UMOJA wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM), umesikitishwa na vitendo vya wabunge wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) bungeni muda mfupi kabla ya Rais Dk. Magufuli kulifungua rasmi Bunge la 11 mwishoni mwa wiki.
Wabunge hao wa Ukawa waliwazomea baadhi ya viongozi walioongozana na Rais Dk. John Magufuli na kuamriwa na Spika wa Bunge Job Ndugai watoke nje.
Wabunge hao wa upinznai walifanya hivyo kama hatua ya kutokubaliana na kufutwa Uchaguzi wa Zanzibar na kutaka atangazwe Maalim Seif Sharif Hamad kama mshindi wa uchaguzi huo wa Oktoba 25, mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa jana na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, ilieleza kuwa kitendo hicho ni cha kuhuzunisha na kufedhehesha.
“Kilichofanyika ndani ya ukumbi wa Bunge si tabia na desturi njema… Bunge si jukwaa la vituko au maigizo bali ni eneo lenye kujenga na kuonyesha ukamilifu na ustawi wa demokrasia na umakini wa kila mbunge na vyama vyao,” alisema Shaka.
Alisema UVCCM inaona kitendo hicho kama kielelezo cha ukomo na upeo wa hekima za wabunge ambao wameaminiwa na wananchi kuwawakilisha kwenye moja ya mihimili ya dola.
“Tukio lile ni ishara na dalili tosha ya wabunge wa Kambi ya Upinzani kuwa hawana dhamira njema ya kuijenga nchi, kupigania maendeleo ya Taifa wala kuheshimu dhamana na amana waliyokabidhiwa na wananchi kwa njia ya demokrasia ya uchaguzi,” alisema Shaka.
Alisema ni aibu iliyovuka mipaka kwa wabunge na vyama vyao kufanya kitendo hicho huku.
Alidai kitendo hicho kinaonyesha wabunge hao kupungukiwa ukomavu wa siasa, uwerevu, maarifa na busara za kutosha.
“UVCCM tunawaomba Watanzania kukitazama kitendo hicho na kukiona kama mwanzo wa harakati za kuzorotesha maendeleo na kasi ya mafanikio iliyopangwa na serikali ya awamu ya tano,” alisema Shaka.
Alisema wanaamini viongozi na vyombo husika vitajipanga kukabiliana nao kuzuia aibu kama hiyo isiendelee kutokea.
UVCCM pia umempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa hotuba aliyoitoa katika uzinduzi rasmi wa Bunge la 11, Dodoma.
“Hotuba ya Rais Dk. Magufuli licha ya kuwa na umakini, matarajio, matumaini, mwelekeo, dira na vipaumbele muhimu pia imebeba malengo mahususi katika kuwatumikia wananchi ikiwamo kuimarisha huduma za jamii, maendeleo ya sekta ya utawala bora, haki na demokrasia, kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na uhusiano wa kimataifa,” alisema Shaka.