TIMU mbalimbali zitakazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao, zinaendelea na harakati za kujiimarisha baada ya dirisha la usajili kufunguliwa Agosti mosi.
Kujiimarisha huko ni pamoja na kufanya usajili wa wachezaji wapya watakaozitumikia msimu ujao wa ligi hiyo na wakati huo huo kuachana na wengine ambao wameonekana kutokidhi matarajio.
Baadhi ya timu zimewatangaza wasiwazi wachezaji ambao tayari zimeafikiana na kusainiana mikataba.
Lengo la kusajili wachezaji wapya ni kutibu kasoro zilizojitokeza kwa timu hizo kwenye ushiriki wa Ligi Kuu msimu uliopita ili kuhakikisha zinafanya vizuri msimu ujao.
Ifahamike kuwa miongoni mwa timu 20 zilizoshiriki Ligi Kuu msimu uliopita, Simba ndiyo iliyofanikiwa kutwaa ubingwa , zilizosalia zipo zilizomaliza nafasi muhimu za juu, zilizomaliza msimu zikiwa katikati na nyingine nafasi za chini.
Zile zilizomaliza nafasi za chini nne zilishuka daraja moja kwa moja.
Zilizoshuka daraja ni Singida United, Lipuli, Ndanda, Alliance na Mbao.
MTANZANIA tunachukuwa fursa hii kuzipa pole timu zilizoshuka daraja. Kwa vile hakuna namna ambayo zinaweza kubadilisha ukweli huo zinapaswa kusahau yaliyopita na kwenda kujipanga upya tena mapema ili zifanye vizuri katika Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao na kurejea Ligi Kuu Tanzania Bara.
Hiyo ndiyo maana halizi ya ushindani kwani ilikuwa lazima bingwa wa Ligi Kuu apatikane na timu nyingine kushuka daraja ili kuziruhusu nyingine kutoka Ligi Daraja la Kwanza kupata daraja.
Ligi Daraja la Kwanza ina changamoti nyingi kwavile washiriki wake kila mmoja anakuwa na kiu ya kufuzu Ligi Kuu, hivyo basi timu zilizoshuka daraja kutoka Ligi Kuu zinapaswa kujipanga sawa sawa kama kweli zinataka kurejea Ligi Kuu.
Mfano mzuri ni msimu uliopita wa Ligi Daraja la Kwanza, haijashuhudiwa timu hata moja ikifuzu tena Ligi Kuu, baada ya kuwa imeshuka daraja msimu mmoja uliopita.
Hali hii inathibitisha jinsi gani Ligi Daraja la Kwanza ina ushindani mkubwa na ili ufanikiwe kufuzu Ligi Kuu unapaswa kupambana kweli kweli.
Tukirejea kwa hili la usajili wa wachezaji unaondelea kwa timu mbalimbali za Ligi Kuu, tunazikumbusha kuhakikisha zinasajili wachezaji watakazozipa tija .
Vitendo kama tulivyowahi kushuhudia misimu iliyopita, timu zinasajili wachezaji kwa kukomoana ni vizuri vikaepukwa.
Ni matarajio yetu timu zitasajili kwa kuzingatia mahitaji na kasoro zilizokuwa nazo msimu uliopita na kwa maelekezo ya makocha.
Hili likizingatia litasaidia kuufanya msimu ujao kuwa wenye ushindani mkubwa zaidi na kuifanya ligi yetu kuwa na mvuto.
Siku zote mashabiki wa soka wao wanachohitaji ni kuona burudani na hilo haliwezi kuonekana ikiwa timu nyingi ni dhaifu na chache ndio imara.
Ushindani ulioonekana msimu uliopita, tunatarajia utakuwa mkubwa zaidi msimu ujao kwakua hata zile timu zilizoonekana dhaifu zaidi zitakuwa zimejifunza kitu kingine kitakachozifanya kuja kivingine.