26.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 12, 2024

Contact us: [email protected]

VIJANA WENGI WANAUGUA KIFAFA

NA VERONICA ROMWALD- DAR ES SALAAM

VIJANA wenye umri wa miaka 15 ndilo kundi linaloongoza nchini kwa kuugua  kifafa, imefahamika.

Vilevile, zaidi ya asilimia 24 ya wagonjwa wa kifafa wana ulemavu mwingine ambao wengi wao unatokana na kuangukia moto wakati mgonjwa anapopatwa na degedege.

Hayo yalielezwa Dar es Salaam  jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu

  katika taarifa yake iliyotolewa  na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Serikali kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Kifafa Duniani.

“Tanzania ina idadi kubwa ya wagonjwa wa kifafa katika bara la Afrika na duniani, mfano vijiji vya Mahenge idadi ya wagonjwa hawa ni kubwa ambako kati ya watu milioni moja kuna wagonjwa asilimia 37.5 wanaougua ugonjwa huu nchini,” alisema.

Alisema ugonjwa wa kifafa ni miongoni mwa sababu zinazochangia vifo nchini ukikadiriwa kuchukua nafasi ya saba hadi nafasi ya 15 kama kisababibishi cha vifo.

“Wagonjwa wa kifafa nchini wako katika hatari ya kifo mara sita zaidi ikilinganishwa na mwananchi wa kawaida katika  jamii.

“Zaidi ya asilima 60 ya vifo vinavyotokana na matatizo ya kifafa husababishwa na athari za ugonjwa wa kifafa moja kwa moja,” alisema.

Hata hivyo, alisema mambo mengi yanayosababisha kifafa yanazuilika kuanzia kuumia ubongo wakati mama anapojifungua, magonjwa yanayosababishwa na vijidudu kama  bakteria.

“Pia kwa sasa watu wengi wanaopata ajali za magari au bodaboda husababisha kuumia kichwani na ubongo kuathirika na hivyo kuugua kifafa,” alisema.

Aliongeza: “Wananchi wengi  bado wana mtazamo hasi kuhusu kifafa. Zaidi ya asilimia 36  bado  wanaamini kuwa ugonjwa wa kifafa unatokana na nguvu za giza au kurogwa na wengi wameufanya kuwa ugonjwa wa siri”.

Waziri Ummy alisema siku ya ugonjwa wa kifafa duniani huadhimishwa Jumatatu ya pili ya Februari kila mwaka. Kaulimbiu ya mwaka huu inasema: ‘Weka ugonjwa wa kifafa kwenye taswira’ ambayo imelenga kuhamasisha jamii kuutambua zaidi ugonjwa huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles