28.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 18, 2024

Contact us: [email protected]

Vigogo wa idara Shinyanga, Wachina kortuni kwa kugushi nyaraka

Na Damian Masyenene, Shinyanga

Aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi/Ugavi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Godfrey Mwangairo na Mkuu wa idara ya Kilimo, umwagiliaji na ushirika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ambaye pia ni Mkurugenzi wa Panda International Co Ltd, Edward Maduhu wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa makosa ya kughushi, kutoa nyaraka za uongo na matumizi mabaya ya mamlaka kwa kujaribu kujipatia fedha isivyo halali.

Watuhumiwa wengine katika mashtaka hayo ni Wang Wei raia wa China ambaye ni Mmiliki na Mkurugenzi Mtendaji wa Panda International Co Ltd, Emmanuel Ipandu ambaye ni Mwajiriwa wa kampuni hiyo na Adam Kilimbi ambaye ni Mkurugenzi wa Shinyanga Farm Supplies.

Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa kazi katika kipindi cha robo tatu ya mwaka wa fedha 2020/2021 (Januari- Machi, 2021) iliyotolewa leo na Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga, Francis Luena katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini hapa, amesema kuwa makosa hayo yalitendwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016 na mwaka 2017.

Ambapo, katika kesi ya kwanza ya uhujumu uchumi inayomkabili Godfrey Mwangairo aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi halmashauri ya manispaa ya Shinyanga mwaka 2017, aliwasilisha nyaraka zenye maelezo ya uongo kwenye kamati ya tahmini na kusababisha bodi ya zabuni kutoa kazi kwa kampuni ya EMC System Ltd pasipo kuwa na ushindani na kampuni hiyo kujipatia fedha Sh 43,249,281.34 kwenye zabuni ya kuweka mfumo wa mtandao kiambo (LAN) katika ukumbi wa mkutano uliopo katika halmashauri ya manispaa ya Shinyanga pasipo kufuata sheria.

Katika Kesi ya pili ya jinai dhidi ya aliyekuwa mkuu wa idara ya kilimo, umwagiliaji na ushirika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ambaye pia ni Mkurugenzi wa Panda International Co Ltd, Edward Maduhu, Mmiliki na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Panda Wang Wei pamoja na Emmanuel Ipandu ambaye ni Mwajiriwa wa Kampuni hiyo, watuhumiwa wanakabiliwa na makosa matatuikiwemo kujaribu kutenda kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu Sh 3,480,000.

Pia, Edward Maduhu akikabiliwa na kosa la kumdanganya mwajiri kwa kuandika kuwa zoezi la kugawa ruzuku za pembejeo lilifanyika wakati siyo kweli na kutumia madaraka vibaya kama mkuu wa idara ya kilimo. Huku, Wang Wei na Emmauel Ipandu wakishtakiwa kwa kosa la kughushi na kutoa nyaraka ya uongo kuonyesha kuwa pembejeo za ruzuku ziligawanywa kwa wananchi wa Kijiji cha Ibubu walioandikwa katika vocha wakati haikuwa kweli.

Kesi ya tatu inawahusu washtakiwa wanne Edward Maduhu, Adam Kilimbi, Wang Wei na Emmanuel Ipandu ambao wanakabiliwa na makosa ya kujaribu kutenda kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu Sh 3,480,000, huku Adam Kilimbi ambaye ni Mkurugenzi wa Shinyanga Farm Supplies akikabiliwa na kosa la kutoa nyaraka za uongo za vocha za pembejeo alizowasilisha halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kwa wana Kijiji aliowaandika katika kila vocha kuwa walipata pembejeo za ruzuku wakati siyo kweli.

Katika hatua nyingine, Takukuru kupitia dawati la kuzuia rushwa katika kipindi cha Januari- Machi, 2021 imeendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayopewa fedha za serikali na ufadhili wa wadau wa maendeleo, ambapo jumla ya miradi sitayenye thamani ya Sh 2,428,687,655 ilifuatiliwa.

Pia ofisi hiyo ilifanya kazi tatu za uchambuzi wa mfumo katika halmashauri tatu ili kubaini kama kuna mianya ya rushwa katika utoaji wa vibali vya ujenzi, ambapo mapungufu kadhaa yalibainika ikiwemo ofisi ya ardhi kutokuwa na vitendea kazi ikiwemo magari ya idara na kupelekea baadhi ya majukumu kukwama, pia kutokuwepo kwa uwazi katika ofisi zote za mitaa na kata juu ya gharama halisi za upatikanaji wa vibali vya ujenzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles