27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

BAJETI 2017/2018: NI BAJETI YA UJENZI

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA


WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amesoma mbele ya wabunge, ukomo wa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/18 ya Sh trilioni 31.69, ambayo miradi mingi ya kipaumbele itakayotekelezwa ni ya ujenzi.

Wakati Dk. Mpango akiwasilisha mapendekezo hayo ya Serikali ya mpango wa maendeleo wa taifa na ya kiwango na ukomo wa bajeti ya 2017/18, alisema pia kwamba bajeti ya 2016/17 iliyokuwa ya Sh trilioni 29.5, haijatekelezeka kwa asilimia 100 kutokana na mambo mbalimbali.

Alisema baadhi ya mambo yaliyokwamisha utekelezaji huo, ni pamoja na mwamko mdogo wa kulipa kodi, matumizi hafifu ya mashine za risisti za kielektroniki (EFDs) na kuchelewa kupatikana kwa mikopo yenye masharti nafuu na ya kibiashara kutoka nje.

Sababu nyingine aliyoitoa ni majadiliano ya muda mrefu yaliyosababisha kuchelewa kupatikana fedha za washirika wa maendeleo.

Alisema hadi kufikia Februari 2017, makusanyo yote ya Serikali yalikuwa Sh trilioni 15.37 sawa na asilimia 79 ya malengo, kati yake mikopo ya ndani Sh trilioni 3.5 sawa na asilimia 78 ya malengo, misaada na mikopo nafuu Sh trilioni 1.25 sawa na asilimia 40 ya malengo.

Dk. Mpango alisema mikopo ya kibiashara kutoka vyanzo za nje ilitarajiwa kuwa Sh trilioni 2.1, lakini hadi sasa hazijapatikana.

Ili kukabiliana na changamoto zilizokwamisha utekelezaji wa bajeti hiyo, alisema hatua zilizochukuliwa ni kusimamia dhana ya kulipa kodi kwa hiari kupitia udhibiti wa matumizi  ya  mfumo wa EFDs, kuendelea na majadiliano baina ya Serikali na washirika wa maendeleo ili kuhakikisha fedha za misaada na mikopo nafuu zinapatikana kama zilivyoahidiwa.

 

“Ili kupata suluhu ya kudumu, Serikali kwa sasa inafanya tathmini ya ushirikiano na washirika wa maendeleo, kazi inayoongozwa na aliyekuwa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika.

“Hatua hii inatarajia kuimarisha ushirikiano na kuwezesha upatikanaji wa fedha za uhakika katika bajeti ya Serikali,” alisema.

Hatua nyingine, alisema ni kuendelea kutoa elimu juu ya umuhimu na faida za kulipa kodi kwa kutumia mitandao ya kielektroniki.

“Aidha, wizara, idara zinazojitegemea na wakala wa Serikali  wanahimizwa kutumia mabenki katika kukusanya maduhuli,” alisema.

Alisema pia wataendelea kusisitiza nidhamu katika utekelezaji wa bajeti kama ilivyoidhinishwa kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015.

Hatua ya mwisho alisema ni kuendelea kuwianisha mapato na matumizi kwa kuhakikisha mgawo wa fedha unaendana na upatikanaji wa mapato na kuendelea kuchukua hatua za kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.

 

MAENEO YA KIPAUMBELE

Dk. Mpango akiwasilisha mapendekezo hayo, alisema maeneo ambayo miradi yake itapewa kipaumbele ni ya makaa ya mawe Mchuchuma na chuma Liganga mkoani Njombe, ujenzi wa reli ya kati na kuboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATC).

Aliyataja maeneo mengine yaliyopewa kipaumbele kuwa ni ujenzi wa mitambo ya kusindika gesi kimiminika mkoani Lindi na uendelezaji maeneo maalumu ya kiuchumi.

“Hapa katika uendeshaji wa maeneo maalumu ya kiuchumi, tuna Kituo cha Biashara cha Kurasini, eneo maalumu la uwekezaji Bagamoyo na eneo maalumu la uwekezaji Mtwara,” alisema.

Waziri huyo aliendelea kuitaja miradi ya kielezo kuwa ni ununuzi na ukarabati wa meli katika maziwa makuu na uanzishwaji wa shamba la miwa na kiwanda cha sukari cha Mkulanzi.

Alisema miradi mingine ya kipaumbele ni ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, kufungamanisha uchumi na maendeleo ya watu, mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na kuhamishia shughuli zake Dodoma.

 

SURA YA BAJETI YA 2017/18

Dk. Mpango alisema katika mwaka 2017/18, Serikali inatarajia kukusanya Sh trilioni 31.69, kati yake mapato ya ndani yakijumuishwa ya halmashauri ni Sh trilioni 19.97 sawa na asilimia 63.

Kati ya mapato hayo ya ndani, yatokanayo na kodi yanatarajiwa kuwa Sh trilioni 17.10 sawa na asilimia 85.6 ya mapato ya ndani.

 “Aidha, mapato yasiyo ya kodi na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri ni Sh bilioni 2,183.4 na Sh bilioni 687.3 kwa mtiririko huo.

“Ili kuhakikisha upatikanaji wa mapato hayo, Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa mapato na kuziba mianya ya uvujaji wa mapato,” alisema Dk. Mpango.

Katika bajeti hiyo, washirika wa maendeleo wanatarajia kuchangia Sh trilioni 3.97 ambazo ni asilimia 12.6 ya bajeti yote.

“Misaada na mikopo hii inajumuisha fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, mifuko ya pamoja ya kisekta na ya kibajeti (GBS),” alisema Dk. Mpango.

Alisema pia Serikali inatarajia kukopa Sh trilioni 6.15 kutoka soko la ndani, ambazo kati yake Sh trilioni 4.94 ni kwa kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva (rollover) na Sh trilioni 1.20 sawa na asilimia moja ya pato la taifa ni mikopo mipya kugharamia miradi ya maendeleo.

Dk. Mpango alisema pia Sh trilioni 1.59 zinatarajiwa kukopwa kutoka vyanzo vya nje vyenye masharti ya kibiashara, zitakazotumika kuongeza kasi katika ujenzi wa miundombinu.

Kati ya fedha zitakazokusanywa, Sh Sh trilioni 19.7 ni kwa matumizi ya kawaida, ikijumuisha Sh trilioni 7,205.8 za mishahara ya watumishi wa Serikali na taasisi na Sh trilioni 9.46 kwa kulipia deni la taifa.

“Bajeti ya kulipia deni la taifa imeongezeka kwa asilimia 18.3 kutoka Sh trilioni 8 mwaka 2016/17 kutokana na kuiva kwa mikopo ya miaka ya nyuma iliyogharamia miradi ya maendeleo, ambayo fedha za kulipia mtaji na riba zimetengwa kwenye bajeti ya matumizi ya kawaida,” alisema Dk. Mpango.

Alisema matumizi mengineyo (OC) yametengewa Sh trilioni 3.03 ambazo kiasi cha Sh trilioni 2.08 ni matumizi yaliyolindwa na Sh trilioni 2.74 ni matumizi yanayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri.

Dk. Mpango alisema matumizi ya maendeleo yatakuwa Sh trilioni 11.99 ambazo Sh trilioni 8.96  ni fedha za ndani na Sh trilioni 3.02 fedha za nje.

 

AKIBA YA FEDHA ZA KIGENI

Dk. Mpango alisema hadi kufikia Desemba mwaka jana, akiba ya fedha za kigeni ilifikia Dola za Marekani milioni 4,325.6 kiasi ambacho kinatosheleza gharama ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa miezi minne na wiki mbili.

Alisema katika kipindi hicho, thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani ilibaki kuwa imara kufuatia usimamizi madhubuti wa sera za fedha na bajeti. Ilishuka kwa wastani wa asilimia 1.2 kutoka Sh 2,144.27 mwezi Desemba 2015 hadi Sh 2,170.44 Desemba 2016.

 

DENI LA TAIFA

Kuhusu deni la taifa, likijumuisha deni la ndani na nje, Dk. Mpango alisema liliongezeka kufikia dola za Marekani milioni 19,021.9 Desemba 2016 (Sh trilioni 42.45) ikilinganishwa na dola za Marekani milioni  18,459.3 (Sh trilioni 41.20) Juni 2016, sawa na ongezeko la asilimia 3.05, lakini likibaki ndani ya vigezo vyote vya uhimilivu.

“Napenda kusisitiza kuwa nchi kuwa na deni si dhambi, jambo muhimu ni kuhakikisha kuwa fedha tulizokopa zinatumika kujenga rasilimali ambazo ni msingi wa kuongeza uwezo wetu wa kuzalisha mali na kuendeleza taifa, lakini pia uwezo wa kulipa mikopo hiyo,” alisema.

 

MFUMUKO WA BEI

Dk. Mpango alisema wastani wa mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 5.2 mwaka 2016 ikilinganishwa na asilimia 5.6 mwaka 2015.

Alisema Januari mwaka 2016 wastani wa mfumuko wa bei ulipungua kutoka asilimia 6.5 hadi 5.0 Desemba 2016.

Dk. Mpango alisema Februari mwaka 2017, mfumuko wa bei ulifikia asilimia 5.5, ambapo wastani wa riba za mikopo ya mwaka mmoja ambayo hutolewa na mabenki ya biashara, ulipungua kutoka asilimia 14.22, Desemba 2015 hadi 12.87, Desemba 2016.

“Riba za amana za mwaka mmoja zilipungua kutoka asilimia 11.16 hadi asilimia 11.03 katika kipindi hicho, hivyo tofauti kati ya riba za mikopo na amana za mwaka mmoja imeendelea kupungua kutoka wastani wa alama 3.06 za asilimia, mwezi Desemba 2015 hadi alama 1.83 za asilimia mwezi Juni 2016,” alisema Dk. Mpango.

Alisema katika kipindi kinachoishia Desemba 2016, mauzo ya bidhaa na huduma za nje yalikuwa dola za Marekani milioni 9,381.6 ikilinganishwa na dola milioni 8.921.9 katika kipindi kama hicho mwaka 2015, sawa na ongezeko la asilimia  5.2.

Dk. Mpango alisema ongezeko hilo lilitokana na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa asilia, dhahabu, bidhaa za viwandani na mapato ya sekta za huduma, hususani utalii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles