MOSCOW, URUSI
SERIKALI ya hapa imetangaza kuendelea na vita ya kupambana na magaidi wanaoendesha shughuli zao nchini Syria ili kuhakikisha makundi yote yanaangamia.
Taarifa hiyo imetolewa jana mjini hapa na Msemaji wa Rais, Dmitry Peskov.
Alisema mashambhlizi dhidi ya magaidi ni vita endelevu.
“Mashambulizi yaliyopangwa dhidi ya magaidi nchini Syria yanaendelea na ni lazima tuendelee na mapambano,” Peskov aliwaambia waandishi wa habari.
Akijibu swali kuhusu shambulizi lililofanywa na Iran jana nchini Syria, alisema ni kutokana na kuwapo kwa vikundi vya wapiganaji haramu na wanajeshi wa kigeni wenye silaha nzito nchini humo.
“Suala hilo serikali imekuwa ikilisema wazi,” alisema Peskov na kuongeza kuwa makundi hayo ndiyo yamekuwa yakifanya vitendo vya kigaidi jambo ambalo alipaswi kufumbiwa macho.
Mapema jana Iran iliungurumisha makombora mashariki mwa Syria, ikiwalenga wapiganaji ambao walidai kuhusika na shambulizi lililotokea Septemba 22 na kusababisha vifo vya wanajeshi wapatao 29 waliokuwa wakifanya gwaride katika mji wa Ahvaz na kujeruhi watu wengine wapatao 60.