Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM Wilaya ya Ilala, Neema Kiusa, amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi za Serikali za kulinda mazingira kwa kupanda miti kwa wingi katika maeneo yao.
Kiusa ameyasema hayo Aprili 14,2023 wakati wa maadhimisho ya matendo mema yaliyoratibiwa na taasisi ya Fahari Tuamke Maendeleo na kufanyika katika Kituo cha Afya Chanika.
Maadhimisho hayo yalihusisha kufanya usafi wa mazingira na kupanda miti katika Kituo cha Afya Chanika.
“Tunapopanda miti pia tunatekeleza matendo mema duniani kwa sababu tunatunza mazingira, pia tunatekeleza agizo la mheshimiwa Rais Samia ambaye ametuelekeza kupanda miti milioni moja kila mkoa,” amesema Kiusa.
Mwenyekiti huyo pia amewataka wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao ili kuepuka wasijiingize katika vitendo viovu.
“Tuishi katika misingi ya Utanzania, tusiige tamaduni zingine, tuwafundishe watoto wetu waweze kujitambua, tuwaeleze wazi waepuke kutenda matendo ambayo ni kinyume cha sheria za nchi yetu na ambayo hayampendezi Mwenyezi Mungu,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa taasisi ya Fahari Tuamke Maendeleo, Neema Mchau, amesema kila mwaka wamekuwa wakiadhimisha siku hiyo kwa kufanya matukio mbalimbali ya kijamii yanayohimiza kutenda matendo mema duniani.
“Mwaka huu tulisema lazima tuunge mkono juhudi za mheshimiwa rais kwa kuja kupanda miti, naamini kama dunia tukitenda mema kila mtu katika nafasi yake hata ukatili katika jamii utapungua… ukitenda mema huwezi kumfanyia ukatili binadamu mwenzako,” amesema Mchau.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Kata ya Chanika, William Mwila, ameipongeza taasisi hiyo na kuwataka wana – CCM kuendeleza matendo mema katika jamii.