28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Vijana kunufaika kidijitali na fursa za Ununuzi wa Umma

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Tanzania imeadhimisha Wiki ya Vijana Kitaifa mwaka 2024 kwa kaulimbiu inayosema, “Vijana na Matumizi ya Fursa za Kidijitali kwa Maendeleo Endelevu.” Kaulimbiu hii inalenga kuhimiza vijana kuchangamkia fursa katika uchumi wa kidijitali na matumizi sahihi ya mitandao.

Mkurugenzi Mkuu wa PPRA akiwa ametembelea banda la Brela kwenye maonesho ya wiki ya vijana kitaifa mwaka 2024 jijini Mwanza.

Katika kutekeleza hili, Serikali imeweka mikakati kupitia Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023. Sheria hii inatoa fursa maalum kwa Watanzania, wakiwemo vijana, kwa kuzitaka taasisi za umma kutenga asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi kwa makundi maalum—vijana, wanawake, wazee, na wenye ulemavu.

Akizungumza leo Oktoba 13, 2024 katika Uwanja wa Furahisha, Mwanza, ambapo maadhimisho hayo yanafanyika, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Denis Simba, alisema kuwa serikali imejenga mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa ununuzi wa umma (NeST) unaohakikisha michakato yote ya zabuni inafanyika kwa uwazi, usawa, na bila ubaguzi. Mfumo huu ulianza kutumika rasmi mnamo Julai 1, 2023.

“Mfumo wa NeST unawawezesha wazabuni, wakiwemo vijana na makundi maalum, kushiriki zabuni bila kumjua mtu au kukutana na maafisa serikalini. Hii inatoa fursa ya kufuatilia kila hatua ya zabuni kupitia mtandao,” alisema Simba.

Kati ya Julai 1, 2023, na Oktoba 8, mwaka huu, jumla ya vikundi 210 vilifanikiwa kushinda zabuni zenye thamani ya Sh bilioni 9.8. Kati ya hivyo, vikundi 85 vya vijana vilipata zabuni zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 3.9 kwa mwaka wa fedha uliopita. “Hawa ni vijana wa Kitanzania waliotoa ajira kwa vijana wenzao na kusaidia jitihada za kupunguza umaskini,” aliongeza Simba.

Simba alibainisha kuwa, katika mwaka wa fedha huu, vikundi vya makundi maalum pia vimenufaika kwa kushinda zabuni zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 1.8, ambapo vikundi 29 vya vijana vilinufaika pamoja na vikundi vya wanawake na wazee. Alitoa wito kwa vijana nchini kuchangamkia fursa hizo zilizowekwa kisheria na serikali ya awamu ya sita.

“Vijana wanapaswa kuunda vikundi vya watu 5 hadi 20 na kuvisajili kwenye taasisi wezeshi ambazo zitawasilisha taarifa zao kwa PPRA ili viandikishwe kwenye mfumo wa NeST,” alieleza Simba. Aliongeza kuwa zabuni za chini ya Sh bilioni 50 zimewekwa kwa ajili ya Watanzania pekee, hivyo kuwataka vijana kujitokeza kwa wingi.

Frank Alex, mmoja wa vijana waliohudhuria maadhimisho hayo, alisema kuwa vijana wanahitaji kujiandaa na ukuaji wa teknolojia ili kuendana na mabadiliko. “Vijana tunapaswa kujifunza zaidi kuhusu teknolojia na kutumia mitandao kujipatia maarifa badala ya kupoteza muda. Maarifa haya yatatuwezesha kuajiriwa au kuanzisha biashara binafsi,” alisema Alex.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles