Mwandishi Wetu
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde, amevutiwa na kuwapongeza vijana wa Kikundi cha Vijana cha IJEN jijini humo kwa matumizi sahihi ya teknolojia katika kuleta ufumbuzi kwenye jamii.
Mavunde ametoa pongezi hizo wakati akifungua duka la bidhaa za mboga mboga la kikundi hicho lililopo Capital City Mall ambao wanajulikana kama Soko Kiganjani ambapo mteja anaweza kuagiza bidhaa zake akiwa nyumbani kupitia simu na bidhaa zikamfikia alipo bila yeye kwenda dukani.
“Nawapongeza sana vijana wote mliokuja na wazo hili la kibunifu na kurahisisha upatikanaji wa bidhaa za nyumbani kwa kutumia teknolojia ya simu, jambo ambalo linampunguzia muda na usumbufu mteja.
“Najua hiki ni kikundi na mna ndoto nyingi na ningependa kuwaona mnafikia malengo yenu, binafsi nitawasaidia kuwalipia gharama zote za kusajili kampuni ili muwe katika mfumo wa kibiashara wa kampuni sambamba na kuwatafutia fursa za kuongeza mtaji wenu wa kibiashara”amesema Mavunde
Akizungumza kwa niaba ya wanakikundi, Mwenyekiti wa kikundi hicho, John Ngalaba amemshukuru Mavunde kwa kukubali kuwaunga mkono katika azma yao ya utoaji wa huduma za bidhaa za nyumbani kwa wananchi wa Dodoma na kuahidi kuboresha huduma zaidi kuwafikia wananchi wengi kwa kutumia teknolojia ya simu.