MAKALA iliyopita ilijenga utangulizi wa uhusiano wa tabia zetu za utu uzima na maisha yetu tulipokuwa watoto. Tuliona nafasi kubwa tuliyonayo wazazi katika kuamua maisha ya baadae ya wanetu. Pamoja na nafasi hiyo tuliyonayo kama wazazi, mabadiliko ya kimaisha yanakwaza nia njema ya kuwa karibu na watoto wetu.
Harakati za kimaisha zimejenga umbali na watoto wetu hasa wanapokuwa wadogo. Umbali huu humfanya mtoto ajitafutie maarifa kwa mfumo wa kujitegemea. Matokeo ya kujitafutia maarifa hayo huria huotesha tabia zinazotustua wazazi tunaotamani watoto wawe wasikivu.
Tunapogundua tabia zisizotarajiwa kwa watoto, wazazi hujikuta tukilazimika kurejesha uhusiano kwa nguvu na watoto, uhusiano ambao hata hivyo watoto huwa hawana haja nao. Hali hii ya mmoja kutafuta uhusiano na asiyeutaka hufifisha mawasiliano kwa sababu sisi wazazi humwona mtoto kama mtu anayeasi mamlaka halali. Mtoto naye hutuona wazazi kama watu wanaojipendekeza na kumfuata fuata kwa sababu alipotuhitaji hatukuwa na muda naye.
Kwanza, tunahitaji kuongeza juhudi katika malezi. Malezi ndiyo fursa muhimu na ya pekee aliyonayo mtu yeyote, bila kujali nafasi yake katika jamii, kuweza kubadili kabisa maisha ya mtu mwingine. Kupitia malezi wazazi tunaweza kuweka alama ya kudumu itakayoathiri na kuongoza sehemu kubwa ya mitazamo, imani na tabia ya mtoto.
Tunaweza kuwekeza ipasavyo katika malezi kwa kupatikana na kuwasiliana na watoto tangu wanapozaliwa. Hatuwezi kuwasiliana na moyo wa mtoto pasipo kupatikana. Kuwa nao, kucheza nao, kutembea nao, kuzungumza nao na kufanya mambo yao pale tunapoweza, kunatusaidia tuweka alama njema ya kudumu katika maisha yao.
Ni kweli mfumo wa maisha ya sasa si rafiki kwa pendekezo hili. Najua tupo wazazi tunaondoka nyumbani kwenda kutafuta maisha ya baadae ya watoto wetu na kurejea usiku. Hata kama hatupendi iwe hivyo, lakini ndiyo hali halisi.
Wakati mwingine huwa nafikiria jambo hili. Kwamba nikiweza kupata saa moja tu kwa wiki nzima – kati ya saa 168 – sawa na dakika zisizozidi 10 tu kwa siku, nikakaa na mtoto mmoja na kumsikiliza yeye binafsi, wakati anapofikisha umri wa miaka 12/13 na kuanza kujiona mtu mzima, nitakuwa nimefanikiwa kukaa naye kwa muda wa siku 27 tu!
Maana yake wakati anaondoka nyumbani kwenda shule ya bweni kukutana na watu wengine wenye mitazamo tofauti na yake na wakati mwingine wenye ushawishi zaidi, nitakuwa nimekaa naye kwa takribani mwezi mmoja tu! Miaka mingine yote nilimwacha ‘ahusiane,’ ‘aelimishwe’ na televisheni na watu wengine nisiowajua! Ninapofika hapo, huwa najiuliza kama ni lazima niendelee kufanya malezi kuwa ‘part time.’ Kipi hasa chenye sifa ya kuwa kazi ya muda kati ya malezi na pilika za maisha? Je, siwezi kufanya maamuzi magumu kukabiliana na changamoto hii?
Pendekezo la tatu ni gumu. Kumpenda mtoto vile alivyo bila kujali alichokifanya. Kumpenda hata anapokuwa mkorofi na kukosa usikivu. Kumpenda hata anapokosea kama namna ya kumfanya ajenge imani na mimi. Kumfanya aelewe kwamba thamani yake, thamani ya moyo wake, ni kubwa kuliko uzito wa kosa lake. Hiyo haimaanishi, hata hivyo, kwamba sitamwadhibu. Nitaadhibu kosa lake nikielewa hatari ya kujeruhi moyo na hisia zake.
Kiboko cha kweli anachokihitaji mtoto ili kujenga tabia njema tangu akiwa mdogo ni upendo. Kumpenda tangu angali mtoto ndiyo silaha ya kumfanya ashawishike kutusikiliza. Kumpenda humfanya ajisikie hatia kutukosea. Mwanadamu anayekulia katika mazingira yanayomsikiliza huwasikiliza wengine akiwamo mzazi wake.
Mwandishi ni mwalimu wa Saikolojia katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Anapatikana kwa barua pepe: [email protected]Â Twita: @bwaya