RIO DE JANEIRO, BRAZIL
MWANARIADHA raia wa Jamaica, Usain Bolt, ameahidi kuvunja rekodi ya mbio za mita 200 katika michuano ya Olimpiki leo nchini Brazil.
Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 29, anatarajia kukimbia leo kwenye fainali za mita 200 baada ya kung’ara kwenye mbio za mita 100 mwanzoni mwa wiki iliopita.
Mwaka 2009, nyota huyo aliweka historia ya kukimbia mbio za mita 200, huku akitumia sekunde 19.12, lakini mwaka huu ameweka wazi kuwa atahakikisha anavunja rekodi hiyo aliyoiweka.
“Nashukuru hadi sasa naendelea kung’aa kwenye michuano hii ya Olimpiki, ninaweza kuiwakilisha vizuri Jamaica pamoja na kujikusanyia medali mbalimbali.”
“Kesho (Leo), ni siku ya mwisho kwangu kuonesha ubora wangu katika mbio za mita 200, ninaamini hii itakuwa siku ya historia kwangu kwa kuwa nataka kufanya makubwa na kuweka historia mpya.
“Nakumbuka niliweka historia mwaka 2009, ambapo nilitumia sekunde 19.19, lakini katika fainali hii natarajia kufanya makubwa zaidi ya mwaka 2009.
“Kikubwa ni kusaka rekodi mpya, ninaamini naweza kufanya hivyo kutokana na maandalizi niliyoyafanya pamoja na muda ambao nimeupata kwa ajili ya kupumzika, hivyo natarajia kuvunja rekodi hiyo,” alisema Bolt.
Bingwa huyo hadi sasa amefanikiwa kutwaa medali tatu katika michuano hiyo na anaamini ana nafasi nyingine ya kuweza kuiwakilisha Jamaica kwenye mita 200.
“Katika mbio ambazo nazipenda sana ni mita 200, lakini sipendi kukimbia wakati wa asubuhi kwa kuwa ninakuwa bado nipo kwenye uchovu kidogo, ila ikiwa majira ya mchana nakuwa katika ubora wangu.
“Lakini bado nina furaha kwa kuwa nimefuzu kushiriki mita 200, hivyo bila ya kujali muda wa asubuhi nipo tayari kushindana na wapinzani wangu kwa kuwa nimekuwa nikishiriki mbio hizi mara kwa mara na ninafanya vizuri,” aliongeza.