26.9 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Vigogo RAHCO wakabiliwa na mashtaka nane

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

MKURUGENZI Mtendaji, Katibu wa Kampuni Hodhi ya Mali za Reli (RAHCO) na mfanyabiashara ambaye pia ni mwakilishi wa Kampuni ya Rothschild (South Africa) Proprietary Ltd, wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuisababishia Serikali hasara zaidi ya Sh bilioni moja.

Washtakiwa hao Benhardard Tito, Kanjia Mwinyijuma na Emmanuel Massawe, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana na kusomewa mashtaka manane mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Akisoma mashtaka hayo, Wakili wa Serikali Mkuu, Timony Vitalis na mawakili wengine wane, alidai washtakiwa wanakabiliwa na jumla ya mashtaka manane.

Katika shtaka la kwanza mshtakiwa wa kwanza hadi wa tatu wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama kati ya Septemba Mosi, 2014 na Septemba 30, 2015 kwa nia ya kutenda kosa kinyume cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa.

Shtaka la pili linamkabili Tito ambapo inadaiwa Februari 27, 2015 katika ofisi za RAHACO wilayani Ilala, akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, alitumia madaraka yake vibaya kwa kuiajiri Kampuni ya Rothschild (South Africa) Proprietary Ltd kama mshauri wa mradi wa uimarishaji reli ya kati bila idhini ya Bodi ya Zabuni ya RAHACO.

Shtaka la tatu linawakabili Tito na Massawe, ambao wanadaiwa kuwa Machi 12, 2015 katika ofisi za RAHACO wilayani Ilala wakiwa katika nyadhifa zao, walisaini barua ya kuihalalisha kampuni hiyo ya Afrika Kusini kuwa mshauri wa mradi wa uimarishaji reli ya kati na kutoa huduma za ushauri wa kifedha kuhusu mradi huo.

“Shtaka la nne linamkabili mshtakiwa Tito na Massawe. Wanadaiwa Machi 12 na Mei 20, 2015 wilayani Ilala walishindwa kuwasilisha mkataba wa huduma ya ushauri kati ya kampuni hiyo ya Afrika Kusini na RAHACO.

“Shtaka la tano linamkabili mshtakiwa Tito na Massawe. Wanadaiwa Mei 20, 2015 katika ofisi za RAHACO, kwa kutumia madaraka yao vibaya walisaini mkataba wa kutoa huduma za ushauri na kampuni ya Afrika Kusini bila ridhaa ya Bodi ya Zabuni ya RAHACO,” alidai Vitalis.

Katika shtaka la sita, Vitalis alidai linamkabili mshtakiwa Tito na Massawe, ambao wanadaiwa kati ya Mei 20 na Juni 20, 2015 walitumia madaraka yao vibaya kwa kushindwa kuwasilisha mkataba walioingia na kampuni ya Afrika Kusini kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Shtaka la saba linawakabili washtakiwa wote watatu, Tito, Mwinyijuma na Massawe, wanaodaiwa kati ya Machi mosi na Septemba 30, 2015 katika ofisi za RAHACO, waliipa kazi  kampuni hiyo ya ushauri na kuilipa kwa kutoa huduma za ushauri, malipo ambayo yaliisababishia RAHACO kupata hasara ya dola za Marekani 527,540.

Wakili Vitalis alidai katika shtaka la nane, mshtakiwa Tito anadaiwa Agosti 18, 2015 katika ofisi za RAHACO Ilala, ambapo kwa kutumia madaraka yake vibaya aliipa Kampuni ya Ujenzi wa Reli ya China kazi ya kujenga kilomita mbili za reli maeneo ya Soga iliyogharimu dola za Marekani 2,312,229.39 bila idhini ya Bodi ya Zabuni ya RAHACO.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa sababu mashtaka yanayowakabili yanasikilizwa Mahakama Kuu, na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) hakutoa kibali kwa Mahakama ya Kisutu kusikiliza kesi hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles