LONDON, UINGEREZA
WATAFITI nchini Uingereza wanasema dawa za kupunguza makali ya Virusi vya Ukimwi (VVU) barani Ulaya na Amerika ya Kaskazini zimeboreshwa kiasi kuwa watu wanaoishi navyo kuweza kuishi karibu sawa na wasionavyo.
Wanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha Bristol nchini hapa, waliwachunguza watu wenye VVU wapatao 90,000.
Makadirio yao yanaonesha mtu mwenye umri wa miaka 21 aliyeanza matibabu mwaka 2008 au baadaye anaweza kuishi hadi kufikia umri wake wa miaka 70.
Hata hivyo, watafiti walionya kuwa wengi wanakosa tiba hizo za dawa za kuokoa maisha kwa vile hawajapima kubaini iwapo wameambukizwa VVU ili waanze matibabu mara moja.
Watafiti wanasema pamoja na umri huo kuwa chini ya wastani wa umri wa kuishi wa miaka 80 wa nchini Uingereza, wana matumaini utafiti huo utapunguza unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU na kuwasaidia kupata bima na ajira.
“Mchanganyiko wa tiba ya dawa za kurefusha maisha umetumika kutibu VVU kwa miaka 20, lakini dawa mpya zina kiwango kidogo cha athari (side effects), huhusisha utumiaji wa dozi chache, huzuia mazalio ya VVU na ni ngumu kwa VVU kugeuka sugu kwa dawa hizo,” mwandishi kiongozi wa utafiti huo, Adam Trickey wa Chuo Kikuu cha Bristol alisema.
Kwa mujibu wa takwimu za kimataifa watu wanaoishi na VVU duniani ni milioni 36, wengi wao wakitokea Afrika huku Ulaya na Amerika Kaskazini zikiwa na waathirika milioni mbili.