Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Mkoa wa Dar es Salaam, umezindua kampeni ya ‘Dar es Salaam ya Kijani’ iliyolenga kurudisha mitaa na majimbo yanayoongozwa na vyama vya upinzani.
Pamoja na mambo mengine, kampeni hiyo inalenga kuweka mikakati kuanzia ngazi za jumuiya zote za mkoa huo, kuanza kujipanga kuelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.
Akizugumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika Chuo Kikuu Kishirikishi cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Kilakala, amesema kuwa kampeni hiyo itachochea ustawi zaidi wa CCM katika Mkoa wa Dar es Salaam na kuzidi kukita mizizi katika ngazi zote kuanzia mkoa hadi majimbo, wilaya hadi kata, na matawi hadi mitaa.
“Kampeni yetu ya Dar ya Kijani kuelekea serikali za mitaa 2019, ni kampeni kabambe kwa ajili ya kuirejeshea CCM mitaa iliyopotea katika uchaguzi uliopita ambayo kwayo itatusaidia kupata ushindi mkubwa kimkoa katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 wa udiwani, ubunge na urais.
“Sote ni mashuhuda kwamba katika uchaguzi uliopita wa 2014 wa Serikali za Mitaa na ule Mkuu wa 2015 tulipoteza baadhi ya mitaa, kata na majimbo yaliyokuwa yakishikiliwa na CCM na sababu za kupoteza huko zinajulikana, sina haja ya kuzirejea sasa.
Hivyo sisi vijana wa CCM tunatambua kuwa ndiyo damu na roho ya chama chetu, na kwamba tunao wajibu wa asili wa kusafisha njia katika kutimiza malengo ya uwepo wa vyama vya siasa kikatiba ya kushika dola,” amesema Kilakala.
Aidha, amesema kampeni hiyo itashuka katika wilaya, kata na matawi yote jijini Dar es Salaam, ili kuhakikisha kila Kijana wa UVCCM anawajibika ipasavyo kuhakikisha falsafa ya Dar es Salaam ya kijani yaani Dar es Salaam ya CCM inaenea kwa wanachama na wananchi ili ikifika wakati wa uchaguzi tuvune wapiga kura wa kutosha.