DA NANG, Vietna
SERIKALI ya Urusi imesema ipo tayari kushirikiana na Philippines katika masuala ya kiufundi kijeshi ili kupambana na magaidi.
Taarifa hiyo ilitolewa juzi na Rais wa Urusi, Vladimir Putin wakati alipokutana na mwenzake wa Philippines, Rodrigo Duterte.
Wawili hao wameshiriki mkutano wa nchi wanachama wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kiuchumi kwa nchi za Asia na Pasifiki (APEC) uliomalizika jana mjini hapa.
Wakizungumza pembeni mwa mkutano huo, Rais Putin alimkumbusha kiongozi mwenzake huyo jinsi alivyolazimika kukatisha ziara nchini mwake kutokana na matatizo ya ugaidi yaliyotokea Philippines na jinsi alivyomuomba washirikiane ili kuyatokomeza.
“Nakumbuka jinsi ulivyolazimika kukatisha ziara yako Urusi kutokana na shambulizi la ugaidi lililotokea nchini mwako na pia nakumbuka ulivyonieleza tunatakiwa kuanzisha ushirikiano ili kuwatokomeza magaidi wote,”alisema Rais Putin katika mazungumzo hayo.
“Ningependa kukupongeza kwa kuweza kuyafanya hayo yote,”aliongeza kiongozi huyo wa Urusi.
Rais Putin alisema kupamba na magaidi ni moja kati ya changamoto kubwa baina ya nchi hizi mbili.
Alisema katika kuheshimu makubaliano hayo inabidi wapange kuongeza ushirikiano zaidi hasa katika nyanja za ufundi kijeshi na pia katika masuala ya kiuchumi.
Alisema ingawa uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili kwa sasa hauridhishi, katika miaka ya hivi karibuni kumekuwapo na mwamko.