26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

Utafiti waibua mapya elimu ya msingi

Na TUNU NASSOR -DAR ES SALAAM

TAASISI  ya Utafiti  TWAWEZA, imetoa utafiti wake wa mwaka 2017 ambao, umeonyesha matumaini mapya kwenye sekta ya elimu ingawa bado idadi ya kujua kusoma na kuandika iko chini.

Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti huo, asilimia 14 ya wanafunzi wanaomaliza darasa la saba hawawezi kusoma hadithi ya Kiswahili ya darasa la pili.

Twaweza kupitia mradi wake wa Uwezo, ilifanya utafiti huo kubaini uwezo wa kusoma na kuhesabu kwa watoto wenye miaka 6 hadi 16.

Katika utafiti huo, watoto 48,530 wenye miaka sita hadi 16 walipimwa uwezo wao wa kusoma na kufanya hesabu rahisi za kiwango cha darasa la pili.   

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo jijini Dar es Salaam jana, Meneja Mradi wa Uwezo, Zaida Mgalla, alisema idadi ya watoto wa darasa la tatu wanaoweza kusoma hadithi hiyo imeongezeka mara mbili.

Alisema kwa mwaka 2011 watoto watatu kati ya 10 ndio waliweza kusoma hadithi ya Kiswahili ya darasa la pili ikilinganisha watoto sita kati ya 10 kwa mwaka 2017.  

Alisema ujuzi wa kusoma kiingereza uko chini na unazidi kushuka ambapo kwa darasa la tatu ni asilimia 15 na darasa la saba ni asilimia 47.

“Tathmini za miaka mitatu iliyopita, ujuzi wa kusoma kiingereza kwa darasa la saba inaonesha kushuka kwa viwango vya ufaulu ambapo mwaka 2014 ulikuwa ni asilimia 56 na mwaka 2017 ni asilimia 47,” alisema Zaida.

Aliongeza kuwa ujuzi wa kuhesabu kwa wanafunzi wa darasa la saba umeshuka kutoka asilimia 88 mwaka 2014 hadi kufikia asilimia 80 mwaka 2017.

Alisema kwa upande wa darasa la tatu ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 50 mwaka 2014 hadi kufikia asilimia 59 mwaka 2017.

“Kwa ujumla kiwango cha ujuzi wa kusoma na kuhesabu umeboreka kiasi kati ya mwaka 2011 na 2017, ambapo watoto wenye umri wa miaka 9 hadi 13 ukijumlisha na wasioenda shule umeongezeka kutoka asilimia 42 mwaka 2011 hadi kufikia asilimia 45 mwaka 2017,” alisema Zaida.

Alisema kuna tofauti kubwa kwenye matokeo ya kujifunza kati ya wilaya zenye ufaulu wa juu ukilinganisha na zenye ufaulu wa chini.

“Watoto saba kati ya 10 wenye umri wa miaka tisa hadi 13 walifaulu majaribio ya kusoma na kufanya hesabu kwenye wilaya zenye ufaulu wa juu ikilinganishwa na watatu kati ya 10 kwa wilaya zenye ufaulu duni ambapo ufaulu wa juu ni asilimia 73 katika wilaya ya Meru ukilinganishwa na asilimia 24 wilaya ya Nzega,” alisema Zaida. 

Alisema idadi ya watoto walio nje ya shule wenye umri wa miaka saba hadi 16 ni asilimia 11 na walio nje ya shule wenye umri wa miaka sita ni asilimia 22, asilimia 78 yao wanatoka katika familia duni.

“Asilimia 19 ya watoto walio nje ya shule wenye umri wa kati ya miaka 9 na 13 walifaulu majaribio ya mitihani mitatu iliyotolewa na Uwezo ukilinganisha na aslimia 60 ya wenye umri huo walioko shuleni,” alisema Zaida.

Aliongeza kuwa watoto walioko mijini walifanya vizuri kwa asilimia 70 ukilinganisha na wa vijijini kwa asilimia 59.

“Watoto wanaotoka katika familia duni walifanya vibaya katika majaribio hayo ukilinganisha na wenye uwezo wa kifedha ambapo masikini sana walifaulu asilimia 60, masikini kiasi walifaulu kwa aslimia 62 na wenye uwezo wa fedha walifaulu kwa asilimia 67,” alisema Zaida.   

Uandikishaji

Alisema kwa mwaka 2017 watoto wenye umri wa miaka sita, asilimia 78.4 waliandikishwa shule ambapo asilimia 41.2 waliandikishwa shule za awali na asilimia 37.2 waliandikishwa shule ya msingi.

“Kati ya watoto waliandikishwa asilimia 1.8 ni wenye mahitaji maalumu huku watoto wengine wenye mahitaji maalumu wenye miaka sita hadi 16 asilimia 28 wakiwa nje ya shule, asilimia 15.6 hawakuandikishwa na asilimia 12.4 waliacha shule kutokana na sababu mbalimbali,” alisema Zaida.  

Mazingira ya kujifunzia

Zaida alisema uwiano mwalimu kwa wanafunzi darasani ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 86 kwa shule za awali kulinganisha na inavyotakiwa kwa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 25.

“Kwa upande wa shule za msingi uwiano ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 44 ukilinganisha na sera ya elimu inayotaka mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45,” alisema Zaida.

Alisema kwa mwaka 2014 kwa shule za msingi ilikuwa uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 46, mwaka 2015 uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 44. 

utoro

Hata hivyo alisema watoto wengi wa shule za msingi wanaacha shule wakiwa madarasa ya mwanzoni, ambapo asilimia 70 ya watoto ya walioacha shule walifanya hivyo wakiwa madarasa ya mwanzo.

“Kwa mfano wastani wa watoto walioacha shule wakiwa darasa la kwanza ni asilimia 23.5 la pili asilimia 20 , la tatu ni asilimia 27.5 na darasa la saba walikuwa ni asilimia 4.5,” alisema.

Zaida aliongeza kuwa viwango vya ukaguzi wa shule kwa ajili ya kuthibiti ubora vinatofautiana kutoka wilaya moja hadi nyingine ambapo shule tatu kati ya nne zilizofanyiwa utafiti zilikaguliwa na wathibiti ubora mwaka 2017.

Ushiriki wa Wazazi

Akizungumzia ushiriki wa wazazi katika kufuatilia masomo ya watotoi wao, Zaida alisema nusu ya wazazi waliofanyiwa utafiti waliwatembelea walimu na watoto wao katika mwaka 2017.

“Wazazi tisa kati ya 10 wilaya Iringa walitembelea walimu na watatu kati ya 10 wilaya ya Nzega sawa na asilimia 32 walifanya hivyo,” alisema Zaida.

Aliongeza kuwa asilimia 21 tu ya wazazi ndio hukagua madaftari ya watoto wao huku asilimia 66 wanasoma pamoja na watoto wao ili kuwahasisha.

“Katika tathmini hii tumebaini kuwa watoto wenye mama waliosoma zaidi ndio wanafanya vizuri kuliko kwa wenye mama wasiosoma kabisa.

“Mfano watoto wenye mama aliyesoma hadi kidato cha nne na kuendelea walifaulu kwa asilimia 72, wenye mama darasa la saba asilimia 63 na wenye mama asiyesoma kabisa walifaulu kwa asilimia 54,” alisema Zaida.

chakula

Alisema kwa upande wa chakula ni shule moja kati ya nne za Tanzania  bara ndio zinatoa chakula kwa wanafunzi na kuna tofauti kubwa kati ya wilaya na wilaya.

“Mfano Wilaya Moshi ni asilimia 96.6 tofauti na wilaya za Rorya, Buhigwe na Ukerewe ambazo hazina shule zinazotoa chakula kwa wanafunzi sawa na asilimia sifuri,” alisema Zaida.

Alisema walihoji ni nani anayestahili kutoa chakula kwa wanafunzi na majibu yalikuwa ni asilimia 50 walisema ni wazazi, asilimia 18 walisema Serikali kuu, asilimia 12 ni wazazi na Serikali za vijiji na asilimia 13 walisema hawajui.

Aliongeza kuwa ni matarajio yao kuwa matokeo ya utafiti huo yanatoa maoni muhimu juu ya hali ya matokeo ya kujifunza Tanzania kwa viongozi na wadau wa sekta ya elimu.

“Takwimu hizi zinatoa changamoto kwa wadau kutafakari juu ya hatua zinazoweza kuchukuliwa kuboresha elimu ya watoto.

“Lengo la msingi la tathmini hiyo ni kukusanya takwimu huru juu ya viwango vya kusoma na kuhesabu kwa watoto wenye umri wa kwenda shule kwa kuzingatia kasi iliyopo ya maboresho ya sera.

“Hitaji la uwepo wa takwimu madhubuti ni muhimu ili kutathimini matokeo ya program mbalimbali za elimu sera na bajeti ni jambo muhimu ,” alisema Zaida.

Naye  Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, alisema uandikishaji wa wanafunzi katika shule umeongezeka katika utafiti huu.

“Wazazi wasikae nyuma katika kufuatilia mienendo ya watoto wao ikiwa ni pamoja na kukagua madaftari yao wanaporudi shuleni,” alisema Eyakuze.

Aliongeza kuwa jamii inatakiwa kuwa na utamaduni wa kusoma mbele ya watoto ili kuwajengea ari ya kusoma. 

Katika utafiti huo, tathmini ilifanyawa katika wilaya 56 za Tanzania bara, maeneo yaliyoidhinishwa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS)yaliyofikiwa ni 1,677 na kaya 25,532.

Watoto wenye umri wa miaka kati ya mitatu na 16 walioshiriki katika tathmini hiyo ni 64,639 kati yao watoto 48,530 wenye umri wa miaka sita hadi 16 walipimwa uwezo wao wa kusoma na kufanya hesaburahisi za kiwango cha darasa la pili. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles