30.3 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Vigogo Chadema, ACT wateta kwa saa tatu

ANDREW MSECHU na NORA DAMIAN –dar es salaam

SIKU chache baada aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharf Hamad kujiunga na ACT-Wazalendo, viongozi wa chama hicho ambacho sasa kimepata nguvu Zanzibar, wamekutana na wenzao wa Chadema na kuteta kwa takribani saa tatu.

Mbali na Maalim Seif, baadhi ya viongozi wengine walioshiriki kikao hicho kilichofanyika ofisi za Chadema makao makuu Kinondoni, ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu Dk. Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalim, Kiongozi wa ACT,  Zitto Kabwe na Mwenyekiti Yeremia Maganja.

Tangu Maalim Seif kutangaza kuungana na ACT Machi 18, mwaka huu, mjadala ulioibuka ni kama kiongozi huyo mwenye ushawishi zaidi Zanzibar ataachana na muungano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ama atafanikiwa kuunganisha chama chake kipya na muungano huo.

Muungano wa viongozi hao unafungua ukurasa mpya kwani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Maalim Seif aliyegombea urais wa Zanzibar kupitia CUF, alikuwa kwenye Ukawa, huku ACT wakiwa si washiriki.

Kikao cha jana kinatoa picha kwamba vyama hivyo viwili vitafungua ukurasa mpya na kuthibitisha kauli ya Maalim Seif aliyoitoa hivi karibuni, kwamba pamoja na mambo mengine, waliamua kujiunga ACT kwa sababu na wao pia walishatoa maombi ya kujiunga na Ukawa. 

Baada ya Maalim Seif kuhamia ACT, CUF iliyo chini ya Profesa Ibrahim Lipumba, ilitangaza kujitoa Ukawa. Vyama vingine vilivyokuwa vikiunda Ukawa ni NCCR-Mageuzi na NLD.

Mmoja wa watu walioudhuria kikao cha jana kilichoanza saa tisa alasiri na kumalizika saa 11 jioni, alilidokeza gazeti hili kuwa kilijadili juu ya vyama hivyo kushirikiana katika nyanja mbalimbali.

“Kikao kilijadili mambo mengi ya kushirikiana, tumejadili suala la Sheria mpya ya Vyama vya Siasa, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao utafanyika mwaka huu na tisho la kufutwa kwa ACT,” kilidokeza chanzo hicho.

Kilisema ushirikiano huo utaenda mbali zaidi kadiri muda utakavyoenda, yote ikiwa ni kusimamia misingi ya demokrasia.

MKUTANO WA ACT WAZUIWA

Katika hatua nyingine, Maalim Seif aliyewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameeleza kusikitishwa na polisi kuzuia mkutano wa ACT uliokuwa ufanyike Temeke jana, akisema walioagiza hilo watakwenda kujibu mbele ya Mungu.

Akizungumza katika ofisi za makao makuu ya ACT, Kijitonyama wilayani Kinondoni jana baada ya mkutano wa kupokea wanachama wapya uliokuwa ufanyike Hoteli ya PR Temeke kuzuiwa, Maalim Seif alisema anajua polisi wametumwa, lakini waliowatuma wana suala la kujibu kwa Mungu.

Alisema yote yanatokea baada ya kuona ACT ni chama chenye mwelekeo, ambacho kwa mipango iliyopo hakina wasiwasi na kinajipanga kuchukua dola.

“Huu ndio ugomvi uliopo baina ya dola na ACT. Dola ipo katika kujilinda tu, wanataka wabaki madarakani hadi mwisho wa dunia, lakini wamesahau kuwa atakayebaki milele ni Mungu pekee.

 “Utakwenda kujibu mbele ya Mungu, kwamba je, ulipochukua fursa hii uliwatendea haki Watanzania wenzako? Leo unaiandama ACT, imefanya nini? Tumefanya ziara Unguja na Pemba hata sisimizi hakukanyagwa na hatukuona uvunjifu wa amani kwa namna yoyote,” alisema Maalim Seif.

Alisema Tanzania ni nchi ya kidemokrasia ambayo katiba yake inaruhusu vyama vingi, pia inatoa haki sawa kwa vyama vyote, hivyo ni vyema katiba ikaheshimiwa.

 “Katiba inakataza ubaguzi wa aina yoyote ile, sasa ujiulize, ubaguzi haupo katika nchi? Na kama upo, nani anausimamia.

 “CCM iko huru wakati wote kufanya shughuli zake, akina Bashiru (Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally) siyo kiongozi wa Serikali, lakini anafanya mikutano ya hadhara kila mahali. Lowassa (Waziri Mkuu mstaafu, aliyerejea CCM kutoka Chadema) siyo kiongozi wa kiserikali, lakini kafanya mikutano ya hadhara kule Monduli, na Jeshi hili hili la Polisi lipo,” alisema.

SI MAGENI

Maalim Seif aliwatua moyo wafuasi wa ACT waliokusanyika kwenye ofisi hizo, akisema hayo kwake si mageni, ameyazoea na kwamba vyovyote wafanyavyo wataendelea kufanya siasa na kukijenga chama hicho.

“Haya sisi tumeshayazoea. Fanyeni mfanyavyo, sisi tunasema tumeshashusha tanga na safari inaendelea, hawatotutoa katika hili, kabisa kabisa.

“Kwanini hamuwaachi wananchi watumie uhuru wao? Kinachowatisha ni kuona watu wengi wanahudhuria mikutano ya upinzani, wakati wao wanataka dunia iamini kwamba vyama vya upinzani havina wapinzani,” alisema.

ZITTO: TUTAWAFUATA MATAWINI

Akizungumza katika mkutano huo, Kiongozi wa ACT, Zitto Kabwe, alisema sasa watapita kila tawi kuandikisha wanachama wapya baada ya mpango wa kuwakabidhi kwa pamoja kushindikana jana kwa kuzuiwa na polisi.

Alisema wanajua kuwa polisi wametumwa, hivyo ni muhimu wanachama kuhakikisha hawaingii katika mtego wa kutaka waonekane ni watu wa fujo, hivyo busara iliyotumika ni kukwepa mtego huo.

“Wanatafuta na kuokoteza kila sababu za kufuta hiki chama. Wamezuia mkutano wa leo makusudi wakiamini viongozi tutalazimisha mkutano kwa lazima na wanachama wagombane na polisi vurugu zitokee wakifute chama kwa sababu kwamba sisi ni chama cha fujo. Tusiwape hiyo sababu,” alisema.

Alisema hawatakata tamaa wala kuvunjika moyo kwa juhudi zinazofanywa na dola, bali juhudi hizo zinawakomaza na watashinda, kwa kuwa haamini kwamba kuna mahali dola iliwahi kuwashinda wananchi pale wanapoamua.

Katika mkutano huo, aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo alikabidhi bendera, katiba, kadi na mavazi kutoka kwa wanachama waliokuwa wanachama wa chama hicho ambao wamehamia ACT, akitaka zikabidhiwe kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.

Alisema wanachama hao zaidi ya 8,800 wa Mkoa wa Dar es Salaam walihitaji wazichome moto, lakini waliona ni vyema waziwasilishe kwa kiongozi wa ACT wakimwomba ampelekee msajili.

Mketo alisema hatua ya polisi kuzuia mkutano wao huko PR imeongeza hamasa ya wanachama kupigania haki zao na kwamba ana uhakika 2020 chama hicho kinakwenda kushika serikali.

Mkutano huo ulifanyika huku askari polisi waliokuwa katika magari matatu wakiwa wamezingira eneo la ofisi za chama hicho.

MKUTANO ULIVYOZUILIWA

Awali MTANZANIA lilifika katika Hoteli ya PR Temeke saa 3 asubuhi ya jana na kukuta askari polisi wakiwa wamezingira eneo hilo, huku wakizuia watu wasiingie ndani.

Nje ya hoteli hiyo kulikuwa na gari tatu zilizokuwa na polisi wenye silaha huku wengine wakiwa wamesimama geti kuu la kuingilia hotelini hapo.

Mwandishi wa gazeti hili alisogea getini hapo na kujitambulisha kwa askari hao, lakini walimweleza kuwa mkutano umezuiliwa.

“Mkutano umezuiliwa na haruhusiwi mtu yeyote katika eneo hili,” alisema mmoja wa askari polisi aliyekuwa nje ya hoteli hiyo.

Kiongozi mmoja wa ACT aliyekuwa getini hapo alisema; “Tunaomba radhi kwa usumbufu, mkutano umezuiliwa tutawataarifu baadaye.” 

KAMANDA MAMBOSASA

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema walizuia kufanyika mkutano huo baada ya kupata taarifa za kuwapo kwa viashiria vya uvunjifu wa amani.

Alisema vyama vya ACT na CUF, hivi sasa vina msuguano na kwamba walipata taarifa kuwa wafuasi wa CUF walipanga kufanya vurugu.

“Wanachama wawe watulivu, sisi tulizuia kwa sababu tulipata taarifa kuwa CUF walipanga kufanya vurugu, hivyo tukaona si vizuri kuacha watu wakaumizana,” alisema Mambosasa.

Mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles