RAMADHAN HASSAN– DODOMA
UTAFITI unaonesha kila watoto 100 waliopimwa ugonjwa wa selimundu 15 ama 20, wamekutwa na vinasaba vya ugonjwa huo huku Kanda ya Ziwa ikitajwa kuwa na wagonjwa wengi.
Akizungumza jijini Dodoma juzi kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali,Profesa Abeid Makubi,Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wazee na Watoto,Dk.James Kiologwe wakati wa hitimisho la mwezi wa kuelimisha jamii juu ya ugonjwa wa huo.
Alisema utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2015, unaonesha kati ya watoto 100 waliopimwa ugonjwa wa selimundu watoto kati 15 mpaka 20 wamekutwa na vinasaba vya ugonjwa huo.
Alisema Tanzania ina wagonjwa 200,000 wa ugonjwa huo, lakini Serikali imechukua hatua kadhaa kukabiliana na ugonjwa huo ikiwemo kuunda kikosi kazi cha wataalamu wa kukabiliana na ugonjwa huo.
Alisema pia mpango wa Serikali ni kuhakikisha kila hospitali ya mkoa inakuwa na kliniki kwa ajili ya kupima ugonjwa wa Sikoseli.
Dk.Kiologwe pia alisema jumla ya watu 1000 huzaliwa na ugonjwa wa Sikoseli kila siku duniani.
Mkurugenzi huyo alieleza Tanzania ni nchi ya tano duniani kuwa na idadi ya wagonjwa wengi wa Sikoseli huku ikishika nafasi ya nne barani Afrika.
“Nchi zenye wangonjwa wengi duniani ni Nigeria,India, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),Angola na Tanzania,ambapo kwa Afrika Tanzania inashika nafasi ya nne hali inayopaswa kutiliwa mkazo zaidi kuhakikisha ugonjwa huu unazuiwa,”alisema
Alisema nchini kila watoto 100 wanaozaliwa,8 kati yao wana ugonjwa huo.
Alisema juhudi nyingi zinazofanywa na wizara kuelekeza nguvu za uelimishaji jamii juu ya ugonjwa huo ,jamii bado haina uelewa wa kutosha.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya ndani kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,Dk.Elisha Osati alisema walitumia mwezi mmoja kutoa elimu kwa jamii katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa ambapo kati ya watoto 1,800 waliowapima 360 wamewakuta na vinasaba vya ugonjwa huo.