25.5 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Utelekezwaji watoto unavyorudisha nyuma juhudi za wanufaika wa TASAF

Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro

KWA miongo kadhaa sasa kumekuwa na juhudi mbalimbali za Serikali za kuhakikisha inapunguza tatizo la umasikini uliokithiri nchini.

Juhudi hizo zimeendana na kuanzishwa kwa mifuko na taasisi kadha wa kadha, zote lengo lake likiwa ni kupunguza umasikini wa kaya ama mtu mmoja mmoja.

Kati ya mifuko hiyo iliyoanzishwa na serikali kwa muda tofauti tofauti, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), kwa kiasi kikubwa umefanikiwa kufikia maisha ya kaya nyingi ambazo ni masikini nchini.

Ikumbukwe pamoja na shughuli nyingine, mifuko ya maendeleo ya jamii hutoa mchango wa fedha moja kwa moja kwa walengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi midogo ambayo husimamiwa na jamii na pia husaidia kujenga uwezo wa kaya maskini na makundi maalum.

Mifuko ya maendeleo ya jamii imeonekana kuwa chombo cha pekee na chenye thamani kwa ajili ya kuwafikia moja kwa moja watu walio katika ngazi ya jamii na kutumia jamii yenyewe, asasi zisizo za serikali, sekta binafsi, na taasisi za serikali kufanikisha utekelezaji.

Mifuko ya Jamii hutumika kukidhi mahitaji na majukumu mbalimbali ya haraka, kama vile, ujenzi na ukarabati wa mifumo ya maji na maji taka, ujenzi wa shule na zahanati, miradi ya lishe kwa wanawake na watoto, ujenzi wa barabara za vijijini na kusaidia miradi ya kiuchumi.

Katika ya kaya zilizowezeshwa na Tasaf nchini, zipo ambazo zimeinuka na kutoka katika hali ya kutokuwa na uhakika na hata mlo mmoja kwa siku na kufikia kwenye hali ya kujitosheleza kwa chakula na kuwa na miradi ya ufugaji, biashara na hata kuishi kwenye makazi yaliyo bora.

Mfumo wa fedha za Tasaf unalenga kaya moja kwa moja, lakini ambao hukabidhiwa fedha hizo ni kina mama na baadaye kwenda kupangiwa matumizi na familia.

Hata hivyo, mkoani Kilimanjaro na hususan Manispaa ya Moshi, Mtanzania Digital, imeshuhudia wanufaika wengi ambao ni akinamama wa familia wakiwa wametekelezewa wajukuu.

Mwajabu Soma (56), ana watoto saba na huku akikiri kuwa fedha za Tasaf zimemuwezesha kutoka kwenye kula mmoja mmoja hadi kuwa na uhakika wa milo mitatu kwa siku.

“Ninaishi na wajukuu watano hapa, watoto wangu waliwaleta hapa na kunitelekezea,” anasema Mwajuma.

Anasema wajukuu zake hao wanasoma na kupitia fedha anazopata Tasaf, anaweza kuwanunulia daftari na mahitaji mengine ya shule.

“Watoto wangu wapo tu huko wanatafuta maisha, wengine hata mawasiliano na nyumbani ni shida, kwahiyo mimi ndo kila kitu kwa watoto wangu hawa,” anasema Mwajuma.

Mmoja wa wanufaika wa Tasaf akiwa katika mradi wake wa nyanya| Picha na Maktaba.

Anasema alipoingia kwenye mradi huo alikuwa akipokea Sh 68,000 lakini kwa sasa kila awamu anapokea Sh 80,000.

Pamoja na changamoto ya mzigo wa wajukuu ambayo inamfanya asiweze kuzungusha fedha anazopokea kwenye miradi ya kuizalisha fedha hiyo, anasema sasa anauhakika wa milo mitatu kwa siku ikilinganishwa na awali ambapo alikuwa anatumia mlo mmoja kwa siku.

Kwa upande wake, Halima Kondokaya (52), mkaazi wa Mtaa wa Matindigani, Kata ya Pasua katika Manispaa ya Moshi, anasema yeye anaishi na wajukuu watatu.

Anasema pamoja na mambo mengine, fedha anazopata Tasaf inambidi aziweke kwenye vikundi vya kukopeshana ili ziweze kuzaliana.

Anasema katika vikundi hivyo ambavyo fedha hizo hukaa kwa takribani siku 10, zinamuwezesha kuendesha maisha na kulea wajukuu zake.

Donata Temba (53) ambaye ni mkaazi wa mtaa wa Katanini Kata ya Magereza, anasema anaishi na wajukuu tisa ambao ameachiwa na watoto wake.

Anasema alivyoanza kupokea fedha za Tasaf ambazo zilikuwa ni Sh 60,000 alia nzilianzisha mradi wa kuku, ambapo walipokuwa wakizalia na kuuza, aliweza kununua mbuzi na baadaye nguruwe.

Hata hivyo kwasababu ya mzigo wa kulea wajukuu, kwa kiasi kikubwa anashindwa kuendeleza miradi hiyo kutokana na kuuza mifugo wake mara kwa mara ili akidhi mahitaji ya shule kwa wajukuu na pia wapate chakula na mahitaji mengine.

Fariji Mishael, ambaye ni Mkurugenzi wa Mifumo na Mawasiliano wa Tasaf, anasema jamii inapaswa ijitazame upya juu ya tatizo la wajukuu kutekelezwa kwa bibi na babu zao.

Pamoja na mambo mengine, anasema fedha zinazotolewa kwa ajili ya kunusuri kaya mbalimbali, zimesaidia kwakiasi kikubwa kupunguza iaidi ya watoto wanaoacha shule.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Rashid Gembe, anasema jukumu la kulea wazazi lipo kwa watoto wao.

“Sasa hao watoto wanaotekeleza wanao kwa wazazi wao wanakuwa wamefanya makosa mara mbili, kwanza wamekwepa jukumu la kulea watoto wao na pili wanakwepa jukumu la kulea wazazi wao, hili ni suala ambalo linahitaji elimu,” anasema Gembe.  

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles