MIONGONI mwa habari kubwa zilizopewa uzito katika gazeti la jana la MTANZANIA ni ile iliyokuwa na kichwa cha habari ‘Benki sita zafungwa ndani ya miezi 24’.
Msingi wa habari hiyo ni hatua iliyochukuliwa juzi na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutangaza kuiweka chini ya uangalizi Bank M, baada ya kubaini ina upungufu mkubwa wa ukwasi kinyume cha matakwa ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake.
Wakati BoT ikichukua hatua hiyo, tayari ilikwisharidhia muunganiko wa Benki ya Wanawake Tanzania (TWB), Benki ya Twiga Bancorp na Benki ya Posta kuwa benki moja itakayoitwa TPB.
Wakati huo huo ikiziruhusu Benki ya Wananchi ya Tandahimba (TACOBA) na Benki ya Ushirika ya Kilimanjaro (KCBL) kuendelea na biashara baada ya kutimiza masharti ya kuongeza mtaji.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa, uamuzi wa kuwekwa mabenki hayo chini ya uangalizi ulianza Oktoba, mwaka juzi, kwa Benki ya Twiga Bancorp, iliyokuwa ikimilikiwa kwa kiasi kikubwa na Serikali.
Januari mwaka huu, BoT ilizifutia leseni benki tano ambazo ni Covenant, Benki ya Wananchi Meru, Benki ya Efatha, Benki ya Wananchi Njombe, Benki ya Ushirika wa Wakulima wa Kagera na Benki ya Wananchi Mbinga, kwa kutokidhi vigezo vya uendeshaji.
Pamoja kwamba Gavana wa Benki Kuu, Profesa Florens Luoga juzi alikaririwa akisema sekta ya fedha ipo salama na mabenki yapo imara, Mei 19 mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei, alisema mazingira ya uendeshaji wa shughuli za kibenki yanatarajiwa kuendelea kuwa na changamoto katika miaka mitano ijayo, hasa katika eneo la ukuaji wa sekta ya fedha.
Kimei, ambaye alikuwa akizungumza na wanahisa wa benki hiyo katika mkutano uliofanyika Arusha, alisema changamoto hiyo imesababishwa na matakwa magumu zaidi ya udhibiti, kupungua kwa faida na ushindani mkali kutoka kwa washindani wa kibenki na usio wa kibenki.
Kimei alieleza jinsi sekta ya fedha inavyokabiliwa na wakati mgumu kuliko mwingine wowote katika miaka ya hivi karibuni, wakati akieleza hayo na jinsi walivyolazimika kupunguza wafanyakazi alimwaga machozi.
Jana katika uchambuzi wake, gazeti la MTANZANIA lilikariri gazeti moja la Kiingereza, likieleza namna faida inayotengenezwa na mabenki ilivyoshuka.
Gazeti hilo lilieleza jinsi faida inayotengenezwa na mabenki ilivyoshuka kutoka Sh bilioni 438 mwaka juzi hadi Sh bilioni 236 mwaka jana.
Tayari wachumi katika chambuzi zao wamegusa maeneo kadhaa ambayo wanaona ndio chanzo cha hayo yanayoshuhudiwa sasa.
Eneo mojawapo ambalo wanadai lilitarajiwa kusababisha sekta hiyo kupata kashikashi ni kuwapo kwa mikopo isiyolipika, ambayo baadhi yake ilitokana na udanganyifu uliokuwa unafanywa na wakopaji, wakati mwingine wakishirikiana na wafanyakazi wa benki wasiokuwa waaminifu.
Lakini pia wateja kuweka dhamana mali isiyo na thamani halisi, usimamizi dhaifu ndani ya mabenki nao umetajwa na wachumi hao kama chanzo kikuu cha misukosuko inayoshuhudiwa sasa.
Wachumi hao pia wameeleza kuwa, kufanya vizuri kwa mabenki kunategemea uimara wa uchumi.
Kwamba hali ngumu inaweza kusababisha mteja kushindwa kulipa mikopo yake.
Kwa sababu kama hizo, sisi tunadhani, waliopewa mamlaka wanapaswa kulitazama jambo hili kwa mapana badala ya kuishia kusema tupo vizuri.
Ushauri uliotolewa na wachumi tunadhani ni vyema ukazingatiwa kwa pande zote, ili kunusuru watu kuendelea kupoteza kazi zaidi, kwani tunaelezwa hadi kufikia Juni mwaka huu, tayari wafanyakazi 381 wamepunguzwa.