- Ni kati ya waliodaiwa kuchoma kituo cha polisi Bunju
ANDREW MSECHU
IDARA ya Ustawi wa Jamii imejitosa kusaidia kumnasua kijana, Baraka Nkoko, aliyehukumiwa kifungo cha maisha kwa kuhusishwa kuchoma Kituo cha Polisi Bunju.
Akizungumza na Mtanzania jana, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Kinondoni katika Kata ya Bunju, Michael Mihayo, alisema ameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kubaini kwamba Baraka (21) alikamatwa akiwa na umri chini ya miaka 18, lakini alijumuishwa na watu wazima kinyume cha sheria.
“Tumebaini kwamba hata ndugu zake ambao walikuwa hawapo Dar es Salaam hawakujua nini cha kufanya katika kufuatilia suala lake hadi hukumu ilipotolewa.
“Kama wangejua wanaweza kusimamia na kufika katika ngazi husika na kumnusuru mapema na adhabu hiyo,” alisema.
Alisema baada ya kuamua kufuatilia walibaini kijana Baraka ambaye alikamatwa baada ya tukio hilo Julai 10, 2015, alizaliwa Januari 24, 1997.
Alisema hadi anakamatwa alikuwa ameishi katika eneo hilo la Bunju kwa wiki moja, kisha kuingia katika mikono ya polisi kupitia msako uliofanywa alfajiri ya Julai 11, 2015.
Mihayo alisema baada ya hukumu hiyo kutolewa ndipo walipopata vizuri taarifa zinazomhusu kijana huyo.
Alisema waliamua kufuatilia taarifa zake na kubaini kuwa ndugu zake wako Kigoma na walipoomba nyaraka za kuzaliwa wake, ikiwamo kadi ya kliniki na cheti cha kuzaliwa, walibaini kulikuwa na tatizo katika mawasiliano na utetezi tangu kukamatwa kwake.
“Baada ya kupata nyaraka hizo ambazo tayari tunazo, tumejiridhisha kuwa huyu alikuwa mtoto kwa kuwa alikamatwa akiwa chini ya umri wa miaka 18, kwa kuwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka 17.
“Tunadhani polisi walitumia vibaya mamlaka yao na inaonekana walitumia hasira.
“Pamoja na kubaini kwamba waliyemkamata alikuwa bado mtoto, walimweka mahabusu ya watu wazima kwa miaka minne baadaye.
“Kwa kweli tumeumizwa na utendaji wa wenzetu kwa sababu wanajua kabisa maelekezo ya sheria ya mtoto.
“Tunasikitishwa kwamba katika umri wa miaka 21 huyu kijana ambaye alikamatwa akiwa mtoto anahukumiwa kifungo cha maisha jela kwa sababu tu ya uzembe wao,” alisema.
Alisema pamoja na kosa hilo, walibaini kuwa katika mwenendo wa mashitaka, hakuna mtu aliyetoa ushahidi wa kuthibitisha kushuhudia ushiriki wake katika tukio hilo.
Alisema hiyo I kwa sababu wakati tukio hilo likitokea alikuwa akiuza duka ikiwa ni wiki moja tu tangu alipokabidhiwa kazi hiyo kwa ajili ya kumsaidia kujikimu.
Alisema tayari wameshafanya mawasiliano na Waziri wa Katiba na Sheria na wamepewa maelekezo ya hatua za kufuata, ikiwamo kuwasadia ndugu wa kijana huyo kumwandikia barua Waziri wa Sheria, Dk. Augustine Mahiga kulalamikia adhabu hiyo na kumwomba kusaidia haki ipatikane.
Alisema ofisi ya Ustawi wa Jamii pia inaendelea kutoa ushirikiano kuhusu suala la kijana huyo.
Aliwaomba Watanzania wenye mapenzi mema kujitokeza kwa ajili ya kusimamia rufani ya kesi hiyo ambayo bado haijawasilishwa rasmi Mahakama Kuu.
Kaka wa kijana huyo, Yoshua Selemani alisema pamoja na ugumu waliokutana nao tangu kijana huyo alipokamatwa, walilazimika kuendelea na mawasiliano wakiwa Kasulu, Kigoma, suala ambalo liliwawia vigumu kupata taarifa za mwenendo mzima wa kesi hiyo.
Alisema ugumu huo ulitokana na ukweli kwamba hawakuweza kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kijana huyo kutokana na hali ngumu ya uchumi waliyo nayo.
“Tulishtushwa baada ya kupata taarifa kuwa amehukumiwa kifungo cha maisha jela.
“Tumejitahidi kufuatilia suala la rufaa na kwa sasa tunaendelea na juhudi nyingine za kumwomba Waziri wa Sheria na Katiba atusaidie kuingilia hili. Tunashukuru msaada tunaopewa na ndugu zetu wa Ustawi wa Jamii hapa Bunju,” alisema.
Edward Luhomela ambaye ndiye aliyekuwa mwenyeji wa kijana huyo katika eneo la Bunju, alisema ataendeela kutoa ushirikiano katika hatua zote kwa kuwa siku ya tukio alikuwa na kijana huyo dukani.
Alisema wakati tukio hilo likitokea, kulikuwa na wateja wengi dukani na kijana huyo alikuwa akimsaidia kuwauzia mahitaji yao, hivyo hakuweza kutoka katika eneo hilo kwa kuwa alikuwa ndiyo ana wiki moja tangu alipopewa jukumu la kuuza duka hilo.
“Yule alikamatwa pamoja na mtoto wangu mkubwa wakiwa wamelala nyuma ya duka baada ya polisi kuvamia na kufanya msako wa nyumba hadi nyumba saa kumi usiku, baada ya tukio hilo lililotokea jioni. Baada ya hapo yaliyoendelea wanayajua wao polisi,” alisema.
Alisema kwa wakati huo kijana huyo alikuwa bado mdogo na alikuwa bado mgeni mjini kwa hiyo inaonekana alikuwa na woga mwingi hata alipokamatwa na polisi, kwa hiyo upo uwezekano wa kushindwa kujieleza na kwa kuwa hakupata usimamizi, waliamua kumtia hatiani.
Katika hukumu hiyo iliyotolewa Februari 22 mwaka huu, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba aliwatia hatiani washtakiwa wanane katika shtaka la sita la kuchoma moto Kituo cha Polisi Bunju.
Waliohukumiwa ni Yusuph Sugu (40), Juma Kozo (32), Rashid Liwima (29), Baraka Nkoko (23), Abuu Issa (36), Abraham Mninga (23), Veronica Ephraem (32) na Ramadhan Said (22).
Walikuwa wanakabiliwa na mashitaka sita likiwamo la kuchoma kituo hicho moto Julai 10, 2015. Walichoma kituo cha polisi ambacho ni mali ya umma jambo amballo ni kosa katika sheria.