukumu ya kutunza watoto.

Mariam ni mmoja tu kati ya wanawake walioonja mateso ya ukatili wa aina hii ambao unafanywa kwa siri tena kwa kuwalaghai wanawake hawa bila ya huruma kisha kuwakimbia.

Kwenye jamii yetu wapo wengi wanaokumbana na mateso haya ambayo yanafanywa na wanaume, ni wakati sasa wa kuungana kwa pamoja tupaze sauti kulikemea hili kwa nguvu.

Elimu ikitolewa, sheria zikashika mkondo wake kwa maana ya kuwapa adhabu wanaume wa aina hii ili kujenga jamii yenye upndo na usawa na isiyobagua watu wengine.

Tusiwanyanyapae wanawake wenye ulemavu wa miguu kwani wao hawakuomba kuzaliwa hivyo pengine ni mipango ya Mungu, anaweza akawa mama yako baba au dada yako je, ungefurahi afanyiwe vitendo hivyo?

Mariam ni mlemavu wa miguu lakini anakabiliwa na changamoto ya kukosa baiskeli hivyo anaomba msaada ili aweze kufanya shuguli zake za mama lishe kama zamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles