HASSAN DAUDI NA MITANDAO
WAKATI uchoraji wa ‘tattoo’ ukizidi kujizolea umaarufu kila kukicha huku ikielezwa asilimia 40 ya vijana wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 29 wanavutiwa na utamaduni huo, utafiti umeonyesha asilimia kubwa ya wanaochora huwa na matatizo ya afya ya akili.
Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Miami kwa kushirikiana na kile cha Florida, nchini Marekani ndio uliokuja na matokeo hayo mapya.
Taarifa zilizochapishwa na gazeti maarufu la mtandaoni la nchini Uingereza, Daily Mail zinaeleza utafiti huo ambao umechukua zaidi ya miaka miwili tangu ulipoanza Julai, 2016, ulihusisha watu 2,008 waliokuwa wameipamba miili yao kwa michoro.
Wasomi hao wa kutoka Miami na Florida walieleza kuwa katika watu hao 2,008, waliohojiwa asilimia 50 walisema wana michoro miwili hadi mitano, huku asilimia 18 wakisema wana sita na kuendelea.
Watu hao waliulizwa maswali kadhaa kuhusiana na afya zao na ndipo wengi walipoonekana kusumbuliwa na ugonjwa wa akili na wengine walikiri kusumbuliwa na tatizo la kukosa usingizi.
Aidha, kutokana na majibu yao kwa watafiti, ilibainika pia kuwa wengi wao walikuwa wakijihusisha na tabia zisizokubalika katika jamii, ikiwamo uvutaji sigara, unywaji pombe n.k.
Kupitia majibu ya watu hao, watafiti waligundua pia kwamba wanaopenda kuchora ‘tattoo’ huwa si waaminifu katika mahusiano yao ya kimapenzi. Kwamba wengi wao ni ‘wachepukaji’.
Utafiti huo wa Miami na Florida ni kama umegongelea nyundo ule uliowahi kufanywa na Chuo Kikuu cha Rochester Medical Center mwaka 2001, ambao ulieleza namna vijana waliochora ‘tattoo’ walivyo wepesi kuingia katika uvutaji wa sigara, kunywa pombe na kuacha shule.
“Utafiti wa mwanzo ulionesha kabisa namna ambavyo kuna uhusiano kati ya kuwa na ‘tattoo’ na kujikuta kwenye tabia za ovyo,” alisema mmoja kati ya watafiti wa Chuo Kikuu cha Miami, Dk. Karoline Mortensen.
Hata hivyo, tafiti zao hizo zinapingana na madai ya mwanasaikolojia, Heather Silvestri, aliyewahi kusema ipo michoro inayoweza kumjenga mtu kiakili inapokuwa mwilini mwake.
“Tattoo zinazohusiana na afya ya akili ni kama zile zinazokukumbusha magumu uliyopitia, zinakupa nguvu na kukufanya upambane zaidi,” alisema Silvestri.
Kwa upande wake, jopo la utafiti la vyuo vikuu vya Miami na Florida linaamini matokeo ya utafiti wake huu mpya utawaongoza wataalamu wengine wa afya kuibua maswali kwa wagonjwa wao wanaowakuta na ‘tattoos’.