MOSCOW, Urusi
SERIKALI ya Urusi imeitaka Afghanistan na Jumuiya za Kimataifa kufanya uchunguzi wa mashambulizi ya ndege za Marekani Kaskazini mwa nchi hiyo na kusababisha vifo vya watu 10.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov amesema watakaobainika kusababisha vifo vya watu hao wasio na hatia wachukuliwe hatua za kisheria.
Taarifa ya waziri huyo imekuja baada ya mapema mwezi huu, ndege za Marekani kufanya mashambulizi katika Wilaya ya Chahar Dara iliyopo katika Jimbo la Kunduz nchini humo na kusababisha vifo vya watu 10 na kujeruhi wengine zaidi ya 20.
“Tunatoa wito kwa mamlaka ya Afghanistan na mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu ya kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hili na mashitaka yafunguliwe dhidi ya wahusika na hii itasaidia kuzuia matukio kama hayo siku zijazo,” alisisitiza waziri huyo.