NA CHRISTOPHER MSEKENA
‘MAPENZI matamu,
Niwapo nawe mpenzi,
Sioni mwingine wa kufanana na wewe,
Nitalienzi penzi lako sitokuacha hasilani.
NI sanaa ya hali ya juu kabisa kutengeneza wimbo ambao unakwenda mtaani kuimarisha uhusiano uliolegea, kurudisha penzi lililotaka kupotea, kuwapa utulivu walioumizwa na mapenzi, kuifunza jamii kuwa mbali na ulaghai mwingi uliopo bado kuna mapenzi ya kweli hakika kwa tungo zile Rehema Chalamila ‘Ray C’, alituweza.
Hivi ni nani kati yetu ambaye hakuwahi kuvutiwa na moja kati ya nyimbo nyingi za Ray C? Ni ngumu kukwepa hili maana kipindi hicho nyimbo za mkongwe huyu aliyepachikwa jina la ‘Kiuno Bila Mfupa’ zilitumika kama ‘dedication’ katika uhusiano mwingi wa mapenzi.
Nyimbo kama Mapenzi Matamu, Mahaba ya Dhati, Upo Wapi, Umenikataa, Sikuhitaji, Nimezama, Penzi Lako, Na Wewe Milele, Sogea na nyingine kadha wa kadha zilitosha kabisa kumpa nafasi ya juu kwenye orodha ya wasanii mahiri kuwahi kutokea kwenye historia ya Bongo Fleva.
Ngoma hizo zilimpa shoo kibao, alikwea pipa na kutua karibu kila nchi ughaibuni, umaarufu wake ukakua si haba na marafiki wazuri hata wabaya wakaingia kwenye himaya yake na kwa kuwa Ray C ni kipenzi cha watu, wote waliokuja mbele yake aliwakumbatia na hilo likawa ndiyo kosa kubwa alilolifanya.
Kasi yake ya kukimbilia mafanikio ilipungua ghafla, Ray C akawa ni nadra machoni pa watu, taarifa zikasikika kuwa amepata bwana nchini Kenya hivyo shughuli zake za muziki pia atazifanyia huko.
Hiyo ilikuwa ni habari njema kwa wote waliompenda ila ikageuka na kuwa mbaya baada ya miaka kadhaa kupita tetesi zikasambaa kuwa ameingia kwenye utumiaji wa dawa za kulevya, alikana mara kadhaa lakini madhara ya unga huwezi kuyaficha kwa mikono.
Afya yake ikateteleka, picha za kusikitisha zikasambaa mitandaoni na wabaya wake wakazusha kuwa Ray C amakufa. Ikumbukwe hiki ni kipaji kilichokosha nyoyo za wengi akiwamom, Rais Mstaafu JK ambaye aliguswa, akaweka mipango thabiti na mwisho wa siku akapelekwa soba.
Baada ya kupata matibabu alipona, akanzisha taasisi yake ya kupambana na dawa za kulevya inayoitwa Ray C Foundation, jembe likaingia kazini ila sijui nini kilimkuta maana nakumbuka mara ya mwisho alikamatwa na vyombo vya usalama akitaka kujidhuru maeneo ya American Chips, Dar es salaam hali iliyodaiwa kusababishwa na kurudia matumizi ya dawa hizo.
Sijui nini kinaikumba tasnia ya burudani, dawa za kulevya zimeendelea kupoteza vipaji vingi ambavyo zilikuwa vinaweza kuwa zaidi ya kina Kanumba, Diamond, Ali Kiba, Vanessa Mdee na wengine.
Wiki hii Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda alitoa orodha ya watuhumiwa wanaojihusisha na dawa za kulevya ikiwa ni mikakati yake ya kuhakikisha Jiji hili linakuwa mahala salama.
Jambo lililozua gumzo kitaa ni pale majina ya watu maarufu kwenye tasnia ya burudani kama vile Petti Man, Mr Blue, Wema Sepetu, TID, Chid Benz, Recho, Dogo Hamidu na Babuu wa Kitaa ambapo walitakiwa kuripoti kituo cha kati polisi kwa maelezo.
Wakati hayo yakiendelea kimya kingi kina mshindo mkubwa, tukiwa tunaisubiri kwa hamu siku ya wapendanao hapo Februari 14 tayari masikioni mwetu tumeanza kusikia ile sauti tamu tuliyoikosa kwa muda mrefu kutoka kwa Ray C.
Ijumaa ya wiki iliyopita alikuwa mkoani Dodoma na kupata fursa ya kutumbuiza wimbo wake unaoitwa Umenikataa mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Siyo Ray C yule aliyetuhuzunisha mwaka jana huyu ni mpya kabisa mwenye kasi na kiwango cha kuwa msanii bora endapo akiendelea kukaza. Tayari amefanya kava ya wimbo wa mdogo wake Recho unaoitwa ‘Upepo’ ambao unaopatikana mtandaoni.
Hali kadharika ameonekana akipiga tizi pale nyumba ya vipaji (THT) na kushiriki kuandaa (Valentine Collection Album) inayoandaliwa na Ema The Boy wa Epic Record itakayotoka hivi karibuni.
Haitoshi anakwenda kuwapa burudani mashabiki wake siku ya wapendanao, Februari 14 akiwa na Barnaba, anaweka muda wake mwingi kwenye kazi ambayo kipindi hiki ameipa kipaombele zaidi kuliko chochote kile.