23.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Vijana wapewa mbinu kujikwamua kiuchumi

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Vijana nchini wametakiwa kuacha kuchagua kazi badala yake wajikite kwenye shughuli mbalimbali kujikwamua kiuchumi.

Wito huo umetolewa Agosti 12, 2023 na Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu, wakati wa kongamano la vijana lililoandaliwa na Shirika lisilokuwa la kiserikali la AMO linalojihusisha na uwezeshaji vijana, wanawake, watoto na watu wenye uhitaji maalumu.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, akitoa mada wakati wa kongamano la vijana lililoandaliwa na Shirika lisilokuwa la kiserikali la Amo, Dar es Salaam.

Zungu ambaye pia ni Mbunge wa Ilala, amesema Serikali inathamini vijana ndio maana inatekeleza program mbalimbali ikiwemo ya BBT (Jenga Kesho Iliyo Bora) na nyingine kwa lengo la kuwakwamua kiuchumi.

“Hiki ni kipindi cha watu kufanya kazi, kuwa na ‘masters’ haimaanishi huwezi kuwa mama lishe. Watu wengi wamefanikiwa kwenye kilimo kwahiyo elimu sio kigezo cha kutolima au kufanya kazi nyingine za mikono,” amesema Zungu.

Pia amewaasa vijana kujiepusha na maadili mabaya na kuheshimu mila na desturi za Kiafrika.

“Mjiepushe na ‘Ilove you’, kuna baadhi ya wanaume waongo, kwa siku atawaambia wanawake saba ‘Ilove you’ ili apate anachokitaka na akitoka hapo anakutangaza…achaneni na mambo hayo akitaka kugusa mwili wako mwambie ‘don’t touch me’,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala ambaye alitoa mada kuhusu umuhimu wa vijana kuwa wawajibikaji, Edward Mpogolo, amewataka vijana kuacha na tamaa na badala yake wawe na nidhamu kwenye maeneo yao ya uwajibikaji.

“Unakuta mtu hajawajibika vizuri kwenye nafasi ya afisa tarafa halafu anatamani ukuu wa wilaya, kosa letu vijana wengi ni tamaa.

“Usipokuwa na nidhamu kwenye eneo la uwajibikaji utajikuta unaingia gharama zisizokuwa na manufaa,” amesema Mpogolo.

Mkufunzi wa masuala ya vijana, Rodrick Nabe, amesema vijana wasipofanya juhudi watapoteza ndoto zao.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Amina Said, amesema wanalenga kumuamsha kijana kujitambua na kujua thamani yake kwani asipojielewa na kujithamini ni vigumu kufanikiwa.

“Tunatambua jitihada zinazofanywa na Serikali ndiyo maana tumeweka mikakati ya kuwezesha kundi hili kwa lengo la kutatua changamoto za ajira zinazolikabili.

“Amo inamuamsha kijana aweze kujiongoza mwenyewe na kutimiza malengo yake binafsi,” amesema Amina.

Katika kongamano hilo vijana wamejifunza mambo mbalimbali kama vile kujitambua, masuala ya biashara na uwekezaji, masoko, na fursa zinazopatikana nchini.

Mkurugenzi huyo amesema watawawezesha vijana wajasiriamali 50 kwa kuwapatia vitendea kazi kama vile bodaboda, vyerehani, vifaa vya saluni, majiko ya gesi na vingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles