29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

UTAFITI: WATOTO WAVIVU HUWA NA MIFUPA DHAIFU

JOSEPH HIZA Na MASHIRIKA


NI wachache mno wasiojua umuhimu wa mazoezi kwa afya ya binadamu kwa vile ni suala linalozungumzwa na kuhimizwa mno na wataalamu wa afya.

Sababu ni faida nyingi zinazotokana na kufanya mazoezi au kwa maneno mengine kujishughulisha kimwili.

Yana umuhimu mkubwa hasa katika nyakati hizi, ambazo ujio wa sayansi na teknolojia umemrahisishia binadamu mambo mengi na hivyo kumsababishia uvivu unaoshuhudia kuibuka kwa maradhi mengi yanayotokana na staili hiyo mbaya ya maisha.

Mazoezi hupunguza lehemu isiyotakiwa mwilini, husaidia kupunguza uzito, huimarisha mifupa, hupunguza shinikizo la damu, huondoa sonona (depression).

Kadhalika mazoezi hupunguza makali ya ugonjwa wa pumu, kisukari, huboresha afya ya ubongo, kupunguza maradhi ya moyo, saratani, kuzuia kiharusi.

Hali kadhalika huboresha mfumo wa usingizi, uwezo wa kufanya tendo la ndoa, husaidia ukuaji wa mimba unaotakiwa kiafya na mengineyo mengi yanayoweza kujaza ukurasa nzima.

Ni kwa sababu hizo. mazoezi huhimizwa mno kwa watu mbalimbali hasa wenye umri wa utu uzima pamoja na wajawazito.

Kwa maana hiyo ni mara chache watoto kuhimizwa kwa kiwango sawa na watu wazima kufanya mazoezi au kujishughulisha.

Sababu ya unadra huo kwa watoto ni kutokana na wengi kutogundua bado au kukosa ufahamu kuhusu umuhimu wa mazoezi kwa watoto.

Lakini pia kuwahimiza watoto kuamka na kujijengea utamaduni wa kufanya mazoezi si kitu rahisi.

Lakini utafiti mpya umethibitisha kuna hitaji la kweli kwa watoto kuachana na simu zao za mikononi na kujishughulisha nje– na si tu kwa ajili ya kuzuia unene.

Vijana wana uwezekano mkubwa wa kuugua miteguko au mivunjiko ya mifupa iwapo hawatakuwa wakijishughulisha, wanasayaansi wanaonya.

Utafiti ulioendeshwa nchini Canada uligundua kuwa watoto waliokosa kiwango kinachokubalika cha kujishughulisha kila siku walikuwa na mifupa dhaifu kuliko wenzao walioendekeza ukakamavu.

Mwanasayansi Leigh Gabel kutoka Chuo Kikuu cha British Columbia nchini humo, anasema: “Tulibaini kuwa vijana ambao hawajishughulishi wana mifupa dhaifu.

“Hiyo inasikitisha mno kwa vile nguvu ya mifupa ni muhimu kuzuia utegukaji au uvunjikaji wao.

“Vitoto ambavyo vinakaa tu bila kujishughulisha haviikomazi mifupa ya miili yao kwa namna ambayo ingeimarisha nguvu ya mifupa yao hiyo.”

Watafiti walipima kujishughulisha kimwili na nguvu ya mifupa ya vijana wadogo 309 katika wakati muhimu wa makuzi yao.

Wavulana waliosimamiwa walikuwa wa miaka kati ya 12 na 16 wakati dirisha la miaka minne kwa wasichana lilianza wakati walipofikisha umri wa miaka 10.

Wakati huu wa maisha yao unahesabiwa kuwa muhimu kwa vile asilimia 36 ya mifupa ya binadamu huundwa katika kipindi hicho cha miaka minne.

Walitumia picha za xray za 3D X kulinganisha tofauti baina ya vijana ambao walifanya mazoezi na wale ambao waliendekeza uvivu.

Watoto ambao walikuwa na mazoea ya kila siku ya kujishughulisha kunakokubalika kwa dakika 60 kwa siku walilinganishwa na wale waliofanya kidogo chini ya nusu saa.

Wakati wavulana walionekana kuwa na mifupa mikubwa na yenye nguvu kipindi chote cha utafiti, jinsia zote zilikuwa na majibu sawa kuhusu umuhimu wa kujishughulisha kimwili.

Sote tunafahamu watoto huiga masuala ya kijamii kutoka kwa wazazi wao – maneno, imani na hata tabia ya sauti.

Lakini Januari mwaka huu, wataalamu wa afya walionya kuwa ni wazazi wachache waliokuwa na ufahamu namna mazoea yao ya kikakamavu yanavyochochea hamasa hiyo kwa kizazi cha vijana.

Watafiti wa Serikali ya Marekani walibaini kuwa watoto walifanya zaidi mazoezi iwapo wazazi wao walikuwa na utamaduni huo.

Nguvu ya mfupa ni muunganiko wa ukubwa wa mfupa, uzito (density) na muunganiko wa mifupa, watafiti waliandika katika Jarida la Mifupa na Utafiti wa Madini.

Mifupa dhaifu inajulikana kwa kuongeza hatari ya maradhi ya mifupa, ambayo kwa kitaalamu huitwa osteoporosis, hali ambayo huathiri watu wazima milioni tatu nchini Uingereza.

Professa Heather McKay, ambaye alishiriki katika utafiti huo anasema: “Ni muhimu kwa watoto na vijana kuondokana na mazoea ya kukaa kwenye skrini, sofa na kwenda kujishughulisha.

Hilo linakuja baada ya watafiti wa Hispania kukuta watoto ambao walikuwa na mazoezi chini ya saa moja kwa siku wakielekea kuwa na hatari ya kukumbwa na maradhi ya moyo kwa siku za usoni.

Utafiti wa mwaka 2013 ulionesha wale watoto walio na umri chini ya miaka 10 wakihitaji kufanya mazoezi kwa wastani kila siku kuwafanya mioyo yao kuwa na afya.

Januari mwaka huu, watafiti wa Norway walibaini watoto ambao wanashiriki katika mazoezi ya viungo walikuwa na nafasi nzuri ya kuwa na afya njema ya akili.

Vijana waliofanya mazoezi mara kwa mara wana uwezekano mdogo kukumbwa na maradhi ya akili kama ilivyo kwa watu wazima, wanasayansi walibaini.

Osteoporosis kwa ufupi?

Osteoporosis ni maradhi ya mifupa yanayotokana na kupungua kwa protini na madini kwenye mifupa.

Hali hii husababisha mifupa kuwa milaini na myepesi, ambapo inaweza kuvunjika kirahisi.

Kipindi cha utoto hadi kufikia umri wa miaka 30 ni muhimu ambacho mifupa hujijenga zaidi.

Dalili za maradhi hayo ni kuteguka hovyo, kukatika mifupa hovyo, maumivu makali ya mifupa na kadhalika.

Mbali ya kukosa mazoezi, upungufu wa vitamin kwa ujumla lishe duni inachangia kwa kiasi kikubwa katika udhaifu wa mifupa.

Ugonjwa huu pia unawapata wanawake zaidi kuliko wanaume. Utafiti unaonesha kuwa asilimia takribani 25 ya wanawake waliokwishafikia kukoma kwa hedhi wanapata matatizo ya udhaifu wa mifupa.

Ni muhimu kula mlo uliosheheni madini ya calcium, phosphorus, shaba pamoja na vitamini C, D, E na B12, kufanya mazoezi na inapobidi kupata ushauri wa tabibu.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles