30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Viongozi wa dini watajwa mapambano dhidi ya TB 

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu  amesema   viongozi wa madhehebu ya dini na waganga wa tiba asili ni nguzo muhimu   katika kutokomeza   Kifua Kikuu(TB) nchini.

Ameyasema hayo mwishoni mwa wiki katika ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa wadau wenye lengo la ushirikiano katika kutokomeza   Kifua Kikuu (TB) nchini, uliofanyika  Dar es Salaam.

Waziri Ummy alisema waganga wa jadi na viongozi wa dini ni wadau muhimu katika mapambano dhidi ya   TB.

Alisema   utafiti uliofanywa 2018 na Mpango wa Taifa wa kudhibiti kifua kikuu na ukoma unaonyesha   waganga wa jadi wamekuwa waathirika wakubwa wa ugonjwa wa kifua kikuu.

Alisema   viongozi wa dini ni kundi jingine muhimu  katika mapambano dhidi ya   kifua kikuu nchini  kutokana na idadi kubwa ya waumini wanaowaamini katika kufikisha ujumbe.

“Waganga wa jadi ni wadau muhimu  katika mapambano ya kifua kikuu, utafiti wa 2018 uliofanywa na mpango wa taifa wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma unaonyesha  waganga wa jadi na wenyewe wamekuwa waathirika wa   kifua kikuu.

“… na viongozi wa dini tunawahitaji wanaposimama katika makanisa na katika misikiti yetu ili wawe wanawakumbusha waumini juu ya   Kifua Kikuu,” alisema Waziri Ummy.

Alisema mwaka 2017 Tanzania iligundua na kuwapatia matibabu takribani wagonjwa 75,000 ikiwa ni asilimia 44 tu ya wagonjwa wanaokadiriwa kuugua TB.

Alisema hiyo  ina maana  ya kuwa wagojwa 85,000 zaidi ya asimilia 50 hawagunduliwi na hivyo kukosa matibabu kila mwaka nchini.

Pia Waziri Ummy alisema  TB huathiri takriban watu milioni 10.4 duniani kila mwaka na asilimia 25 ya wagonjwa wanatoka barani Afrika. Tanzania ni miongoni mwa nchi 13 barani Afrika zenye kiwango kikubwa cha wagonjwa wa TB na inakadiriwa kuwa na  wagonjwa wapya wa TB 154,000 kila mwaka.

Alisema wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, imeendelea kutoa huduma za uchunguzi na matibabu bila malipo katika vituo vya kutolea huduma vya serikali na binafsi, hali iliyoleta mafanikio ikiwamo kuvuka malengo ya mwaka 2018 ambako walifikiwa  wagonjwa 75,845 ikiwa ni   ongezeko la asilimia 22 kutoka mwaka 2015.

  Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohammad Kambi, alisema Tanzania ina wastani wa wagonjwa 154,000 ambao wanatakiwa  kuibuliwa na kuanzishiwa matibabu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles