25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

NHC ilivyowakomboa vijana wa vijiweni  

Kikundi cha vijana waliokuwa kijiweni wakiwa kazini baada ya kupatiwa mafunzo ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu na NHC.Na Sussan Uhinga, Tanga

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) inafanya kila linalowezekana kuhakikisha inasaidia jamii kwa kutekeleza miradi ya maendeleo hasa inayogusa sekta ya nyumba, afya, elimu pamoja na majanga ya mafuriko.

Katika utekelezaji wa sera yake ya kusaidia jamii, limeweza kusaidia vijana wapato 400 mkoani Tanga, waliowapatia mafunzo ya utengenezaji wa matofali ya kufungamana ya bei nafuu pamoja na mashine za kufyatulia.

Akizungumza na mwandishi wa makala hii, Meneja wa Shirika hilo mkoani Tanga, Isaya Mshamba, anasema wametumia takribani Sh milioni 36.4 katika kuendesha mradi huo.

Anasema lengo la shirika ni kuhakikisha linakuwa na miradi ya nyumba za gharama nafuu pamoja na kuwawezesha vijana kujiajiri hatimaye kujikwamua kiuchumi na kuzalisha ajira kwa wengine.

Mshamba anasema vijana waliopata mafunzo ya utengenezaji wa matofali hayo pamoja na mashine, watatumika katika ujenzi wa nyumba za gharama nafuu.

Anasema pamoja na mambo mengine, wanaunga mkono juhudi za serikali katika kuwaletea wananchi maisha bora, na kumfanya kila Mtanzania aweze kumudu gharama za ujenzi wa nyumba.

Kwa Mkoa wa Tanga, jumla ya vijana 400 wamepatiwa mafunzo ya kufyatua matofali pamoja na matumizi ya mashine zinazotumika katika kufyatua matofali hayo ya kufungamana.

Vijana hao wametoka katika wilaya zote nane za Mkoa wa Tanga, ambapo kila wilaya imetoa kikundi kimoja ambacho kilikuwa na vijana 10 walioteuliwa kutoka katika halmashauri zao.

“Mbali na kutoa mafunzo na mashine kwa vijana hao, pia tumetoa Sh 500,000 kama kianzio cha uendeshaji, ambapo fedha hizo tumewaingizia kupitia halmashauri,”anasema meneja huyo.

Kwa upande wao vijana ambao wamepata mafunzo hayo, wameishukuru NHC kwa kuwapatia mafunzo, vitendea kazi na fedha za kuanzia kufanya kazi.

Yohana Shedafa ambaye ni Mwenyekiti wa kikundi cha Jikomboe kilichopo jijini Tanga,  chenye jumla ya wanachama 10, anasema NHC imesaidia kuwaondoa katika umasikini.

Anasema wanatumia mashine hizo katika kujipatia kipato lakini pia kusaidia jamii ya Watanzania wenye kipato cha chini kuweza kujenga nyumba nzuri kwa gharama nafuu.

“Dada kama unavyotuona, hapa tupo kazini tumepata kazi kuna jamaa tunamjengea nyumba ya vyumba vitatu, sebule, jiko, choo pamoja na stoo huko maeneo ya Kange na tayari ameshatulipa fedha zetu,” anasema Shedafa.

Anasema mwanzo walikuwa wakiishi kwa kubahatisha, lakini mara baada ya kupata mafunzo hayo wameweza kujiajiri wenyewe na kusaidia familia zao.

Mbali na kufanya shughuli za ujenzi, pia wanauza matofali hayo ya kufungamana kwa gharama nafuu tofauti na matofali ya ‘block’ ambayo hutumia saruji nyingi na mchanga, na kwamba matofali ya kufungamana yanatumia udongo na saruji kidogo.

Naye Mwanachama wa Kikundi cha Mbavu Kazi, Yusuph Juma, anasema wao hujishughulisha na kufyatua matofali na kuuza kwa wananchi, huku wakiwajengea wananchi nyumba za gharama nafuu.

Anasema kama kijana anapata faraja kupata ujuzi lakini pia shukrani zake anazipeleka kwa serikali kupitia NHC kwa kuona umuhimu wa kuwasaidia vijana.

“Shirika limetusaidia mno, sasa tunajishughulisha hivyo hatuna sababu ya kukaa vijiweni wakati mashine tumepewa, mafunzo na fedha… kilichobaki ni kupiga kazi tu dada yangu,”anasema Yusuph.

Akizungumzia changamoto wanazokumbana nazo, Yusuph anasema tatizo lao kubwa linalowakabili ni soko la kuuzia matofali kwa kuwa jamii bado haijawa na uelewa juu ya ubora wa matofali hayo.

Anasema bado jamii hajafahamu kama kuna matofali ya kufungamana ambayo husaidia ujenzi kwa gharama nafuu.

“Tunatumia nguvu kubwa kushawishi watu kuhusu ubora wa matofali haya,” anasema.

Aidha, wameiomba Serikali kuweza kuvitambua vikundi hivyo vya vijana na kuvipa tenda za ujenzi kama kujenga madarasa na vyoo.

Naye Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, aliwaagiza viongozi wa halmashauri kuwasaidia vijana hao kwa kuwapa miongozo ya namna ya kujisajiri ili waweze kupata kazi kutoka serikalini.

Pia aliwaagiza wakurugenzi kuwatambua vijana hao ambao tayari serikali imeshawekeza na kuwapa vitendea kazi, wapewe kazi za ujenzi kwa kuwa gharama zao ni nafuu.

“Kuwatelekeza vijana hawa ni sawa na kupoteza rasilimali za serikali ambazo imewekeza kwao ili waweze kuisaidia jamii. Lakini pia mashine hizi zimenunuliwa ili zitumike hivyo wapeni kazi,” alisema Mabula.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles