Na JUSTIN DAMIAN
KAMA ilivyo kwa baadhi ya nchi za Kiafrika, Tanzania ni moja kati ya nchi ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi ya kuridhisha.
Kwa mujibu wa takwimu za uchumi za Shirika la Fedha Duniani (IMF World Economic Outlook Database), Tanzania ni miongoni mwa nchi tano ambazo uchumi wake unakuwa vizuri kwa wastani wa asilimia 7.1
Nchi nyingine ambazo zinafanya vizuri kwenye ukuaji wa uchumi ni pamoja na ni Ivory Coast (asilimia 7.9) Senegal (asilimia 6.6), Djibouti (asilimia 6.5) na Ethiopia (asilimia 6.5).
Hata hivyo pamoja na mwenendo mzuri wa ukuaji wa uchumi kwa baadhi ya nchi za Kiafrika ikiwamo Tanzania, ukuaji huo umekuwa hauonekani kwa wananchi wa kawaida.
Wakati tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa, ukuaji wa kiuchumi unatarajiwa kuimarika katika Bara la Afrika wakati ambao sera, sheria na kanuni zikiwa dhaifu na hivyo kufanya makampuni ya kimataifa, watawala na wafanyabiashara wenye ukwasi kunufaika na ukuaji huo huku wananchi wa kawaida wakibaki kama wasindikizaji.
Ili kuweza kuboresha maisha ya watu wake, nchi za Kiafrika hazina budi kuhakikisha kuwa zinatoza kodi stahiki lakini katika hali ya kushangaza, matajiri wamekuwa hawalipi kodi au wanalipa kidogo sana. Upo ushahidi wa tafiti unaoonyesha kuwa matajiri huficha fedha walizozipata kwa njia haramu ikiwamo kukwepa kodi nje ya nchi kwenye mataifa ambayo hutoza kodi ndogo (Tax haven) huku yakilinda siri za wateja kwa kutozitoa kwa mamlaka zozote zile. Inakadiriwa kuwa asilimia 30 ya utajiri wa Afrika umefichwa nje ya bara hili.
Kwa kipindi kirefu utoroshwaji wa fedha kutoka nchi zinazoendelea pamoja na suala la matajiri kutolipa kodi ipasavyo, limekuwa ni mjadala usiokwisha. Pamoja na mjadala huu, hakujawahi kufanyika utafiti wa kujua ni kwa kiasi gani masuala haya yamekuwa yakiathiri ulipaji kodi kwa wananchi wa kawaida.
Wiki iliyopita, kitabu kinachoelezea kuhusu kuondoa usiri kwenye eneo la sera za kodi za kimataifa na utoroshwaji wa mitaji kutoka nchi za Kiafrika ulifanyika jijini Dar es Salaam.
Mmoja kati ya waandishi wa kitabu hicho ambacho kwa lugha ya kigeni kinajulikana kama “Lifting the Veil of Secrecy, Perspective on International Taxation and Capital Flight from Afrika,” kilichoandikwa na Profesa Odd-Helge Fjeldstad, anasema mwanzoni maficho hayo ya fedha yalikuwa yakitumiwa na wahalifu.
Lakini kwa sasa maficho haya (Tax havens) yanatumiwa na watu binafsi, taasisi na makampuni ambayo yanafanya shughuli halali lakini wakati wanapata fedha kwa njia zisizo halali kama kukwepa kodi. Ili mamlaka za sehemu zao zisijue wanapata kiasi gani na kuwataka kulipa kodi huamua kuzificha katika sehemu hizo ambazo zina usiri wa hali ya juu,” anasema Prof. Odd.
Prof Odd kutoka taasisi ya CMI ya nchini Norway na ambaye amekuwa akifanya utafiti kuhusiana na masuala ya kodi hapa Tanzania kwa zaidi ya miaka 30, anasema tatizo hili lina athari kubwa kwa nchi za Kiafrika kwa kuwa fedha ambazo zingetumika kuwaletea maendeleo wananchi zinatoroshwa na wajanja wachache huku akisisitiza ushirikiano katika kutatua tatizo hili sugu.
Akizungumzia kuhusiana na masuala hayo, Profesa Honest Ngowi ambaye ni mhariri wa kitabu hicho na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mzumbe tawi la Dar es Salaam, anasema tatizo hilo lipo Tanzania na ni kubwa.
“Tunapozungumzia mabilioni ya Uswisi ndiyo mambo haya ya utoroshwaji. Pia katika Panama papers, tunaambiwa wapo Watanzania kadhaa. Ni tatizo ambalo madhara yake kwa Tanzania ni makubwa,” anasema.
Kuhusiana na jitihada mbalimbali zinazofanyika kukabiliana na tatizo hili hapa nchi ni anasema “juhudi mbalimbali zinafanyika. Hata hivyo, ili mafanikio yaweze kupatikana katika suala hili, juhudi za kitaifa tu hazitoshi. Hili ni tatizo la kimataifa na linahitaji juhudi za pamoja za kimataifa. Nchi ambazo ni za misamaha ya kodi (tax haven) kwa maana ya maficho ya fedha zinazotoroshwa lazima zitoe ushirikiano.
Hili limekuwa tatizo kwa sababu nchi hizi zinafaidi kutokana na fedha hizi. Hata hivyo, kuna juhudi za kimataifa za kutaka uwazi zaidi zinaendelea. Nchi kama Uswisi imetoa ahadi ya kutoa ushirikiano zaidi na Tanzania kwa mfano.”
Prof. Ngowi anasema kuna haja ya kufanya mambo mengi na hasa juhudi za pamoja za kimataifa; kufanya tatizo hili lifahamike na athari zake kwa nchi ni muhimu pia.
“Pamoja na haya, ni vizuri kujua kuwa hili ni tatizo la kimaadili vile vile. Viongozi wa dini wana nafasi kubwa katika kupunguza na hata kumaliza tatizo hili kwa kuwakemea na kuwafundisha waumini wao,” anaeleza.