JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA YA HABARI
KICHWA cha habari hapo juu kilicho katika mfumo wa swali kinaweza kukushtua msomaji usipate picha kabla hujasoma maudhui yaliyokizunguka.
Lakini baada ya kuyasoma na kuelewa kusudio lake, hata kama hautakubaliana na ‘jawabu la ndio’ kuhusu swali hilo utakuwa umeshapata picha.
Katika tovuti ya Shirika la Habari la Uingereza (BBC) upande wa habari za elimu kuna habari iliyojengwa chini ya kichwa hicho cha habari yaani; Je, vifutio shuleni ni silaha ya shetani?
Simulizi hiyo inabainisha kuwa mwanasayansi mmoja mashuhuri wa utambuzi nchini Uingereza amependekeza kupigwa marufuku kwa matumizi ya vifutio madarasani.
Inajulikana wazi kwamba vifutio kote duniani ikiwamo hapa kwetu Tanzania, hutumika kwa ajili ya kufuta makosa au uchafu karatasini unaotokana na penseli.
Kwa wale wanaotumia pen, hutumia wino mweupe kama tunaotumia maofisini au mwingine kama huo ukijulikana kama (corrective fluid) kufuta makosa au uchafu uliotokana nayo.
Na wino huu wa kuficha makosa au uchafu, katika baadhi ya shule nchini Uingereza nao tayari umepigwa marufuku.
Kwa hiyo, badala ya kutumia corrective fluid katika kufuta kosa, wanafunzi hutakiwa kupigia mstali jawabu, ambalo wanahisi wamekosea na kuandika katika mstali mpya au ukurasa mwingine jibu sahihi.
Lakini pia kilichosababisha sehemu kubwa ya shule hizo zilizoharamisha matumizi ya wino huo, ni uwapo wa wanafunzi waliopotoka wanaoutumia kuvuta ili kupata kilevi kana kwamba wananusa dawa za kulevya.
Watoto hawa hawana tofauti na wale tunaowasikia hapa Tanzania wakivuta gundi na au petroli ili kupata kile wanachokiita nishai.
Kuhusu kifutio, suala lililozua ubishani na mjadala mkubwa nchini humo liliibuliwa kufuatia pendekezo la mwansayansi huyo Guy Claxton wa Chuo Kikuu cha Wafalme London.
Akizungumza na gazeti la Daily Telegraph wiki iliyopita, Professa Claxton alisema: “Kifutio ni kifaa cha shetani kwa sababu kinachochea utamaduni wa kuonea haya makosa. Ni njia ya kuidanganya dunia, ikisema, ‘sikufanya kosa. Nilipata mara ile ile nilipoandika.’ Hivyo basi ndivyo inavyotokea wakati unapofuta kosa na kuandika upya jawabu sahihi.”
“Badala yake, tunahitaji utamaduni, ambao watoto wetu hawahofii kufanya kosa, utamaduni ambao utawafanya kuyaangalia makosa yao na kujifunza kutokwa kwayo. Katika hilo wataendelea kuakisi na kuimarika juu ya kile walichofanya, si kuumiza kichwa kupata jibu sahihi na kuonekana nadhifu. Huko ni kujidanganya,” alisema.
Aliongeza: “kuharamisha kifutio, badala yake mahala pake pawepo ishara kubwa ambayo itamwambia mtoto; ‘usifute makosa yako, yape kipaumbele kwa sababu makosa ni marafiki zako na walimu wako.’
Kauli yake hiyo ya kuharamishwa kwa vifutio madarasani ni sehemu ya mjadala mpana unaoendelea nchini humo kuhusu kuachana na utamaduni wa kutoa maksi na kufanyia kazi tabia, mioyo na silka za wanafunzi ili kuwaandaa kwa maisha ya ajira.
Mwandishi huyo wa Educating Ruby, kitabu kinachoeleza namna ya kujenga tabia katika wanafunzi, alisema: “Shule hazipaswi kuwa mahali pa kupata majibu sahihi ili kufaulu mitihani, zinapaswa ziwe mahali pa kuandaa watoto wote kwa ajili ya kuyamudu maisha. Tunapaswa kupunguza pengo kati ya kujifunza kama dunia halisi na namna inavyofanyika shuleni.”
Ametoa pendekezo hilo huku ikijulikana wazi kuwa watoto wengi wanapenda vifutio, ambavyo vipo katika kila aina ya muundo na harufu tofauti tofauti za kupendeza.
Wakati kukiwa na wanaomuunga mkono, wengi wanampinga ila wakikubaliana na hoja zake kuhusu athari za kisaikilojia za matumizi ya vifutio.
Kundi hili linakubaliana naye hatari ya kulea kizazi cha watoto, ambao wanahofia kufeli. Linataka kuona watoto wanakuwa na mwamko wa namna ya wanavyofanya vitu.”
Naam, kundi hili kubwa halipendi kuona vifutio, ambavyo wao wenyewe walivitumia katika miaka yao ya utotoni na ujanani shuleni vikifutiliwa mbali, linakiri uwapo umuhimu wa kuwahimiza wanafunzi kukuza uelewa sahihi wa jinsi ya kufanya kwa kutumia makosa yao.
Kwa maneno mengine wanakiri umuhimu wa kuhamasisha watoto kuyaona makosa kama sehemu muhimu ya kujifunzia.
Maoni ya mtaalamu huyo wa utambuzi yametokana na utafiti uliobainisha kuwa ujasiri na udadisi ni viungo viwili muhimu kwa ajili ya mafanikio ya wanafunzi.
Lakini, je, pendekezo la profesa huyu mstaafu wa Sayansi ya Kujifunza wa Chuo Kikuu cha Winchester kuwa vifutio vipigwe marufuku darasani ni sahihi?
‘Nadhani kupiga marufuku vifutio ni kitendo cha kikatili mno,” anasema John Coe, msemaji wa Chama cha Taifa cha Elimu ya Msingi Uingereza (NAPE).
“Hata hivyo, nakubali kwa wakati fulani vifutio havipaswi kutumika. Iwapo ninafundisha darasa hisabati, ningewataka wanafunzi waoneshe kazi. Nisingependa wanafunzi wangu wajikite zaidi katika kupata jawabu sahihi, ambalo hawakuonesha kiashiria chochote kuwa awali walikosea.”
‘Kubaini makosa ya watoto ni sehemu muhimu ya kujifunza. Walimu wanahitaji kuchunguza jitihada zote watoto wanazofanya ili waweze kulenga mafundisho yao,” anasema.
Hoja ya Claxton ni kwamba kwa kuwafanya watoto wakane kuwa hawafanyi makosa, itashindikana kuwaaandaa kuendana na dunia halisi, ambako makosa hayaepukiki na gharama kufuata.
“Kwa watoto wadogo hatua ya kuweza kumiliki kosa ni hatua kubwa kuifikia,” anasema Dk. Anthony Williams, mtaalamu wa saikolojia ya mtoto kutoka Chuo Kikuu cha Sheffield. “Hii ni pamoja na kwamba watu wazima tumekuwa tukikubali au kukataa kufanya makosa.”
Lakini iwapo vifutio vitapigwa marufuku darasani kama Claxton anavyopendekeza, hatua hiyo itaishia wapi?
“Madarasa mengi zaidi yanazidi kutumia Teknolojia ya Habari,” anasema Williams.
“Sasa hebu jiulize, ukiondoa ufunguo wa kufutia katika keibodi ya kompyuta(delete key)? Unaweza kufikiria ukiwa na kompyuta yako ukichapa kazi kama kawaida au wengine wakifanya zao, huku ‘delete key’ ikiwa imeondolewa? Katika dunia halisi, daima tunafanya makosa madogo madogo, kuyarekebisha na kuyabadili.”
Anachomaanisha Williams ni kwamba haiwezekani kupiga marufuku vifutio hata kama kuna athari, isipokuwa anashauri kuwepo mipaka ya matumizi yake ili kuwajenga watoto kisaikolojia wazoee makosa na kuyaona kama sehemu ya kujifunza.