Na ESTHER MNYIKA-DAR ES SALAAM
PAMOJA na mchango wake katika maendeleo duniani, viwanda ndiyo vinaelezewa kuwa mchafuzi namba moja wa mazingira.
Uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na viwanda unaendelea kuwa changamoto kubwa kote duniani, kutokana na kukua kwa sekta hii muhimu kwa uchumi.
Akizungumza na MTANZANIA, Ofisa Mkuu wa Mazingira wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Arnold Kisiraga, anasema viwanda ndio chanzo kikuu cha uchafuzi wa mazingira kwa Tanzania, kama ilivyo sehemu nyingine nyingi duniani.
Anasema hata hivyo, Baraza hilo limekuwa likifanya jitihada kubwa kuhakikisha kuwa uchafuzi unaosababishwa na viwanda unadhibitiwa kupitia tathmini ya athari kwa mazingira ambayo viwanda vinatakiwa kufanya kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2014 .
“Nawataka wawekezaji wa viwanda nchini kufanya tathimini ya athari za mazingira kabla ya ujenzi wa viwanda ili kuepuka athari za uchafuzi wa mazingira zinazotokana na shughuli za uzalishaji wa bidhaa za viwanda kama majitaka na kemikali,” anasema Kisiraga.
Ofisa huyo anafafanua kuwa, sekta ya viwanda ni sehemu muhimu ya uchumi wa kisasa ambapo bidhaa zinatengenezwa kwa wingi kwa kutumia mashine na michakato maalumu, lakini anasisitiza suala la kutunza mazingira ili kuokoa afya za binadamu na wanyama.
Kisiraga anasema, Serikali imedhamiria kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ili kuongeza kasi ya kufikia lengo la Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, ambayo imedhamiria kuifikisha Tanzania kuwa nchi yenye hadhi ya kipato cha kati na kupunguza umaskini kufikia mwaka 2025.
Anasema nchi inapoelekea kuwa ya viwanda, wawekezaji lazima watunze mazingira na kuzingatia Sheria ya Mazingira ya mwaka 2014.
“Umuhimu wa kufanya tathmini ya athari za mazingira kama sasa ni mkubwa, kwa kuwa Serikali imeamua kwenda katika uchumi wa kati kwa kutumia viwanda. Viwanda ni chanzo cha uchafuzi wa mazingira kutokana na kuzalisha kemikali, majitaka na uharibifu wa afya za watu, viwanda vingi vitafunguliwa ila tunahitaji vifuate Sheria ya Mazingira namba 20 ya mwaka 2014,” anasema.
Anasema, ni jukumu la Baraza kufanya ukaguzi kila wakati katika maeneo ya viwanda, ili kuhakikisha sheria zinazingatiwa ipasavyo.
Anaeleza kuwa, idadi ya watu duniani inaongezeka kila siku na hivyo mahitaji ya bidhaa mbalimbali yanaongezeka pia.
“Ukiachilia mbali ongezeko la watu duniani, ukuaji wa teknalojia kwa sasa unawafanya wazalishaji wa bidhaa mbalimbali kuzalisha na kuendelea kuwekeza,” anasema.
Anaendelea kufafanua kuwa, kutokana na hali hiyo, bado viwanda vinaendelea kuzalisha kwa wingi ili kukidhi haja za wateja, jambo ambalo husababisha uchafuzi wa mazingira.
Anasema mwanzoni wawekezaji wa kwenye viwanda walikuwa hawana uelewa wa kutosha wa sheria hiyo, ila kwa sasa uelewa ni wa kuridhisha.
Kisiraga ametoa wito kwa wawekezaji wanaotaka kuanzisha viwanda kujiandikisha katika baraza hilo ili kupata vibali vya tathmini ya mazingira kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa viwanda bora vinavyojali mazingira.
Naye Ofisa Mazingira Mwandamizi NEMC, Fredrick Mulinda, anasema hadi sasa baraza hilo limechunguza asilimia 20 ya viwanda vilivyojengwa, pamoja na kufanya tathimini ya athari za mazingira kwa miradi zaidi ya 1,800 inayohusisha viwanda, ujenzi wa barabara, shule na miundombinu mingine.
“Mwaka huu tumefanya tathmini ya athari za mazingira kwa miradi 1,800, ikiwamo ya viwanda, majengo, barabara, shule. Tangu mwaka 2013 hadi sasa tumepokea maombi ya kufanya tathmini zaidi ya 6,000 na tunategemea kupata maombi zaidi, hususan katika kipindi hiki ambacho kuna mwamko wa ujenzi wa viwanda,” anasema Mulinda.