NA MWANDISHI WETU,
SIKU moja baada ya Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), kutangaza kuzui mkutano mkuu maalumu wa CCM utakaofanyika Julai 23, mwaka huu, vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) nao wamejibu mapigo.
Umoja huo wa vijana wa CCM umesema, ikiwa Bavicha watathubutu kufanya vurugu hizo wanaweza kujuta na UVCCM haitasita kupita juu ya nyayo zao ili kukihami chama chao.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa umoja huo, Shaka Hamdu Shaka, alisema kama Bavicha wataamua kuendeleza siasa za kishetani zinazohusisha hujuma, kutishia maisha, kujenga hofu kwenye jamii au kuiingiza nchi katika vurugu, watawakabili kwa nguvu zao.
Alisema ikiwa baraza hilo limeelekezwa na viongozi wao kufanya siasa za vurugu, mapigano au ghasia kama njia ya kujijenga kisiasa, UVCCM itajibu mapigo kwa gharama ile ile watakayoitumia.
“Hatutaona muhali kupita njia zilizotumiwa na wapiganaji wa Maumau wa Kenya ili kukihami chama, kulinda viongozi wake na kupigania hadhi na heshima yetu,” alisema Shaka.
Alisema mataifa yote yaliyoendelalea kiuchumi na kidemokrasia yamefikia malengo yake baada ya kutenganisha vipindi vya siasa na vya kujijenga kiuchumi hivyo, Tanzania nayo haitakubali kuendeleza malumbano ya kisiasa na kupoteza muda kwenye mambo ambayo msimu wake umepita na kuacha kusaka maendeleo.