30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

USHIRIKINA CHANZO CHA UBAKAJI, ULAWITI


Na ELIZABETH KILINDI-NJOMBE

Wananchi na jamii kwa ujumla mkoani Njombe, wametakiwa kuachana vitendo vya kishirikina vinavyosababisha kubaka na kulawiti kwa kigezo cha kujipatia utajiri.

Rai hiyo imetolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Njombe, Erasto Ngole katika kongamano la maadili la chama hicho Wilaya ya Wanging’ombe.

Ngole alisema kumekuwa na matukio mengi ya wanaume kuwabaka watoto wao ili kujipatia utajiri, jambo ambalo ni kinyume cha maadili ya kitanzania na mafundisho ya dini.

“Wanaume tunakokwenda siko, tumefikia hatua ya kuwabaka watoto wetu wa kike kwa kigezo cha kujipatia utajiri jambo ambalo siyo kweli, hakuna utajiri wa namna hiyo pia mmekuwa mkiwasababishia maumivu makubwa watoto hawa,’’ alisema Ngole.

Aliwataka watoto wa kike kijilinda na wanaume walaghai wenye nia mbaya ya kuwashawishi ili kuwabaka.

“Kuna wanaume wana lugha laini lakini yote hayo wanataka kuwarubuni ili kuwafanyia kitendo cha ubakaji. Msikubali, ukiona mtu anakwambia lugha tamu piga kelele, huyo ni mbakaji,’’ alisema Ngole.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Wanging’ombe, Stephano Kinyangadzi alisema wazazi wamekuwa chanzo cha kuporomoka kwa maadili kwa sababu wameshindwa kuwaonya watoto wao wanapokosea.

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM, Wilaya ya Wanging’ombe, Juma Nambaila alisema lengo la kongamano hilo ni kuzungumzia maadili ya Mtanzania sambamba na kuwahimiza wazazi kutimiza wajibu wao katika kuelimisha vijana au watoto wao.

“Tumefanya hivyo baada ya kuona mmomonyoko wa maadili umekithiri sana na endapo sisi kama wazazi tukiendelea kufumbia macho tatizo hili maana yake tutatengeneza Tanzania ambayo haitajulikana.

“Ndiyo maana katika kongamano hili tumewakalisha wazazi lakini pia na vijana kupitia makundi ya wanafunzi kuwaasa kwa sababu ndiyo wahanga wa tatizo hili,’’ alisema Nambaila.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles