Washington, Marekani
RAIS wa Marekani, Donald Trump amewaonya Wamarekani kujitayarisha kwa idadi ya kutisha ya vifo vinavyotokana na virusi vya corona katika siku zijazo wakati idadi jumla ya vifo duniani kote ikifikia 60,000.
Kesi zilizothibitishwa na wagonjwa wa virusi vya Covid-19 nchini Marekani juzi Jumamosi imepindukia watu 300,000, lakini Ulaya inaendelea kuadhibiwa na janga hilo ambalo limesababisha karibu nusu ya watu wote duniani kote kujifungia ndani ya majumba yao kwa gharama kubwa ya uchumi wa dunia.
Zaidi ya vifo vya watu 45,000 duniani kote vimetokea katika mataifa ya Ulaya, ambapo Uingereza imeripoti kiwango cha juu kipya cha vifo kwa siku, na kufikisha idadi jumla ya vifo kuwa 4,300 kutoka jumla ya kesi za maambukizi 42,000.
Malkia Elizabeth II alitoa hotuba maalum ya binafsi jana Jumapili kuwataka watu kusimama na kupambana na changamoto hii inayotokana na virusi vya corona, na binafsi kuwashuruku wafanyakazi wanaowahudumia wagonjwa wa Covid-19.
“Nina matumaini katika miaka inayokuja kila mmoja ataweza kujivunia ni kwa njia gani aliweza kupambana na changamoto hii,” alisema katika hotuba yake hiyo jana.
Hivi sasa kuna zaidi ya kesi milioni 1.2 zilizothibitishwa za mambukizi ya virusi vya corona duniani kote na zaidi ya watu 65,000 wamefariki tangu virusi hivyo vilipozuka nchini China mwishoni mwa mwaka jana, kwa mujibu wa idadi iliyojumlishwa na Chuo Kikuu cha Johns Hopkins.
Hata hivyo, Trump amesema Marekani inaingia katika “wakati ambao ni wa hali ya kutisha” kwa “idadi mbaya kabisa.”
“Hii huenda itakuwa wiki ngumu kabisa, kutakuwa na vifo vingi sana,” alisema katika Ikulu ya White House.
Wakati huo huo, Rais huyo amesisitiza kuwa Marekani haiwezi kuendelea kufungwa kwa milele.
“Mapambano dhidi ya virusi ni muhimu, lakini hatuwezi kuiharibu nchi yetu. Nilisema tangu mwanzo, tiba haiwezi kuwa mbaya kuliko matatizo,” alisema.
Kitisho cha mikusanyiko mikubwa kimeonekana tena mwishoni mwa juma, mara hii nchini Pakistan ambako maofisa wanajaribu kuwafuatilia na kuwaweka katika karantini mamia kwa maelfu waumini ambao walihudhuria tukio kubwa la Kiislamu mwezi uliopita.
Zaidi ya watu 150 ambao wamehudhuria wamethibitishwa kuambukizwa na virusi vya corona hadi sasa, na watu wawili wamekufa. Wageni kutoka nchi kadhaa pia walikwenda katika tukio hilo, ambalo lilifanyika licha ya Serikali kuomba kufutwa kutokana na kitisho cha virusi.