NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM
MAMIA ya waombolezaji wamejitokeza katika uwanja wa Uhuru kuaga mwili wa Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, wakiwemo viongozi mbalimbali ambao wameeleza jinsi kiongozi huyo alivyowaibua.
Tofauti na juzi idadi ya waombolezaji jana ilikuwa kubwa na kuibua tafsiri kwa namna ambavyo kiongozi huyo aligusa maisha ya wengi.
Viongozi hao wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa na wilaya, wakuu wa taasisi walieleza jinsi kiongozi huyo alivyowagusa.
Wakizungumza uwanjani hapo kwa nyakati tofauti walimwelezea Mkapa kutokana na falsafa yake ya uwazi na ukweli pamoja na dhana nzima ya ugatuaji wa madaraka.
Mkuu wa Mkoa na Balozi mstaafu, Daniel Ole Njolay, alisema Mkapa ndiye aliyemfanya akafahamika kwa Watanzania baada ya kumteua mara mbili mwaka 1995 na 2000 kitu ambacho hakikutarajia.
Njolay ambaye aliwahi kuwa mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Balozi wa Nigeria alisema Mkapa alipenda mtu mchapakazi na anayesema ukweli.
“Aliniamini na kunipenda, aliniandikia barua ya pongezi ambayo ninayo mpaka sasa, kitu hasa kilichomgusa nilikaa Mwanza kwa miaka mitatu tu lakini ndani ya kipindi kifupi tuliasisi mpango wa kujenga shule za kata kabla hata serikali haijaanza.
“Tuliubadilisha mji wa Mwanza kutoka kuwa wa mwisho katika mashindano ya miji hadi ukawa wa kwanza, tuliijenga upya hospitali ya Sekouture na alipokuja kuizindua hakuamini.
“Mzee Mkapa alipenda umfanyie mambo mawili, umweleze ukweli na uchape kazi. Mambo haya mawili aliyapenda sana, usiwe ‘blaa blaa,” alisema Ole Njolay.
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema Mkapa alimtoa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) akiwa anafundisha Sheria na kumpa uenyekiti wa Chuo cha Uandishi wa Habari (TSJ) ambacho sasa ni Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC).
“Kuniopoa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kunipa wajibu wa kuongoza baraza la Chuo cha TSJ nilishtuka sana, nikaitendea haki nafasi hiyo,” alisema Dk. Mwakyembe.
Alisema pia mchango wa Mkapa katika tasnia ya habari ni mkubwa kwani aliamini katika umahiri na weledi.
“Alijua kwamba kazi ya kuhabarisha umma ni wajibu wa kikatiba ndiyo maana alisisitiza sana katika umahiri na weledi. Ametufanya wanahabari tujivunie kwamba tunaweza kuwa viongozi wan chi na uongozi uliotukuka,” alisema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela, alisema Mkapa atamkumbuka Mkapa kwani ndiye aliyemgharamia kusoma shahada yake ya pili UDSM.
“Alitoa mchango wa mimi kwenda ‘masters’ pengine ningeweza kuishia ‘degree’ ya kwanza lakini alitoa fedha nikaendelea kusoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,” alisema Shigela.
Alisema pia kiongozi huyo aliyeanzisha pia Jiji la Tanga atakumbukwa kwa dhana ya ugatuaji madaraka kutoka Serikali Kuu hadi Serikali za Mitaa ambayo imeleta mafanikio makubwa hasa ya uboreshwaji wa huduma za kijamii.
Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali Davis Mwamunyange, alisema wakati Mkapa anaingia madarakani yeye alikuwa Ofisa Mnadhimu makao makuu ya jeshi na kwamba ndiye aliyemteua kuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
“Taarifa za uteuzi wangu nilizipata kutoka kwa viongozi wangu, alinipa maelekezo turudi katika utaratibu wa awali wa kuwalea vijana ili wawe tayari kuilinda, kuitumikia na kuijenga nchi yao.
“Wananchi waliona kuna mapungufu ya vijana ambao hawakupitia JKT, walionyesha utovu wa nidhamu na ari ya utendaji kazi na uzalendo haikuwepo,” alisema Jenerali Mwamunyange.
Alisema pia Mkapa alikuwa kiongozi mahiri aliyefuatilia mambo kwa karibu na kwamba alikuwa na shauku ya kuleta maendeleo kwa haraka.
“Hata katika taasisi zetu za ulinzi na usalama alikuwa anapenda kujua tuna mapungufu gani ili tuweze kuwa na jeshi zuri na la kisasa, hivyo kila nilipopata nafasi ya kukutana naye, kusafiri naye alikuwa anauliza sana masuala ya jeshi kwa ajili ya kuliboresha,” alisema Jenerali Mwamunyange.
Akizungumzia namna Mkapa alivyomteua Balozi mstaafu wa Burundi, Francis Mndolwa, alisema; “Wakati nikiwa makao makuu ya jeshi nilikuwa mkurugenzi wa oparesheni, nilitembea sana kujua mipaka yetu inavyofanya kazi, mpaka wa Burundi ulikuwa na matatizo na ubalozi ulifungwa miaka kumi.
“Kwahiyo katika ripoti yangu ya kawaida tu wala isiyokuwa na malengo fulani nilieleza katika mipaka yote saba ilikuwa na mabalozi ila Burundi ulikuwa umefungwa.
“Rais Mstaafu Kikwete wakati huo akiwa waziri wa mambo ya nje alipokutana na Mkapa akamdokeza hilo na ‘process’ zikaanza za kutafutwa balozi…nikateuliwa,” alisema Balozi Mndolwa.
VIONGOZI WENGINE
Naye Naibu Waziri wa Elimu Zanzibar, Simai Mohamed, alisema; “Namfahamu Mkapa kwa sababu alifanya kazi na marehemu baba yangu miaka ya 1970, wiki tatu zilizopita nilipata bahati ya kwenda kumsalimia na tulikaa zaidi ya saa tatu kubwa aliloniambia ‘leadership’ ya vijana lazima uzalendo uwe mbele.
“Alikuwa mcheshi sana wakati nazungumza naye aliniambia nifunguke…nikamwambia funguka, alisisitiza umuhimu wa Muungano wetu na nitakuwa balozi mzuri wa kuwaambia wenzangu,” alisema Mohamed.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, alisema Mkapa alifanya kazi kwa bidii na uaminifu mkubwa na kwamba hakujilimbikizia mali.
“Mwaka 1995 nilikuwa darasa la tano na nilikuwa sina sifa ya kumpigia kura kumweka madarakani lakini mambo makubwa aliyoyafanya yanatufanya sisi vijana kujivunia uongozi wake,” alisema Chalamila.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, alisema Mkapa atakumbukwa kwa uthubutu wake, uzalendo na kuingia kwenye maamuzi magumu kwa manufaa ya taifa.
“Kila awamu ya Tanzania inakuja na changamoto za kihistoria ambazo hazifanani, zilizomkuta Mkapa alizisimamia kama mwanadiplomasia, alihudumu kwenye urais wake kwa ‘marks’ za juu kabisa.
“Ukibahatika kukaa naye hakuwa na ugumu katika kukupa uzoefu wake na alikuwa mcheshi sana,” alisema Malima.
WAFANYAKAZI
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, alisema wataendelea kumkumbuka Mkapa kutokana na alivyoishi na wafanyakazi vizuri.
Alisema Mkapa alianzisha utaratibu wa kukutana na wafanyakazi kila baada ya miezi mitatu na kusikiliza kero zao na kwamba kipindi chake pia Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ilitungwa na kuanza kutumika.
“Tucta tuna jengo kubwa la makao makuu tulipewa na Mkapa, tulimuomba akatukabidhi hivyo tunamkumbuka kwa jambo hilo.
“Aliimarisha uchumi wa nchi na watumishi tulianza kulipwa kila mwezi tofauti na ilivyokuwa kabla yake,” alisema Nyamhokya.
WAKUU WA TAASISI
Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya DCB, Godfrey Ndalahwa, alisema Mkapa ndiye mwanzilishi wa benki hiyo kwani alitoa agizo kwa halmashauri za manispaa jiji la Dar es Salaam kuianzisha kusaidia wananchi wa kipato cha chini ambao walikuwa wakitaabika kupata mikopo.
“Kupitia kilio cha wananchi wa Dar es Salaam hasa wa kipato cha chini alitoa agizo kwa halmashauri za manispaa kuanzisha benki na mpaka sasa inaendelea kusaidia wananchi,” alisema Ndalahwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei, alisema mafanikio ya benki hiyo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na Mkapa kutokana na ushirikiano aliokuwa akiutoa.
“Nilipokwenda CRDB alikuwa ananipigia anasema anataka iwe ni mfano wa ubinafsishaji, nilipotaka msaada wakati wowote alinipa. Sifa ya benki ilikuwa kwa sababu yake, kitu ambacho sitakaa nisahau alikuwa akitoa hotuba za kinadharia za kuijenga benki…heshima tuliyopata yeye alichangia zaidi,” alisema Dk. Kimei.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Dar es Salaam (DAWASA), Cyrpian Luhemeja, alisema Mkapa ndiye alianzisha mageuzi ya huduma za maji nchini baada ya kuivunja iliyokuwa mamlaka ya maji (NUA).
“Mwaka 1981 tulikuwa na mamlaka ya maji nchi nzima lakini kwa bahati mbaya haikufanikiwa, mwaka 1997 Mkapa aliivunja na kuanzisha mamlaka tatu za maji Dar es Salaam, Arusha na Tanga ambazo zilifanikiwa.
“Mwaka 2001 ikapitishwa sheria zianzishwe nchi nzima, mpaka sasa tuna mamlaka zaidi ya 65 na hali ya maji nzi nzuri, mjini upatikanaji wa maji ni asilimia 84,” alisema Luhemeja.
Aliwataka vijana kumuenzi Mkapa kwa kuacha tamaa ya maisha na badala yake wapende kujifunza kwangu kusoma kunaongeza maarifa.
“Wakati anachukua nchi nilikuwa ‘form four’ hivyo, kama vijana wakati ule tulianza kujifunza uongozi na ndiyo maana hadi leo mnaona Dawasa iko ‘stable’…vijana waache tama, tuna haraka, tupende kujifunza, ukisoma unapata maarifa na unapata uwezo wa kuongoza,” alisema.
ALIYECHAPA KITABU CHAKE
Mkurugenzi wa Kampuni ya Uchapishaji ya Mkuki na Nyota iliyochapisha Kitabu cha Rais Mkapa cha ‘My life my purpose’, Walter Bugoya, alisema kitabu hicho na hotuba zake kuna mengi ya kujifunza hasa kwa vijana na kushauri watu wakasome.
“Nimepata faraja kwamba wananchi wengi wanamjua na wanakumbuka alichofanya, wanafahamu ni hasara gani tunaingia kwa kumpoteza, alikuwa kama nanga fulani katika kuhakikisha amani, utulivu na maendeleo ya nchi yetu,” alisema Bugoya.
KUAGWA KITAIFA LEO
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa watashiriki katika shughuli za kuagwa kitaifa leo.
“Wale ambao wanaweza kufika Masasi wanakaribishwa, hatujazuia mtu yeyote ambaye anataka kwenda aende kwa usafiri ambao unaweza kumfikisha,” alisema Majaliwa.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas, alisema leo shughuli zitaanza kwa misa itakayofanyika Kanisa la Imakulata kisha mwili utaletwa uwanjani ambapo wananchi wataruhusiwa kuingia kuanzia saa 12:30 asubuhi.
Alisema viongozi wameandaliwa utaratibu ambapo kutakuwa na magari maalumu kuanzia saa 12:30 asubuhi katika ukumbi wa Karimjee hivyo hawatatakiwa kuja na magari yao.
Dk. Abbas alisema pia kutakuwa na hotuba mbalimbali za viongozi na kwamba baada ya shughuli ya kuaga mwili utasafirishwa kuelekea Masasi kwa ajili ya maziko.
Alisema kesho kutwa misa itaanza nyumbani kuanzia saa 2 asubuhi kisha shughuli za mazishi zitaanza kuanzia saa 4 asubuhi.
Katika uwanja huo ulinzi uliimarishwa na kabla ya kuingia tahadhari zote za kujikinga na corona zilizingatiwa ambapo kila mwananchi alitakiwa kunawa mikono kisha kupimwa joto la mwili na kukaguliwa.
Katika kuhakikisha ulinzi unaimarika kuna wakati askari polisi waliwachomoa baadhi ya watu waliokuwa kwenye foleni kisha kuwasachi na kuruhusiwa kuendelea kutoa heshima za mwisho.