Eliya Mbonea, Arusha
Watanzania na wadau wa utalii nchini wametakiwa kuwekeza katika zao la utalii wa utamaduni wa asili nchini ili kukuza utalii.
Kauli hiyo imetolewa leo mjini Arusha na Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Suzan Mlawi alipofungua Tamasha la Urithi Festival kwa niaba ya Waziri Dk. Harrison Mwakyembe.
Tamasha hilo linafanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha likishirikisha tamaduni mbalimbali za makabila yanayopatikana mkoani Arusha.
Akizungumza wakati wa ufunguzi Katibu Mkuu Mlawi amesema, utalii wa utamaduni umekuwa kivutio duniani pote hivyo ni vyema Wadau wa utalii wakautumia kama fursa ya kujiletea maendeleo.
“Utalii wa utamaduni duniani umekuwa kivutio kioya kutokana na jamii nyingi kupoteza utamaduni wao na hivyo kuwafanya watu kusafiri maeneo mbalimbali ili kujifunza tamaduni nyingine,” amesema Mlawi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tamasha hilo, Professa Audax Mabula, amesema, zao hilo jipya la utalii litaongeza ajira na kufungua soko jipya la bidhaa.