23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Vikosi vya Tigray vyaamriwa kujisalimisha ndani ya saa 72

ADDIS ABABA, ETHIOPIA

WAZIRI Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed ametoa muda wa saa 72 kwa vikosi vya jimbo la Tigray kusalimu amri kabla ya jeshi la serikali kuu halijaanza operesheni kubwa dhidi ya mji mkuu Mekelle.

Waziri Mkuu Ahmed alituma ujumbe jana akisema anautaka umma wa Mekelle kujinusuru kutokana na mashambulizi ya mizinga na kujikomboa kutokana na wanajeshi wa Tigray na baada ya hapo hakutokuwepo na huruma.

Katika ujumbe huo wa Ahmed, pia alitowa muda wa saa 72 kwa vikosi vya Tigray wajisalimishe akiwatanabahisha kwamba hawana namna tena.Ujumbe wake huo ulichapishwa katika ukurasa wa Twitta juzi Jumapili jioni.

Pamoja na ujumbe huo wa Ahmed, Msemaji wa Jeshi la Ethiopia, Dejene Tsegaye kwa upande mwingine alitoa maelezo kuhusu operesheni hiyo iliyopangwa dhidi ya mji mjii wa Tigray Mekelle. 

“Awamu zijazo ni sehemu muhimu ya operesheni ambayo inahusu kuuzingira mji mkuu Mekelle kwa kutumia vifaru na kumaliza mapambano katika maeneo ya milimani na kuingia katika uwanja wa mapigano,” alisema Tsegaye.

Operesheni hiyo kwa mujibu wa msemaji huyo wa jeshi la Ethiopia inalenga kuwalazimisha wanajeshi wa Tigray kujisalimisha. 

Hata hivyo vikosi vya Tigray vya kundi la TPLF bado havikuweza kupatikana haraka kutoa tamko kuhusiana na suala hilo, ingawa kundi hilo la ukombozi wa watu wa Tigray kaskazini mwa Ethiopia limesema vikosi vyake vinachimba njia za chini kwa chini na viko imara.

Kwa upande mwingine, Shirika la Habari la Reuters limefafanua pia kwamba haliwezi kuthibitisha juu ya matamko yaliyotolewa hivi karibuni kuhusu vita hivyo vya Tigray.

Ifahamike kwamba madai yanayoripotiwa kutoka pande zote mbili za mgogoro ni vigumu kuthibitishwa kutokana na kutokuwepo mawasiliano ya simu na mtandao.

Juu ya hilo inaelezwa kwamba vikosi vya jeshi la shirikisho vimeitwaa miji kadhaa baada ya kufanya mashambulizi ya anga na ardhini na sasa inaelezwa kwamba wanajeshi hao wanawania kuukamata mji mkuu Mekelle,mji ulioko milimani unaokaliwa na kiasi watu 500,000 na ambako ni makao makuu wa TPLF.

Kufikia sasa inaelezwa kwamba mamia ya watu huenda wameshauwawa na zaidi ya 30,000 wamekimbilia nchi jirani ya Sudan. Jumuiya ya kimataifa imetowa mwito wa kufanyika mazungumzo kuumaliza mgogo huo lakini waziri mkuu Abiy amekataa katakata kukaa na viongozi wa TPLF.

AP

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles