Winfrida Mtoi -Dar es salaam
LIGI Kuu Tanzania Bara, inatarajia kuanza hivi karibuni ikiwa ni hatua ya lala salama kwa msimu wa 2019/2020.
Timu 20 zinachuana katika ligi hiyo, huku Simba ikionyesha dalili zote za kutetea ubingwa wake, baada ya kujikusanyia pointi 71, wakati anayefuatia Azam ana pointi 54, zote zikicheza mechi 28, Yanga iliyopo nafasi ya tatu ina alama 51, ikicheza michezo 27.
Ikumbukwe kuwa, ligi hiyo ilisimama kutokana na agizo la serikali kwa tahadhari ya kuepuka maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa corona, tangu Machi 17, mwaka huu.
Katika kipindi hiki ambacho Ligi Kuu imesimama, kinachoendelea ni harakati za usajili ili kuimarisha vikosi kwa msimu ujao.
Hali hiyo inatokana na wachezaji wengi katika timu hizo, kumaliza mikataba yao mwisho wa msimu ambao ulitarajiwa kuwa mwezi huu.
Kama ilivyo kawaida, inapofika kipindi cha usajili, kuna timu ambazo huwa zinatolewa macho, kila mmoja akihitaji mchezaji kutoka huko.
Kinachochangia timu hizo kutazamwa zaidi hasa na klabu kubwa, ni viwango vilivyooneshwa na nyota wao katika kipindi chote cha ligi.
Mara nyingi timu zenye wachezaji wenye viwango vizuri, walioweza kutoa upinzani kwa vikosi vikubwa kama Simba na Yanga, ndio kimbilio la kila mmoja katika kipindi hiki cha usajili.
Kutokana na hilo, timu hizo inapofikia kipindi hiki huwa zinajiandaa kupoteza nyota wake wengi wanaohamia timu nyingine kutokana na kutangaziwa dau nono hasa kama wamemaliza mikataba kule waliko.
Kitendo hicho kinazifanya timu hizo, kusuka upya vikosi vyao katika msimu unaofuatia.
MTANZANIA linakupa baadhi ya timu ambazo zipo hatarini kuwakosa nyota wake wakali kutokana na kuanza kunyemelewa na klabu mbalimbali kipindi hiki cha maandalizi ya usajili wa msimu ujao.
Na tayari timu hizo zimeshajiandaa kuanza kusuka vikosi vyao upya ,endapo wachezaji wao wataondoka.
Namungo FC
Hii ni timu mpya katika Ligi Kuu, lakini imeonesha uwezo mkubwa na kuwapa upinzani wakongwe kutokana na ubora wa nyota wake.
Kikosi hicho kimefanikiwa kuingia Ligi kuu kwa kasi ya aina yake, hadi sasa kinachanua kikiwa katika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi na pointi zake 50.