23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Viongozi wanaodaiwa kuchukua milioni 14 za Kijiji waingia matatani

Derick Milton, Meatu

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Meatu ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk Joseph Chilongani ameagiza kufanyika uchunguzi mara moja na kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa viongozi wa kijiji cha Makao, wilayani humo wanaodaiwa kuchukua kiasi cha fedha zaidi ya Sh milioni 14 za Kijiji hicho.

Mbali na agizo hilo, Chilongani ameagiza kupatiwa kwa taarifa ya ukaguzi wa fedha ambazo Kijiji hicho kimekuwa kikipata, taarifa ya mapato na matumizi kwa kipindi cha miaka mitano taarifa ambazo ametaka kupatiwa ndani ya wiki mbili kuanzia leo Mei 28.

Maagizo hayo ameyatoa jana wakati akipokea kiasi cha pesa Sh milioni 14.2 kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani humo ambazo zimerejeshwa na viongozi wa Kijiji hicho baada ya kudaiwa kuzitumia kwa matumizi yao binafsi.

Kabla ya maagizo hayo, akizungumza jinsi walivyorejesha fedha hizo, Mkuu wa Takukuru Wilaya, Marco Matyane amesema viongozi hao walichukua fedha hizo kusikojulikana na kuzitumia kwa matumizi yao binafsi kinyume na malengo yake toka Mei, 2020.

Amesema kuwa Kijiji hicho ambacho kinapakana na hifadhi ya WMA, Makao, Mwiba kilipokea fedha hizo kutoka kwenye hifadhi hizo kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Kijiji ikiwa ni maandalizi ya kupandishwa hadhi kuwa Mamlaka ya mji mdogo wa Makao.

“Baada ya kupata taarifa tulifanya ufuatiliaji na kubaini ni kweli viongozi wa kijiji hicho walichukua pesa hizo kutoka benki, lakini hazikwenda kufanya shughuli iliyokusudiwa, tuliwabana na kuanza kuzirejesha kwa awamu wale wote waliozichukua na leo zimekamilika,” amesema Matyane na kuongeza kuwa;

“Tuliona ni vyema kwanza waliohusika kuzichukua, wazirejeshe kwanza, kisha hatua nyingine za kisheria zitaendelea, kwani tuliona pesa zimechukuliwa Benki lakini hazikupelekwa katika kazi ambayo ilikuwa imekusudiwa,” amesema Matyane.

Mara baada ya taarifa hiyo Mkuu wa Wilaya aliagiza uchunguzi zaidi kuendelea na kuchukuliwa kwa hatua zaidi za kisheria kwa viongozi wote ambao walichukua fedha hizo kwa matumizi yao binafsi.

Dk. Chilongani alisema kuwa Kijiji cha Makao kimekuwa kikipokea kiasi cha zaidi ya Sh ilioni 100 kwa mwaka kutoka hifadhi mbalimbali ikiwemo lanchi ya wanyama ya Mwiba kutokana na kuzungukwa na hifadhi mbalimbali ikiwemo Serengeti.

“Kwa mwaka kijiji kinapokea fedha nyingi, lakini cha kushangaza hakuna maendeleo hata kidogo, huduma za afya, elimu ziko ovyo sana, kama hizi milioni 14 zilichukuliwa vipi, hizo milioni 100, Takukuru lazima mzichunguze matumizi yake,” amesema Dk. Chilongani.

Kwa upande wao viongozi wa Kijiji hicho, walikiri kutoa pesa hizo huku wakibainisha kuwa siyo kweli kuwa walizitumia kwa matumizi mengine au kujinufaisha wenyewe bali zilikuwa zimehifadhiwa kutokana na zoezi la ukarabati wa barabara hizo kuwa na changamoto.

“Wakati tunatoa fedha hizo taratibu zote zilifuatwa, halmashauri ya kijiji iliidhinisha ikiwemo mkutano mkuu wa kijiji, tatizo lilitokea baada ya fedha kutolewa vifaa ambavyo tulitegemea kuja kutengeneza barabara viliaribika” amesema Izack Magaka Mtendaji wa Kijiji.

Mtendaji huyo amesema kuwa baada ya wao kutoa fedha hizo, ndipo walipopata taarifa kuwa vifaa vimearibika hivyo kuamua kukaa nazo hadi pale vifaa hivyo vitakapotengamaa.

Naye, Ester Zakayo mjumbe wa serikali ya Kijiji alisema kuwa walichokosea wao ni kutoa fedha hizo na kukaa nazo muda mrefu bila ya kufanya kazi iliyokusudiwa huku akikanusha madai kuwa walizitumia kwa matumizi yao binafsi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles