27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Urais roho juu CCM, Ukawa

napeslaaPatricia Kimelemeta na Aziza Masoud, Dar es Salaam
JOTO la kuwatangaza wagombea urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), linazidi kupanda huku kila upande ukimvizia mwenzake aanze kutangaza mgombea wake.
Hatua hiyo imekuja baada ya viongozi wa Ukawa katika mkutano wao na wanahabari kueleza mgombea wao atatangazwa Machi mwaka huu, lakini hadi sasa imepita miezi miwili bila kujulikana.
Wakati hayo yakiendelea ndani ya Ukawa, CCM nayo hadi sasa imeshindwa kueleza ni lini atapatikana mgombea wake pamoja na kutangazwa kwa hatima ya makada sita wa chama hicho wanaodaiwa kuanza kampeni kabla ya wakati.
Nchi ikiwa imebakiza miezi mitano ili kufika Oktoba utakapofanyika Uchaguzi Mkuu, hadi sasa vyama vya upinzani hasa vile vinavyonda Ukawa pamoja na CCM vimekuwa vikitegeana nani aanze kutangaza mgombea wake jambo ambalo linaelezwa limekuwa tofauti na miaka iliyopita.
Akizungumzia taratibu za uteuzi wa mgombea ndani ya CCM hivi karibuni alipokuwa akizungumza na MTANZANIA, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, alisema amekuwa akisikia maneno ya baadhi ya wanachama wakilalamika kuchelewa kuanza mchakato wa uteuzi wa majina ya wagombea ndani ya chama hicho wakati utaratibu bado haujafika.
“Maneno hayo nimekuwa nikiyasikia tukilaumiwa CCM kuchelewa kuanza mchakato wa uteuzi wa mgombea wa urais, lakini wanasahau kwamba muda wa uteuzi wa wagombea kwa taratibu za chama chetu bado haujafika,” alisema Nape.
Aliongeza hali hiyo pia ilijitokeza katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2005 na 1995.
Nape akatolea mfano wa uchaguzi wa mwaka 2005, ambapo alisema mgombea wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete aliteuliwa kuwania nafasi hiyo Mei 4, 2005.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, alisema muda wa kumtangaza mgombea wa urais ndani ya chama hicho bado haujafika.
“Kwa mujibu wa katiba ya chama chetu, muda wa kumtangaza mgombea wa nafasi ya urais ndani ya chama bado haujafika, jambo ambalo limetufanya hadi leo tushindwe kumtangaza mtu yeyote kuwania nafasi hiyo,” alisema Dk. Slaa.
Alisema Chadema inaendeshwa kwa misingi ya sheria na kanuni, na kwamba hawawezi kufuata utaratibu wa vyama vingine ili waweze kumtangaza mgombea wao.
Dk. Slaa alisema kutokana na hali hiyo, wanachama wa chama hicho wanapaswa kusubiri muda uliopangwa ili waweze kumjua mgombea wao.
“Chama kina utaratibu na misingi yake, hatuwezi kukurupuka kufanya uamuzi bila ya kufuata utaratibu uliopo ambao unatupa mwongozo ili tuweze kutekeleza majukumu yetu kisheria na kikanuni,” alisema.
Alisema hata kama CCM itaamua kumtangaza mgombea wa nafasi hiyo, wao bado wataendelea kusimamia misingi ya chama hicho inavyowataka.
Dk. Slaa alisema kila chama kinafuata utaratibu wake waliojiwekea, hivyo basi muda utakapofika watamtangaza mgombea wao.
“Hata kama CCM wataamua kumtangaza mgombea wao leo, kama sisi muda wetu bado hatuwezi kumtangaza,” alisema Dk. Slaa.

CUF waibuka
Akizungumzia uteuzi wa mgombea urais kupitia Ukawa, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Bara, Magdalena Sakaya, alisema kwa upande wao tayari wameshapendekeza jina la Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mgombea wa urais ambaye anasubiri kupitishwa jina lake na vikao vya uamuzi vya chama.
Alisema jina la Profesa Lipumba litakwenda kupambanishwa na wagombea wengine wanaowakilisha Ukawa ili kuweza kupata jina la mgombea mmoja ambaye atapambana na wagombea wa vyama vingine katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.
“Chama chetu kina jina moja la mgombea urais ambaye ni Profesa Lipumba ambaye atakwenda kupambanishwa na wagombea wengine wa Ukawa,” alisema Sakaya.
Alisema Ukawa wamekubaliana kufanya mkutano mwishoni mwa mwezi huu ili waweze kupitisha jina la mgombea wa nafasi hiyo.
“Tuna vikao vyetu mwishoni mwa mwezi huu ambapo kila chama kitatangaza jina la mgombea wake ili waweze kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kumpata mgombea mmoja atakayewakilisha Ukawa katika uchaguzi mkuu,” alisema Sakaya.

NCCR-Mageuzi na fomu
Akizungumzia uteuzi wa mgombea urais, Katibu Mwenezi wa Chama cha NCCR-Mageuzi, David Kafulila, alisema chama chao kimetoa fursa kwa wanachama wao kuchukua fomu kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu.
Alisema wanachama wataendelea kuchukua fomu hadi Mei mwaka huu ambapo watafanya kikao kujadili majina ya waliojitokeza kuwania nafasi hiyo.
“Hadi sasa aliyejitokeza kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya urais ni Dk. George Kahangwa ambaye anasubiri wanachama wengine waweze kujitokeza ili waingie kwenye mchujo,” alisema Kafulila.
Wakati CCM na Ukawa wakiendelea na mchakato wa kupata mgombea urais, tayari Chama cha Tanzania Labour (TLP) kimemtangaza Macmillan Lyimo kuwa mgombea wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles