SOCHI, Urusi
SERIKALI ya hapa imekanusha taarifa zilizosambaa katika vyombo mbalimbali vya habari zikidai kwamba, Rais Vladimir Putin, amemkasirikia mwenzake wa Syria, Bashar Assad, kuhusu tukio la ajali ya ndege yake aina ya Ilyushin-20 iliyotunguliwa kimakosa na vikosi vya nchi hiyo na kwamba ndio maana hakupokea simu yake.
Taarifa hiyo ilitolewa juzi mjini hapa na Msemaji wa Ofisi ya Rais, Dmitry Peskov, katika mkutano wake na waandishi wa habari na akasema kwamba habari hizo zimekuwa zikikuzwa na vyombo vya habari vya Israeli.
Msemaji huyo alisema kwamba, jambo hilo halihusiani na chochote na huku akisisitiza kuwa habari zilizosambaa ni za uzushi.
“Jambo hili halihusiani na chochote na huu ni uvumi ambao unasambazwa na vyombo vya Israel,” alisema msemaji huyo.
“Ikumbukwe kwamba, Rais Putin, tayari alishatoa kauli yake kuhusiana na ajali hii ambayo ilitokea katika mazingira ya kutatanisha na hivyo si kweli kwamba amemkasirikia mwenzake,” aliongeza Peskov.
Kauli ya msemaji huyo imekuja zikiwa ni siku chache baada ya Waziri wa Ulinzi wa nchi hii, Sergei Shoigu, kuishutumu Israeli kuhusu tukio hilo, akisema kuwa ndiyo inayotakiwa kubeba lawama kwa kupoteza ndege na wafanyakazi na huku akisema Serikali ya Moscow haitavifumbia macho vitendo kama hivyo bila kuchukua hatua.
Hata hivyo, pamoja na kutwishwa lawama, Israel, nao wamekuwa wakizitupia mpira nchi za Syria, Iran na kundi la Hezbollah na huku ikiahidi kutoa msaada wa kuifanyia uchunguzi ajali hiyo.