Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAMÂ
KITENGO cha usalama barabarani kinatarajiwa kuondolewa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kuundiwa mamlaka yake ili kukiimarisha zaidi imefahamika.
Hayo yalielezwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Mhandisi Joseph Nyamhanga alipokuwa akizungumza kwenye kongamano la Taasisi ya wadau wa barabara Tanzania (TARA).
Mhandishi Nyamhanga alisema Serikali inakusudia kuunda chombo au mamlaka ya kusimamia kitengo cha usalama barabara, hivyo kukiondoa chini ya Jeshi la Polisi.
Alisema mamlaka hiyo itakapoundwa itakuwa taasisi kiongozi wa masuala yote ya usalama barabarani na haitakuwa chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kama ilivyo sasa.
“Serikali inatambua kazi na juhudi kubwa zinazofanywa na polisi kitengo cha usalama barabarani lakini tutakuwa na sera ya kuwa na taasisi kiongozi. Hii itakipa nguvu chombo hiki ili kiwe imara kushughulikia masuala hayo.
“Chombo hiki kitajumuisha taasisi mbalimbali zikiwamo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, zimamoto na tutaangalia namna ya kuingiza wadau mbalimbali pamoja na vitu vya kitaalamu.
“Jeshi la Polisi litabaki na kazi moja ya kulinda raia na mali zake, lengo ni kuimarisha zaidi Baraza la Taifa la Usalama barabarani.
Akizungumza katika kongomano hilo, Mwenyekiti wa TARA, Mhandisi Abdul Awadhi aliiomba Serikali kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotokana na makongamano yao mbalimbali tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo.
“Sisi kama wadau wa barabara, lengo letu ni kushirikiana na serikali katika masuala yote yanayohusu usalama barabarani, hususani mapendekezo yote ambayo tumekuwa tukiyatoa kwa manufaa yetu sote.