Mafundi wakifungua vifaa vya jukwaa la Tamasha la Tigo Fiesta baada ya kuahirishwa kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wa waandaaji.
JOSEPH SHALUWA NA AGATHA CHARLES-DAR ES SALAAM
TASNIA ya burudani Bongo inaendelea kukua kwa kasi na muziki wa Bongo Fleva unaonekana kuleta mafanikio kimuziki na kimaisha kwa wasanii wa sanaa hiyo.
Watu wanaofuatilia masuala ya burudani wanasema wakati mafanikio hayo yakiendelea kupaa huwezi kuyatenganisha na tamasha kubwa la burudani la kila mwaka linalokwenda kwa jina la Fiesta linaloandaliwa na Kampuni ya Prime Time Promotion chini ya Kampuni ya Clouds Media Group.
Hata hivyo katika hali ya kushangaza, wakati tamasha hilo linalokusanya pamoja wasanii wa muziki wa Bongo fleva na mashabiki likipangwa kuhitimishwa katika viwanja vya Leaders Jijini Dar Es Salaam jana baada ya kufanyika katika mikoa mingine nchini, ghafla likahairishwa.
Kuahirishwa kwa tamasha hilo kuja baada ya maandalizi yote kuwa tayari, huku baadhi ya mashabiki wakiwa wameshanunua tiketi zao kumeibua hisia tofauti.
UTATA
Wakati waandaji wenyewe wakikataa kutaja sababu za kuchukua uamuzi huo zaidi wakiishia tu kueleza kuwa;”wamelazimika kuhairisha onesho la Dar kwa sababu zilizo nje ya uwezo wao”, kitendo hicho kimewaweka wafuatiliaji wa tamasha hilo njia panda.
Wapo ambao wamejenga hisia kwamba pengine kuna jambo baya limewapata au wamehujumiwa.
Jana kabla ya Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tigo Fiesta 2018, Sebastian Maganga kuzungumza na Vyombo vya Habari jana na kueleza sababu hizo zilizo nje ya uwezo wao, juzi usiku ilianza kusambaa barua inayodaiwa kuandikwa na Ofisa Utamaduni wa Halmashauri ya Kinondoni, ikieleza sababu za kufuta kibali cha kufanyika tamasha hilo.
Sababu hizo zilitokana na kile kilichoelezwa kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi na wagonjwa waliolazwa hospitali wakilalamikia matangazo yaliyoambatana na muziki uliokuwa ukipigwa kwa sauti kubwa siku tatu kabla ya kufanyika kwa tamasha hilo.
Barua ya Ofisa Utamaduni wa Halmashauri hiyo, F. Kombe ambayo iliandikwa kwenda kwa Mkurugenzi, Clouds Media ilielekeza nakala pia kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Oysterbay pamoja na taarifa kwa Ofisa Mtendaji Kata ya Msasani.
“Ofisi imepokea malalamiko ya wananchi na wagonjwa waliolazwa hospitalini kutokana na matangazo yaliyoambatana na muziki unaopigwa kwa sauti kubwa kutoka uwanja wa Leaders Club jambo ambalo linahatarisha afya za wagonjwa wakiwemo wa moyo,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.
Barua hiyo ilieleza kuwa kutokana na hilo ilifuta kibali kilichotolewa Novemba 22 cha kufanya Fiesta viwanja vya Leaders na kuihamishia uwanja wa Tanganyika Peakers –Kawe.
Pamoja na hayo wataalamu wa burudani na wale wanaoujua nguvu ya Fiesta, sababu zinazoelezwa kuwa “zipo nje ya uwezo wao” au zile zilizoelezwa na Ofisa Utamaduni huyo, hawazipi uzito kwa hoja kwamba miaka yote ikiwamo mwaka jana lilifanyika na hakukuwa na hayo yaliyojitokeza sasa.
FEDHA ZARUDISHWA
Akizungumza na waandishi wa habari jana Maganga ambaye aliambatana na jopo la kamati ya Fiesta wakiwemo kutoka Tigo pamoja na wasanii Maganga alitoa ufafanuzi wa namna mashabiki waliokata tiketi hizo watakavyorudishiwa fedha zao.
“Natoa rai kwenu kwamba tiketi ambazo mlishanunua kwa fedha 15,000 katika vituo mbalimbali kuzunguka jiji la Dar es Salaam ni tiketi ambazo zinapatikana kwa hiyo mnaweza kwenda kwenye vituo ambavyo mlinunua fedha hizo na mtarejeshewa fedha zenu, lakini mlionunua tiketi kupitia Tigo pesa na mitandao mingine zitarejeshwa kwenye mitandao yenu,” alisema Maganga.
Manganga pia mbali na kumshukuru Mungu kwa kuwalinda na kuwapitisha kwenye msimu wa tamasha hilo katika miji takribani 14 kuzunguka Tanzania, pia aliishukuru Serikali, viongozi wa mikoa mbalimbali pamoja na wadau waliohusika na tamasha hilo.
Maganga alisema wanafahamu wakazi wa jijini hilo na maeneo jirani walijiandaa na kujipanga vyema kupata burudani kutoka kwa wasanii hao lakini aliomba radhi kwa wote waliojitoa kwa hali na mali akisisitiza harakati za burudani ni endelevu.
JE NI BARUA YA CAROL NDOSI?
Wakati Clouds wenyewe wakishindwa kuweka wazi msingi wa kuahirisha tamasha hilo, lakini pia baadhi wakiona kile kilichoelezwa na na Ofisa Utamaduni kama ni jambo linaloacha maswali, wapo wanaojiuliza iwapo barua iliyoandikwa na mjasiliamali muandazi wa tamasha la Nyama Choma Festival, Carol Ndosi nayo imechangia kuahirishwa kwa tamasha hilo.
Katika barua hiyo ya wazi iliyokuwa ikisambaa katika mitandao ya kijamii, Ndosi alimwandikia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akilalamikia ruhusa iliyokuwa imetolewa kufanya tamasha la Fiesta huku la kwake likiwa limezuiwa kufanyika katika viwanja hivyo takribani miaka miwili iliyopita na kudai kuna mgongano wa kimaslahi.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Ndosi ambaye a alithibitisha kuandika barua hiyo ya wazi alisema ilikuwa ni kuelezea namna jina la tamasha lake lilivyoathiriwa wakiwemo wafanyakazi na wadai kutokana na kusitishwa kwa Nyama Choma Festival.
Jana baada ya tamasha la Fiesta kusitishwa Ndosi aliandika kuwa alipokea ujumbe nyingi kuhusu kusitishwa kwa tamasha hilo.
“ Napokea jumbe nyingi sana zenye hisia tofauti. Naomba kwanza nitangulize pole zangu za dhati kwa @CloudsMediaLive kwani nawaelewa sana kama muandaji wa tamasha, na kupitia wanayopitia wao sasa ingawa sisi tulisitishwa wiki moja kabla. I wouldn’t wish that on anyone. Anyone,” aliandika Ndosi.
Novemba 22, baada ya Carol kuandika barua yake hiyo, Katika ukurasa wa Twitter, Makonda aliweka ujumbe mwaka huu uliosomeka;
“Nasikia kuna barua. Barua andika kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Humu mitandaoni ofisi haina anwani”.
HASARA NI KUBWA
Jambo linalozidisha maswali kuahirishwa kwa tamasha hilo ni kutokana na hasara kubwa ambayo waandaaji wamepata pamoja na wadau wengine walioshirikiana nao kwa namna moja ama nyingine katika tamasha hilo.
Fiesta kwa ukubwa wake, ni tamasha linalokuja na neema kwa wafanyabiashara wa chakula na vinywaji katika maeneo wanayofanyia onyesho, hivyo kusababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara waliotayarisha vyakula kwa ajili ya kuuza kwenye onyesho.
Mchungaji Silvanus Mumba kupitia ukurasa wake wa Twitter alindika kuwa;
“Habari zenu? Nina mtu namjua alikuwa na kibanda leo kwenye shughuli ya Fiesta pale Leaders, kuku (100) bila kusahau nyama fillet ya mishkaki, utumbo supu ndizi mikungu ya kutosha. Kwa anayehitaji kwa bei ya hasara ampigie (ameweka mawasiliano yake),”
HASARA PRIME TIME
Lazima kuna wasanii ambao wameshapewa malipo ya awali; wengine wakiwa wamekataa shoo kwa siku ya jana wakijua wana kazi ya Fiesta, kuna mabaunsa, matangazo, kutayarisha jukwaa nk
ILIVYOKUWA
Fiesta yenye kauli mbiu tofauti kila mwaka, mwaka huu imekuja na ‘Vibe kama lote’ ilifanya vizuri katika miji tofauti tangu msimu wa mwaka huu ulivyoanza wiki kadhaa zilizopita.
Mji wa kwanza ulikuwa ni Morogoro ukafuatiwa na Sumbawanga, Iringa, Songea, Mtwara na Moshi Tanga, Mwanza, Musoma, Kahama, Muleba, Arusha, Singida na Dodoma.
Baada ya kumalizika maonyesho ya mikoa hiyo, moto ulitarajiwa kuwaka jana katika Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar es Salaam.