22.9 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Urais CCM kazi ipo

M????????Na Waandishi Wetu

Membe: Hakuna anayenizidi

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ametangaza rasmi nia ya kuwania urais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kupitia CCM, huku akiahidi kupambana na ufisadi na rushwa kwa kuhakikisha sheria ya makosa ya rushwa inabadilishwa.
Akizungumza mjini Lindi jana, alisema ili nchi iweze kupiga hatua, akifanikiwa kuwa rais wa awamu ya tano, atabadili sheria ya kupambana na rushwa inayosema ‘mpokeaji na mtoaji wote wana makosa’.
Badala yake, alisema sheria hiyo itatoa nafuu kwa watoaji rushwa endapo wataripoti kutoa rushwa hizo.
Alisema watendaji wa Serikali na mawaziri watafukuzwa kazi hata kama walipelekwa mahakamani kwa rushwa na kushinda kesi kwa ushahidi kutojitosheleza.

AOMBA RUHUSA KWA NYERERE
Katika mkutano huo uliofanyika kwenye ofisi za CCM Mkoa wa Lindi, Membe alisema hivi karibuni Chifu Wanzagi wa Kabila la Wazanaki alimkaribisha Butihama na akatumia fursa hiyo kwenda kwenye kaburi la Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere kuomba ridhaa ya kuwania urais.
Alisema aliomba kuachiwa viatu hivyo ambavyo alihisi vinamtosha ikiwa wajumbe wa Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu wa CCM itawapendeza.

VIGEZO VYA CCM
Membe alisema CCM imeweka vigezo 13 vya kumpata mgombea urais, kati ya hivyo suala la uadilifu likiwa miongoni mwake.
“Mimi nina uadilifu wa kuzaliwa ambao katu siwezi kuuacha ndugu zangu Watanzania,” alisema Membe.
Alisema yeye pekee ndiye mwenye vigezo stahiki kama vilivyowekwa na chama chake.
“Nimetafakari kwa kina na nimewachambua wagombea wote, nimejilinganisha na wenzangu, lakini hakuna anayenizidi,” alisema.

VIPAUMBELE

Afya
Membe alisema: “Kazi kubwa sana imefanywa na Rais Kikwete, nami ninataka kusema ikiwa nitachaguliwa kupeperusha bendera ya CCM, nitahakikisha ujenzi wa zahanati na vituo vya afya unafanyika kwa kuwafuata wananchi walipo,” alisema.

Ajira
Alisema suala la ajira kwa vijana ni moja ya kipaumbele chake ambapo atahakikisha Tanzania inakuwa nchi ya uchumi wa viwanda vitakavyoweza kuzalisha ajira.

Ulinzi na Usalama
Alisema ataitumia elimu yake ya masuala ya ulinzi na usalama katika kukomesha vitendo vya kigaidi, dawa za kulevya pamoja na mapambano dhidi ya wahalifu nchini. Pia atahakikisha anapambana na kukomesha mauaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).

Muungano
Membe alisema hatokuwa tayari kuona watu wakileta chokochoko na kuuchezea Muungano wa kihistoria wa Tanganyika na Zanzibar. “…Tutawashughulikia kwa mujibu wa sheria…,” alisema.

Haki za wanawake
Membe alisema katika Serikali yake atahakikisha haki inatolewa kwa wanawake katika uongozi, huku akitoa onyo kwa wanaume wanaolewa na kwenda kuwapiga wake zao.

Elimu
Akizungumzia sekta ya elimu, alisema anashangazwa na watu wanaokebehi kazi iliyofanywa na marais waliotangulia, na kuongeza kuwa atahakikisha anamalizia pale walipoishia kwa kujenga chuo cha ufundi stadi kwa kila wilaya nchini.
“Tunahitaji vijana waende katika vyuo vya ufundi vya VETA ambapo hivi sasa viwanda vingi vinahitaji wasomi waliopita kwenye vyuo hivi ili kuimarisha ajira,” alisema.

Uchumi
Alisema ataimarisha uchumi kwa kuhakikisha anaishirikisha sekta binafsi ambayo itakuwa na kazi ya kulinda viwanda vya ndani.

Utawala Bora
Alisema moja ya mambo atakayoanza nayo ni kuhakikisha anaimarisha utawala bora kwa kubadili kipengele cha sheria cha anayetoa na anayepokea rushwa wote kutokuwa wakosaji.
“Ninachotaka kusema hapa ni kwamba jambo ambalo linaniudhi sana ni pale mtu anayetoa taarifa ya rushwa na kugeuka ni sehemu ya mkosaji, hili si sawa na hiki kipengele tutaanza nacho.
“Kuna watu wanawalazimisha wengine kutoa rushwa na asivyofanya hivyo eti watamshughulikia, nipeni mimi Membe mtakuwa salama kabisa, ndiyo maana hata kundi
langu linalonizunguka hakuna hata mtu mmoja mwenye tuhuma na wote tupo safi kabisa,” alisema Membe.

Kuwalinda wastaafu
Alisema katika kipindi chake cha uongozi hatokuwa tayari kuona viongozi wastaafu wakisumbuliwa na watu na atakayejaribu kufanya hivyo atakiona.

KOMBORA KWA UKAWA
Membe alitumia mkutano huo kurusha vijembe kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kusema kazi yao ni kulalamika kuibiwa kila mwaka huku wanaogombea ni walewale ambao wanashiriki uchaguzi kila unapofika na kudondoka.
“Mwaka 1995 walipigwa, hivyo hivyo 2000 na 2010 na sasa 2015 watagaragazwa halafu unasema tu umeibiwa, hawa watu namna gani, na CCM ikitokea wakaniteua mimi, na upinzani ndiyo utakufa kabisa nawaambia,” alisema.

 

Sigombei kugombana na watu – Makamba

NAIBU Waziri wa Mwasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, amesema hagombei urais ili kugombana na watu bali anagombea nafasi hiyo apambane na matatizo ya watu.
Amesema CCM itakuwa salama chini ya uongozi wake endapo akiteuliwa kugombea urais kupitia chama hicho.
Akitangaza nia ya kuwania nafasi hiyo kupitia chama hicho jijini Dar es Salaam jana, aliainisha vipaumbele vitano ambavyo atavifanyia kazi katika Serikali atakayounda ikiwa na mawaziri 18 tu.
“Kugombea siyo kugombana na ndiyo sababu sijamtukana mtu katika hotuba yangu, sigombei kugombana na mtu bali kupambana na matatizo ya wananchi,” alisema January.
January ambaye aliambatana na baba yake, Yusuf Makamba, alisema ataisuka Tanzania mpya kwa kubadili mfumo wa Serikali uliopo aliosema ndiyo tatizo linalosababisha mambo mengi kutokwenda sawa.

VIPAUMBELE
Alisema kipaumbele chake cha kwanza itakuwa ni kukuza kipato cha mwananchi mmoja mmoja, hali itakayofanya wote wawe na nguvu sawa ya kiuchumi.
January alisema katika kukuza uchumi wa kuendesha nchi, ataangalia uwezeshwaji wa sekta za uvuvi, ufugaji na viwanda.
“Falsafa yetu ni kwamba yeyote anayevuja jasho lazima afaidike na jasho lake, mtu asiye na shughuli apewe shughuli labda asitake mwenyewe,” alisema.

HUDUMA BORA ZA UHAKIKA
Alisema kipaumbele cha pili kitakuwa kuhakikisha huduma bora na za uhakika zinapatikana kwa wananchi wote.
“Huduma bora zinajumuisha upatikanaji wa uhakika wa maji safi na salama, huduma bora za afya ambayo bado ni changamoto, tutaendelea kuitazama sekta hii kwa kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na bima ya afya na anapata matibabu bila kujali kipato chake.
“Ukiritimba katika Bohari ya Dawa kwenye usambazaji wa dawa, haya yote yanatokana na mfumo mbovu wa kusambaza dawa ambao Serikali yangu nitakayounda itauondoa,” alisema.

UTAWALA BORA NA SHERIA
January alisema Tanzania inaongozwa kwa misingi ya sheria, lakini Watanzania wengi hawapati haki zao mahakamani.
“Ubadhirifu wa mali za umma hautavumiliwa, Rais Jakaya Kikwete aliweka mfumo mzuri wa kuweka hadharani ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), na kujadiliwa.
“Serikali yangu itakwenda mbali zaidi ambapo baada ya kujadiliwa viongozi ambao wameguswa kesho yake ni polisi kisha mahakamani ili sheria ifuate mkondo wake,” alisema.

USIMAMIZI WA UCHUMI
Katika suala la usimamizi wa uchumi, January alisema ataanzisha Baraza la Taifa la Uchumi litakalosimamiwa na wataalamu katika kudhibiti mfumumo wa bei na kushuka kwa uchumi.
Alisema kwa kuwa Serikali ndiyo msimamizi mkuu wa kila kitu, Serikali yake itaweka sheria itakayowezesha manunuzi yote ya umma kufanywa na kampuni ndogo zitakazoendeshwa na vijana na kinamama.
“Tutatoa motisha mpya ya kikodi kwa mwajiri atakayewezesha kuajiri, atapata motisha ya punguzo la kodi kwa kila ajira tano au zaidi atakazotoa.
“Tutachukua hatua za muda mfupi ili kuwezesha biashara ya viwanda na sekta ya nyumba ambayo inachangia kwa asilimia kubwa kuipatia Serikali fedha ambapo tutapunguza bei ya vifaa vya ujenzi na kuongeza miradi ya ujenzi na kutoa ajira hizo kwa makandarasi wazalendo,” alisema.
Aidha, kwa upande wa wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama machinga, alisema ndani ya mwaka mmoja watapatiwa sehemu zao za uhakika.

KULINDA AMANI NA UMOJA WA NCHI
Kipaumbele cha tano ametaja kuwa ni amani, umoja na usalama wa mali na maisha ya Watanzania ambazo ni tunu za urithi ulioachwa na waasisi wa taifa hili.
“Nitaanzisha Jukwaa la Rais na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Jumuiya ya Wakristo Tanzania (CCT) na Baraza la Waislam Tanzania (BAKWATA) litakalokutana kila miezi miwili kujadili na kupanga mikakati ya kuendeleza amani, umoja, upendo na maadili ya jamii,” alisema.
Alisema atahakikisha anachukua hatua mpya za kuimarisha Muungano na kuupatia uhalali mpya na wa ziada miongoni mwa Watanzania.

UTEKELEZAJI
Alisema ataipa nguvu Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), ili iweze kutokomeza tatizo hilo nchini kwa kushirikiana na mahakama maalumu ya rushwa atakayoiunda.
“Tutaiwezesha Takukuru kuwa na mamlaka kisheria ya kuwashitaki watuhumiwa wa rushwa moja kwa moja mahakamani. Pia, tuanzishe Mahakama Maalum ya Uhujumu Uchumi.
“Pia tutaanzisha Kurugenzi ya Uchunguzi na Mashtaka ya Uhujumu Uchumi.
“Katika uchaguzi huu, tunayo fursa ya kuanza safari ya kumaliza tatizo hili,” alisema.
Alisema Serikali yake itafufua viwanda vya katani na korosho nchini ili kuweza kuongeza ajira na kusaidia wakulima.
Makamba alisema uchumi wa Tanzania hautategemea mikopo na atahakikisha deni la taifa linapunguzwa kwa kutumia maliasili zilizopo nchini.
Katika hali nyingine, alisema anaamini kiongozi bora huchaguliwa na Mungu.
Kuwapatia motisha walimu na mishahara mizuri ili kuhakikisha elimu inaboreka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles